Nenda kwa yaliyomo

Mgwaru

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Cyamopsis tetragonoloba)
Mgwaru
(Cyamopsis tetragonoloba)
Migwaru
Migwaru
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Plantae (Mimea)
(bila tabaka): Angiospermae (Mimea inayotoa maua)
(bila tabaka): Eudicots (Mimea ambayo mche wao una majani mawili)
(bila tabaka): Rosids (Mimea kama mwaridi)
Oda: Fabales (Mimea kama mharagwe)
Familia: Fabaceae (Mimea iliyo na mnasaba na mharagwe)
Nusufamilia: Faboideae (Mimea inayofanana na mharagwe)
Jenasi: Cyamopsis
DC.
Spishi: C. tetragonoloba
(L.) Taub.

Mgwaru ni mmea wa nusufamilia Faboideae katika familia Fabaceae (miharagwe). Maua na makaka yake ni katika mafundo mazito. Mbegu zake huitwa magwaru (kutoka na Kiurdu گوار, guaar). Yamkini mhenga wa mgwaru ni mmea wa Afrika Cyamopsis senegalensis lakini umegeuka mashambani kwa Uhindi na Pakistani.

Mmea huu hukuzwa huko Uhindi na Pakistani hasa lakini siku hizi unaanza kupandwa mahali pengine pia kwa sababu ya gundi ya mbegu zake. Hutumika kwa mbolea kijani na kwa chakula pia. Majani na makaka mabichi huliwa na hata magwaru, lakini lazima yabanikwe kwanza ili kuharibu dumazaji ya tripsini (trypsin inhibitor: tripsini ni kimeng'enya kinachomeng'enya proteini). Mgwaru unaweza kutumika pia kwa malisho lakini lazima makaka yawe yakikomaa kwa sababu makaka mabichi yana asidi hidrosianiki.

Lakini utumiaji muhimu sana wa mgwaru ni utengenezaji wa gundi ya gwaru (guar gum). Magwaru yana endospermi kubwa iliyo na polisakaridi ya galaktosi na manosi. Ikiyeyuka katika maji, haya yanakuwa rojorojo. Kwa hiyo gundi ya gwaru hutumika katika tasnia ya chakula, vitambaa, karatasi, dawa na utamaradi. Tangu hivi karibuni gundi hii hutumika sana katika tasnia ya mafuta na gesi ya mwambatope. Inasaidia maji yaingie katika mivunjiko ya miamba.