Nenda kwa yaliyomo

Ernst Dammann

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ernst Karl Alwin Hans Dammann (alizaliwa Pinneberg, Holstein, tarehe 6 Mei 1904 – alifariki Pinneberg, tarehe 12 Julai 2003[1]. Pamoja na Walter Markov, anachukuliwa kama mmoja wa waanzilishi wa Taaluma za Kiafrika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (Ujerumani Mashariki - DDR). Akiwa mwanafunzi wa Carl Meinhof na mfuatiliaji wa Diedrich Westermann, ni sehemu ya "wimbi la pili"[2] la Wajerumani waliobobea katika Taaluma za Kiafrika.

Dammann alikuwa mwanazuoni wa lugha za Kiafrika na mmisionari huko Tanga, Tanzania. Hata hivyo, alikuwa mwanachama mwanzilishi wa chama cha Nazi (NSDAP), na kazi zake za kisayansi zinakosolewa kwa kuingiliwa na itikadi za ubaguzi wa rangi.[3] Licha ya mapungufu hayo, tafiti zake bado ni msingi muhimu kwa ajili ya usomaji wa Kiswahili cha kale.

Elimu na kujiunga na Chama cha Nazi

[hariri | hariri chanzo]

Dammann alilelewa katika jimbo la Schleswig-Holstein. Mama yake alifariki akiwa mdogo mwaka 1916, na baba yake alikuwa amekwenda Afrika mwaka 1908 kufanya kazi nchini Tanzania kwa muda wa miaka mitatu kwenye shirika la treni la Central Line[2]. Alisoma katika shule ya sekondari ya Christianeum[4] huko Hamburg, kisha akaendelea na masomo huko Kiel na katika Chuo Kikuu cha Hamburg.

Alipata udaktari wake (PhD) huko Kiel mwaka 1929 na kupewa daraja la upadri mwaka 1930[2]. Kulingana na Ernst Klee, alujiunga na Chama cha Nazi mwaka 1931[1], ingawa vyanzo vingine vinataja tarehe 1 Agosti 1933. Meinhof, Dammann na wengineo walikuwa na mitazamo ya kibaguzi iliyojikita katika nadharia za karne ya 19 kuhusu ubora wa mbari za Ulaya, hasa Waarya, wakiamini kuwa "uduni" wa Waafrika ulijidhihirisha katika fasihi na lugha zao.

Kazi barani Afrika na maisha ya baadaye

[hariri | hariri chanzo]

Kati ya mwaka 1933 na 1937, alifanya kazi kama mmisionari wa Kilutheri huko Tanga kwa ajili ya jamii ya wakoloni wa Kijerumani[5]. Alitembelea Lamu, ambapo (kwa msaada wa mke wake, Ruth) alikusanya mashairi[2] ya mshairi wa Kiswahili Zahidi Mngumi; mkusanyiko huo unatajwa kuwa kamili zaidi kuhusu kazi za Mngumi[6]. Dammann alikuwa kiongozi wa tawi la kigeni la Chama cha Nazi (Landesgruppenleiter) nchini Tanganyika[7]. Utiifu wake kwa Chama cha Nazi ulizidi nguvu imani yake ya Kikristo, na mgogoro ukazuka kati yake na Misheni ya Bethel. Akaondolewa kazini kwenye misheni baada ya 'kujivunjia heshima'.[7]

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, alitumikia jeshi huko Denmark na kisha Tunisia, ambapo alikamatwa na majeshi ya Marekani na kuwa mfungwa wa vita kuanzia 1943 hadi 1946 nchini Marekani na baadaye Uingereza.

Mwaka 1957, aliteuliwa kuwa mkuu wa idara ya lugha na utamaduni wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Humboldt mjini Berlin. Mwaka 1961, wakati Ukuta wa Berlin ukijengwa, alitoroka kutoka Ujerumani Mashariki (RDA) na kwenda Ujerumani Magharibi (RFA), ambapo alipata uprofesa katika Chuo Kikuu cha Marburg mwaka 1962.

Utafiti na Mirathi

[hariri | hariri chanzo]

Dammann alifundisha lugha nyingi za Kiafrika, ikiwa ni pamoja na Kiswahili, Kizulu, Kiherero, Kinama na Kioromo. Licha ya kuwa mfuasi wa itikadi za ubaguzi wa rangi hadi mwisho wa maisha yake[5], kazi zake zimekuwa na umuhimu wa kipekee kwa namna isiyotarajiwa[2].

