Nenda kwa yaliyomo

Elise Blenker

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Elise Blenker (1824 - 1908[1]) alikuwa mke wa Louis Blenker, afisa wa mapinduzi wa Kijerumani wa miaka ya 1848/1849. Elise pia alishiriki kikamilifu katika matukio mbalimbali ya Mapinduzi ya Kijerumani ya 1848–49 katika maeneo ya Palatinate na Baden.

Maisha nchini Ujerumani

[hariri | hariri chanzo]

Elise Blenker alizaliwa katika mji wa Aue katika jimbo la Saxony mashariki mwa nchi ya Ujerumani. Alikuwa binti wa mchungaji wa Kiinjili, Johann Christian. Mwaka 1843 aliolewa na aliyekuwa afisa wa Uhlan, Louis Blenker, katika Worms ndani ya Hesse. Wakati huo Louis alikuwa akiendesha biashara ya kuuza divai mjini Worms. Mwaka 1848 alikua kanali katika wanamgambo wa Worms. Wakati mapinduzi ya 1848 yalipozuka Baden, Elise aliungana na mume wake katika kampeni zake,huku wakati mwingine akiwa amevaa sare za kijeshi .[2] Wakati huu Elise alikutana na wanawake wengine wa kimapinduzi, wakiwemo Kathinka Zitz-Halein, Emma Herwegh, Amalie Struve na Mathilde Franziska Anneke. Tarehe 20–21 Mei Elise na mume wake walishiriki katika shambulio lisilofanikiwa dhidi ya Landau. Pia alicheza jukumu muhimu katika uporaji wa Ngome ya Eberstein huko Baden.

Maisha nchini Marekani

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya mapinduzi kuzimwa, Elise alilazimika kukimbia pamoja na mume wake, kwanza kwenda Uswisi, na kisha mwaka 1850 kwenda Marekani.[3] Kwa msaada wa baba yake, Elise na Louis walijenga maisha mapya katika Kaunti ya Rockland, ambako waliendesha shamba la maziwa.[4] Kwa pamoja Elise na Louis walikuwa na watoto wanne (binti watatu na mvulana mmoja).

Baada ya kuanza kwa Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani mwaka 1861, Louis aliunganisha kikosi cha wanajeshi wa kujitolea jijini New York , ambamo alikuwa kanali.[3] Kwa ushujaa wake katika Bull Run alipandishwa cheo kuwa brigedia jenerali wa wanajeshi wa kujitolea.[3] Mwezi Oktoba 1863 Louis alifariki kutokana na majeraha aliyopata alipokuwa na kikosi chake huko Warrenton, Virginia,[3] akimwacha Elise na watoto wao katika umaskini.[2] Elise hakuweza kugharamia mazishi yake, na alilazimika kuomba msaada kutoka kwa marafiki na familia.[5] Baadaye pensheni yake ya ujane iliongezwa kutoka dola 30 hadi dola 50 za Marekani kwa mwezi.

Elise Blenker alifariki tarehe 15 Mei 1908 katika nyumba ya binti yake huko Mount Vernon (New York).

  1. Taarifa ya kifo, The New York Times, 17 Mei 1908
  2. 1 2 ADB
  3. 1 2 3 4 NIE
  4. Wittke, Carl (1952). Refugees of Revolution: The German Forty-Eighters in America. Philadelphia: University of Pennsylvania Press. ku. 233–235.
  5. Washington ist begeistert von dem Deutschen katika FAZ, 30 Oktoba 2013, ukurasa wa 30