Nenda kwa yaliyomo

Fainali ya Kombe la Dunia la FIFA 2022

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Fainali ya Kombe la Dunia la FIFA la 2022 ilikuwa mechi ya mwisho ya Kombe la Dunia la FIFA la 2022, toleo la 22 la mashindano ya FIFA kwa timu za kitaifa za mpira wa miguu za wanaume. Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Lusail mjini Lusail, Qatar, tarehe 18 Desemba 2022, Siku ya Kitaifa ya Qatar, na ilishindaniwa na Argentina na mabingwa watetezi Ufaransa . Huku ikiwa na rekodi ya kutazamwa kwenye televisheni na watu bilioni 1.5, fainali hiyo imekuwa ni mojawapo ya matukio ya michezo yaliyotazamwa na watu wengi zaidi katika historia. [1]

Michuano hiyo ilijumuisha timu 32 ikiwemo wenyeji Qatar na timu nyingine 31 ambazo zilijipatia nafasi kupitia hatua za kufuzu, zilizoandaliwa na mashirikisho sita ya FIFA . Timu hizo zilichuana katika hatua ya makundi, ambapo timu 16 bora zilifanikiwa kufuzu hatua ya mtoano. Katika safari yao kuelekea fainali, Argentina walimaliza wa kwanza Kundi C licha ya kupoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Saudi Arabia kwa mabao 2-1. Baadaye waliwashinda Meksiko na Poland kwa mabao 2-0 kila mmoja. Katika hatua ya 16 bora waliifunga Australia kwa mabao 2-1, kisha wakawatoa Uholanzi kwenye robo fainali kwa mikwaju ya penalti baada ya mechi kuisha 2-2 katika muda wa ziada, na hatimaye wakaifunga Kroatia kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa nusu fainali. Kwa upande mwingine, Ufaransa ilimaliza wa kwanza katika Kundi D wakishinda michezo miwili na kupoteza moja (ushindi wa 4-1 dhidi ya Australia, ushindi wa 2-1 dhidi ya Denmark, na kupoteza 1-0 dhidi ya Tunisia ), Katika hatua za mtoano, waliifunga Poland 3-1 katika hatua ya 16 bora, Uingereza 2-1 kwenye robo-fainali, na Morocco 2-0 katika nusu-fainali. Fainali hiyo ilihudhuriwa na watazamaji 88,966 na kuchezeshwa na mwamuzi Szymon Marciniak.

  1. "One Month On: 5 billion engaged with the FIFA World Cup Qatar 2022". FIFA.com. Fédération Internationale de Football Association. 18 Januari 2023. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 18 Januari 2023. Iliwekwa mnamo 22 Mei 2023.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)