Kweli kinzani: Itikadi ya Kinazi dhidi ya kutambulika kwa fasihi ya Kiswahili

[hariri | hariri chanzo]

Utafiti wa Dammann huko Lamu katika miaka ya 1930 ulileta aina ya kweli kinzani ; ingawa alikuwa na nia ya kibaguzi, kazi yake ilichangia katika kueneza maarifa ya fasihi ya Kiswahili[8] duniani kwa kukusanya mkusanyiko mkubwa wa maandishi ya Kiamu. Kwa maana nyingine, data za kilugha zilizopatikana kupitia utafiti wake zilikuja kusaidia baadaye katika kutambulika kwa utamaduni wa Kiswahili kama utamaduni uliostawi na wenye kiwango cha juu cha kifasihi, kifalsafa na kiteolojia[9]. Jambo hili linapingana moja kwa moja na itikadi ya kibaguzi ya Kinazi iliyokuwa ikidharau uwezo wa kiakili wa Waafrika.

Hata hivyo, ushiriki wa Ernst Dammann katika harakati za Kinazi[7] uliathiri namna alivyochanganua lugha za Kiafrika. Kwa kuchambua ushairi wa Kiswahili (hasa Utenzi) kupitia kigezo cha mizani ya ushairi wa kale wa Kijerumani[10], Dammann anadhaniwa kujaribu kufanya utamaduni wa Kiswahili kuonekana kama ni wa Kijerumani[9]. Hatua hiyo ilifanana na mbinu za wasomi wa Ahnenerbe (Urithi wa Wahenga, taasisi ya utafiti ya SS wenye msimamo mkali zaidi)[11]: kwa kujaribu kuonyesha uhusiano wa kale kati ya maandiko ya Kiswahili na asili ya Kijerumani, alilenga kuhalalisha madai ya utawala wa Nazi (Dola la Tatu) kurejesha koloni la zamani la Afrika Mashariki ya Kijerumani (Deutsch-Ostafrika). Katika mtazamo huo wa kiitikadi, kupora na kumiliki utamaduni wa "Mwananchi" kulitumika kama kisingizio cha kukamata ardhi iliyowasilishwa kama sehemu ya urithi wa Kijerumani.

Maandishi yake (Baadhi)

[hariri | hariri chanzo]
  • Dichtungen in der Lamu-Moundart des Suaheli. Hamburg 1940.
  • Die Religionen Afrikas. Stuttgart 1963.
  • Ndonga-Anthologie. Berlin 1975.
  • 70 Jahre erlebte Afrikanistik: ein Beitrag zur Wissenschaftsgeschichte. Berlin 1999.
  1. 1 2 Klee, Ernst (2003). Das Personenlexikon zum Dritten Reich wer war was vor und nach 1945?. Internet Archive. Augsburg Weltbild. ISBN 978-3-8289-0569-6.
  2. 1 2 3 4 5 Jungraithmayr, « Ernst Dammann (1904–2003) », Zeitschrift der Deutschen Morgenländischen Gesellschaft, vol. 157, no 1,‎ 2007, 1–6
  3. Sara Pugach, Africa in Translation: A History of Colonial Linguistics in Germany and Beyond, 1814–1945, University of Michigan Press, 2012 (ISBN 9780472027774, uk. 187
  4. Ernst Dammann, Beiträge aus arabischen quellen zur kenntnis des negerischen Afrika, H.H. Nölke, 1929
  5. 1 2 Arno Sonderegger, Racisms Made in Germany, Münster, LIT Verlag, 2011, 123–144. (ISBN 9783643901255), « Racist Fantasies: 'Africa' in Austrian and German African Studies »
  6. Biersteker, Ann; Shariff, Ibrahim Noor (1995-04-30). Mashairi ya Vita vya Kuduhu: War Poetry in Kiswahili Exchanged at the Time of the Battle of Kuduhu (kwa Kiingereza). MSU Press. ISBN 978-0-87013-894-2.
  7. 1 2 3 Poewe, K. (2001). Politically compromised scholars, or what German scholars working under missions, National Socialism, and the Marxist-Leninist German Democratic Republic can teach us. American Anthropologist, 103(3), 834–837.
  8. Vierke, Clarissa (2011). On the Poetics of the Utendi: A Critical Edition of the Nineteenth-century Swahili Poem "Utendi Wa Haudaji" Together with a Stylistic Analysis (kwa Kiingereza). LIT Verlag Münster. ISBN 978-3-643-80089-3.
  9. 1 2 Mathieu Roy pamoja na Mahmud "Mao" Ahmed Abdull ibn Kadir, KIAMU, archipel de Lamu (Kenya): Analyse phonétique et morphologique d'un corpus linguistique et poétique (French Edition), Saarbrücken, PAF, 2013, 317 p. (ISBN 9783838179438, SUDOC 188249419, Une germanisation de l'Utenzi?, 47-51
  10. ROY, Mathieu, 2014, Ushairi wa Kiswahili kuanzia karne ya 16 mpaka karne ya 20, Slaidi za mhadhara, Open University na DL2A Buluu Publishing, Dar es Salaam, Tanzania.
  11. Johann Chapoutot, La révolution culturelle nazie (Mapinduzi ya Kiutamaduni ya Kinazi), Paris, Gallimard, 2022 (ISBN 978-2-07-299248-3, BNF 47155291)

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]