Dida Shaibu
| Kuzaliwa | Oktoba 22, 1982 |
| Kufariki | Oktoba 4, 2024 |
| Umri | Miaka 42 |
| Mume | Mohammed Mchopanga |
| Mtoto | Samira M Mchopanga |
| Tuzo | Mtangazaji bora wa kike wa vipindi vya redio |

Khadija Shaibu (alijulikana zaidi kwa jina la Dida Shaibu; 22 Oktoba 1982 – 4 Oktoba 2024) alikuwa mtangazaji mahiri wa redio, MC (master of ceremonies), na mjasiriamali kutoka Tanzania. Alikuwa mmoja wa watu muhimu katika tasnia ya habari nchini Tanzania na Afrika Mashariki, hasa akisifika kwa sauti yake nzuri ya mamlaka na ujuzi wake katika muziki wa Taarab.
Maisha ya awali na kazi
[hariri | hariri chanzo]Dida Shaibu alianza kazi yake ya utangazaji mwaka 2003, akiwa na umri wa miaka 21 kama mwanafunzi wa field kutoka DSJ.
Alipata umaarufu mkubwa akiwa mtangazaji wa redio Times FM katika kipindi maarufu cha mitikisiko ya pwani alichokua akifanya na muigizaji mkongwe na mtangazaji marehemu Chuma Suleiman almaarufu kama Bi Hindu, ambapo alitambulika kwa uwezo wake wa kuwasiliana na hadhira na ujuzi wake wa kina kwenye muziki wa Taarab na misemo ya utani ya uswahilini inayojulikana kama "michambo". Mchango wake ulikuwa muhimu sana katika kuufikisha muziki huu wa asili wa Kiswahili kwa hadhira kubwa kupitia redio [1][2].
Taji Liundi, msimamizi wa vipindi wa Times FM kwa wakati huo, ndiye aliyependekeza jina la "Dida" [3].
Baada ya kufanya kazi Times FM, Mwaka 2020 Dida alijiunga na Wasafi Media Group na kuwa mtangazaji mkuu wa Wasafi FM, moja ya vituo maarufu zaidi vya redio nchini Tanzania. Akiwa Wasafi FM, alikuwa mtangazaji wa kipindi maarufu cha Mashamsham. Kipindi hicho kilisifika kwa muundo wake wa kusisimua na wenye mwingiliano, kikijumuisha mchanganyiko wa burudani, ikiwemo Taarab, Bongo Flava, na muziki wa Singeli, pamoja na mijadala na mahojiano yenye mvuto.
Mbali na kazi yake ya utangazaji, Dida Shaibu alikuwa mjasiriamali aliyefanikiwa. Alikuwa mmiliki wa duka la nguo la Classic Boutique lililopo Kinondoni Dar es Salaam.
Dida pia aliwahi kuachia kibao cha muziki wa taarabu alichokipa jina la "Waniache miaka 800" katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine iliyopo Magomeni, Dar es Salaam, akisindikizwa na kundi maarufu la muziki huo la Jahazi [4].
Utambulisho na ushawishi kwa umma
[hariri | hariri chanzo]Dida Shaibu aliheshimika sana katika tasnia ya habari ya Tanzania kwa sauti yake ya kipekee na haiba yake isiyo na maigizo. Alijulikana kwa kuwa mkweli na mzungumzaji wa moja kwa moja, mara nyingi akijadili masuala binafsi na ya umma kwa ujasiri na kujiamini, jambo lililowavutia sana wasikilizaji wake.
Ushawishi wake ulivuka mipaka ya redio; alikuwa MC maarufu, akiendesha matukio mbalimbali ya umma na matamasha kote Tanzania. Kifo chake kilitangazwa kwa simanzi kubwa kutoka kwa wananchi na viongozi mashuhuri. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa salamu zake za rambirambi na kumuenzi Dida Shaibu, akisisitiza mchango wake mkubwa kwa tasnia ya redio nchini [5][6].
Kifo
[hariri | hariri chanzo]Dida Shaibu alifariki dunia tarehe 4 Oktoba 2024, akiwa na umri wa miaka 42 [7][8], kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa za madaktari na kutoka kwa familia na wafanyakazi wenzake, kifo chake kilitokana na matatizo ya vidonda vya tumbo.
