Nenda kwa yaliyomo

Edward Tingatinga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Edward Said Tingatinga)

Edward Saidi Tingatinga (1932 - 1972) alikuwa Msanii wa Tanzania aliyeanzisha mtindo wa uchoraji wa Tingatinga, ambao leo unajulikana sana na unapendwa na wapenzi wa sanaa ya Tanzania duniani kote.

Maisha kabla ya Sanaa

[hariri | hariri chanzo]
Kijiji kilichopo karibu na Namocheli alipozaliwa Edward Tingatinga

Tingatinga alizaliwa mwaka 1932 katika kijiji kilichoitwa Namochelia, wilaya ya Tunduru, mkoa wa Ruvuma kusini mwa Tanzania, karibu na mpaka wa kaskazini wa Msumbiji. Kijiji hicho hakipo tena leo; inaaminika kilipotea miaka ya 1960 kutokana na mpango wa Ujamaa wa Rais Julius Nyerere uliosababisha watu kuhamishwa kutoka vijiji vidogo.Maeneo yaliyopo sasa katika eneo hilo ni Mindu, Nakapanya na Mtonya. Watu wengi wa familia ya Edward Tingatinga upande wa mama bado wanaishi katika vijiji hivyo, huku ndugu wa upande wa baba wakiishi Ngapa, takribani kilomita 20 kaskazini mwa Nakapanya.

Edward Tingatinga alizaliwa katika familia maskini. Mama yake, Agnes Binti Ntembo, alikuwa wa kabila la Makua na Mkristo, huku baba yake, Saidi Tingatinga, akiwa wa kabila la Ngindo na Muislamu. Ndiyo sababu mtoto alipewa jina la Kikristo (Edward) na pia jina la Kiislamu (Saidi).Kwa kuwa jamii ya Makua hurithi kwa upande wa mama, Edward Tingatinga anahesabika kuwa wa asili ya Makua. Alipokuwa mtoto, alilelewa zaidi na familia ya mama yake. Baadaye, uhusiano kati ya Agnes Ntembo na Saidi Tingatinga ulivunjika.Agnes Ntembo alipata wana wengine watatu na wanaume wawili tofauti, ambao ni Andrea Gallusi, Simon Mpata na Cesilia Mpata. Simon Mpata pamoja na Agnes Mpata (binti wa Cesilia) baadaye walifuata nyayo za Edward na kujiunga na kundi la wasanii wa uchoraji alilolianzisha

Kuchora kwa kujipatia chakula

[hariri | hariri chanzo]

Siku zile alianza kuchora ingawa haijulikani ilikuwa kwa njia gani. Katika miaka ya 1960 aliuza picha zake barabarani kwa Shilingi 15 iliyokuwa sawa na bei ya mlo.

Mwaka 1968, baada ya kufunga ndoa na Agata Mataka, alikazania uchoraji. Wengine walisema ya kwamba aliendelea na kazi ndogo kwenye hospitali ya Muhimbili ingawa hapa haijulikani alifanya kazi gani kamili na hadi lini.

Mtindo wa Tingatinga

[hariri | hariri chanzo]

Tazama makala Tingatinga (uchoraji)

Wakati ule alianzisha mtindo wake. Badala ya karatasi alichora kwenye ubao aina ya "ceiling board" iliyokuwa rahisi lakini ni imara. Alikata vipande vya mraba vya futi 2x2. Akishirikiana na wadogo zake alianza kuchora picha za wanyama.

Mnamo mwaka 1970 Wazungu kutoka Skandinavia walianza kutafuta picha zake wakimsaidia kuhudhuria maonyesho ya biashara ya kwanza ya Dar es Salaam. Ghafla Tingatinga akawa maarufu, picha zake zilitafutwa na bei zikapanda. Picha zake zilikuwa uso wa sanaa ya Tanzania akawa mchoraji maarufu wa Afrika yote.

Kifo na ushirika wa Tingatinga

[hariri | hariri chanzo]

Edward Tingatinga aliaga dunia mnamo mwaka 1972. Alipigwa risasi na polisi kimakosa akidhaniwa ni mhalifu. Alizikwa kwenye makaburi ya Msasani Mikoroshini mjini Dar es Salaam.

Ndugu zake waliendelea na mtindo wake wa uchoraji na wengine wengi walimfuata wakiiga mtindo huo. Mtindo wa uchoraji wa Tingatinga (Tingatinga painting) uliendelea kukua na kuwa kivutio kwa watalii nchini Tanzania, Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Awali walikuwa na matatizo kwa sababu walifukuzwa mara nyingi toka mahali walipofanya kazi. Mwaka 1977 wachoraji Hashimi Mruta, Zaburi Muradi Chimwanda, Amonde, Tedo, Mpata, Amadi Saidi, Mchisa, Abasi, Salum Mussa, Mohamedi Saidi Chilamboni na Fr. J. Linda waliunda ushirika wa "TINGATINGA Partnership" wakaiandikisha serikalini. Mwenyekiti wa kwanza alikuwa Omari Amonde.

Washirika walijenga vibanda karibu na Morogoro Stores ambako picha zao ziliuzwa.

Ushirika ulibadilisha jina mwaka 1990 kuwa "Tingatinga Arts Cooperative Society Limited".

    Viungo vya Nje

    [hariri | hariri chanzo]
    Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
    Je, unajua kitu kuhusu Edward Tingatinga kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
    Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
    Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.