Taarifa rasmi ya kifo cha Dida kilithibitishwa na Majid Mbinga, mtayarishaji wa kipindi cha Mashamsham. Kifo chake kiliombolezwa sana kama pigo kubwa kwa tasnia ya burudani na habari nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Mwili wa Dida ulizikwa jioni ya Oktoba 5, katika makaburi ya kisutu jijini Dar es salaam [9].
Familia na Ndoa
[hariri | hariri chanzo]Dida wakati wa uhai wake, alibahatika kufunga ndoa kadhaa mojawapo ikiwa na aliekuwa Diwani wa Vingunguti. Lakini pia aliyekua Meya wa jiji la Dar es Salaam, Mh. Omary Kumbilamoto, Dida na Kumbilamoto walifunga ndoa mwaka 2021, lakini ndoa hii ilikumbwa na changamoto na kuvunjika baadaye.
Pia Dida aliwahi kufunga ndoa na mfanyabiashara Mohammed Mchopanga almaarufu kama Mchops, na nyingine na mfanyabiashara Gervas Mbwiga, pamoja na mtangazaji mwenzake, Ezden Jumanne [10].
Dida ameacha mtoto mmoja tu wa kike, Samira, aliyezaa na Mohammed Mchopanga [11]. Baada ya kifo cha Dida, mkurugenzi wa Wasafi Media, Diamond Platnumz alitoa ahadi ya kumsomesha Samira mpaka atakapo maliza Elimu yake [12].
Mizozo
[hariri | hariri chanzo]Dida aliweza kukabiliana na changamoto nyingi katika maisha yake binafsi na ya kitaaluma, licha ya kupitia migogoro ya ndoa na kukosolewa, aliendelea kuwa mmoja wa watangazaji maarufu wa redio nchini Tanzania na Afrika Mashariki.
Tuzo
[hariri | hariri chanzo]Kwa uhodari na ujuzi aliokua nao kwenye utangazaji, Dida alifanikiwa kushinda tuzo mbali mbali katika maisha yake ya taaluma, ikiwemo tuzo ya mtangazaji bora wa kike katika vipindi vya redioni, ikiwemo kushinda tuzo kwa miaka miwili mfululizo, 2006 na 2007, tuzo zilizotolewa na kampuni ya George Inc LTD
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Kabla ya Taarab Dida alipenda Hip-Hop na R&B". youtube.com. Iliwekwa mnamo 2024-11-01.
- ↑ "Times FM Twist". ReverbNation. Iliwekwa mnamo 2023-04-16.
- ↑ "Kabla ya Taarab Dida alipenda Hip-Hop na R&B". youtube.com. Iliwekwa mnamo 2024-11-01.
- ↑ "DIDA' Mtangazaji wa radio aliyejitosa kwenye muziki wa mipasho". liwazozito.blogspot.com. Iliwekwa mnamo 2010-10-14.
- ↑ "Rais Samia aomboleza kifo cha Dida Shaibu". Daily News. Iliwekwa mnamo 2024-10-05.
- ↑ "INTERVIEW DIAMOND ALIVYOMWAGA MACHOZI KIFO CHA DIDA SHAIBU "SIAMINI HATA KIDOGO". youtube.com. Iliwekwa mnamo 2024-12-04.
- ↑ "Dida Shaibu, mtangazaji wa Wasafi FM afariki Dunia". jamiiforums.com. Iliwekwa mnamo 2024-10-04.
- ↑ "Kumbukumbu ya wakongwe wa burudani tulio wapoteza mwaka 2024". Thecitizen.co.tz. Iliwekwa mnamo 2024-12-27.
- ↑ "Kabla ya Taarab Dida alipenda Hip-Hop na R&B". youtube.com. Iliwekwa mnamo 2024-11-01.
- ↑ "Mtangazaji Dida Afunga Ndoa Serena Dar". liwazozito.blogspot.com. Iliwekwa mnamo 2021-06-11.
- ↑ "DIDA SHAIBU :HATUKUWEZANA NA MCHOPSI SINA SHIDA / WANAJUA MAISHA YA WATU / WANAROGA SANA". youtube.com. Iliwekwa mnamo 2024-10-06.
- ↑ "Diamond amejitolea kumsomesha mtoto wa Dida mpaka anamaliza Elimu". jamiiforums.com. Iliwekwa mnamo 2024-10-06.