Kanisa la Ungamo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Confessing Church)

Kanisa la Ungamo (kwa Kijerumani: Bekennende Kirche, kwa Kiingereza: Confessing Church) lilikuwa harakati ndani ya Uprotestanti wa Ujerumani wakati wa utawala wa Adolf Hitler. Ilipinga juhudi zilizofadhiliwa na serikali ya Wanazi za kuunganisha makanisa yote ya Kiprotestanti kuwa kanisa moja la kushikamana na serikali yao.[1]

Mandharinyuma[hariri | hariri chanzo]

  • Mnamo mwaka 1933 idadi ya Wakristo Waprotestanti nchini Ujerumani ilikuwa milioni 45 (kati ya jumla ya wakazi milioni 78) waliohudumiwa na wachungaji 18,000.
  • Waprotestanti hao walikuwa wakristo walioandikishwa katika makanisa ya kieneo yaliyowahi kuwa makanisa rasmi ya kidola hadi mwaka 1918. Baada ya mapinduzi ya Ujerumani ya 1918 dola na makanisa yalitengwa. Kidhehebu makanisa hayo yalikuwa ama makanisa ya Kilutheri, makanisa ya Kireformed au makanisa ya maungano yaliyounganisha sharika za kilutheri na za kireformed.
  • Kanisa kubwa lilikuwa Kanisa la Kiinjili katika Prussia lenye Wakristo milioni 18.
  • Idadi ya wachungaji wa Kiprotestanti: 18,000
    • Idadi ya hawa walioshikamana sana na kikundi cha kanisa la "Kikristo cha Kijerumani" kama cha 1935: 3,000
    • Idadi ya hawa walioshikamana sana na kikundi cha kanisa la "Kukiri Kanisa" kufikia 1935: 3,000
      • Idadi ya hawa waliokamatwa wakati wa 1935: 700
    • Idadi ya hizi ambazo hazijafungamana sana au kushikamana na kikundi chochote: 12,000
  • Jumla ya wakazi wa Ujerumani: 65 milioni
  • Idadi ya Wayahudi nchini Ujerumani: 525,000 [2]

Baada ya mapinduzi ya 1918 maelewano yalifikiwa: kusiwe tena na makanisa ya kidola, lakini makanisa yabaki mashirika ya umma yakiendelea kupokea sehemu ya ruzuku kutoka serikalini kwa huduma walizofanya kama kuendesha hospitali, chekechea n.k. Kanisa lilipaswa kuachana na usimamizi wa shule. Kwa upande mwingine serikali iliendelea kukusanya michango kutoka kwa wanakanisa kutokana na kodi ya walioandikishwa kama washirika wa kanisa na waligawa fedha hizi kwa makanisa. Ada hizo zilikuwa, na hadi leo zinatumika kufadhili shughuli za kanisa. Idara za theolojia katika vyuo vikuu viliendelea kuwapo, na mafundisho ya dini shuleni yaliendelea wakati wazazi waliweza kuondoa watoto wao. Haki zilizokuwa zikishikiliwa na wafalme katika Dola la Ujerumani zilikabidhiwa kwa mabaraza ya kanisa na sinodi.

Kwa hiyo, katika kipindi cha kwanza cha Jamhuri ya Weimar, mnamo 1922, makanisa ya Kiprotestanti huko Ujerumani yaliunda Shirikisho la Kanisa la Kiinjili la Ujerumani lenye makanisa wanachama 28 ya kieneo. [3] Mfumo huo wa shirikisho uliruhusu uhuru mwingi wa kieneo katika utawala wa Uprotestanti wa Ujerumani. Iliruhusu pia kuanzishwa kwa sinodi au bunge la kanisa la kitaifa ambalo lilikuwa jukwaa la majadiliano na ambalo lilijaribu kusuluhisha mizozo ya kitheolojia na ya kiutawala.

Utawala wa Wanazi[hariri | hariri chanzo]

Waprotestanti wengi waliwapiga kura Wanazi katika uchaguzi wa miaka 1932 na 1933. Katika maeneo yenye Wakatoliki wengi kura kwa Wanazi zilikuwa chache kulingana na maeneo ya Waprotestanti.[4] Makanisa ya Kiprotestanti hayakupinga kimsingi itikadi ya Hitler. Waprotestanti wengi walizoea wazo la serikali yenye madaraka mengi na uhusiano wa karibu baina ya serikali na kanisa, jinsi ulivyowahi kuwepo hadi mwaka 1918, miaka michache iliyopita. Waprotestanti wengi walikuwa na wasiwasi kuhusu jamhuri ya Weimar na demokrasia. Wengi walishikamana na vyama vilivyochora picha nzuri ya miaka iliyopita chini ya wafalme wa Ujerumani.

Idadi ndogo ya viongozi Waprotestanti, kama vile Karl Barth, Dietrich Bonhoeffer na Wilhelm Busch, [5] [6] walipinga Wanazi juu ya kanuni za maadili na kitheolojia; hawangeweza kupatanisha madai ya serikali ya Wanazi kwa udhibiti kamili juu ya jamii upande mmoja na mamlaka kuu inayostahili kuwa upande wa Mungu katika imani yao kwa upande mwingine.

Harakati ya "Wakristo Wajerumani"[hariri | hariri chanzo]

Miaka michache kabla ya 1933 ilitokea harakati ya wafuasi wa Hitler kati ya wachungaji na Wakristo wa Kiprotestanti.[7] Walianza kujipanga kama chama ndani ya kanisa na kushiriki katika uchaguzi wa sinodi na mabaraza ya wazee wa sharika wa 1931 katika kanisa la Prussia.

Wakristo Wajerumani walikubali shabaha ya Wanazi ya "kuratibu" makanisa ya Kiprotestanti ya kieneo kuwa kanisa kubwa moja ya kitaifa lililolingana na itikadi ya "Taifa moja, Dola moja, Kiongozi mmoja" ya Wanazi.

Kuundwa Kanisa Jipya la Kitaifa ( Deutsche Evangelische Kirche )[hariri | hariri chanzo]

Askofu Müller baada ya uchaguzi wake huko Wittenberg, akiinua mkono kwa "salamu ya Hitler".

Wakati Wanazi walipochukua madaraka kwenye Januari 1933, kanisa la Kiprotestanti la Ujerumani lilikuwa shirikisho la makanisa huru ya kieneo pamoja na urithi wao wa Kilutheri, Kireformed na kimaungano.

Kwenye mwezi wa Aprili 1933 uongozi wa shirikisho la Kiprotestanti ulikubali kuandika katiba mpya ya kanisa "la kitaifa" Kanisa la Kijerumani la Kiinjili (Deutsche Evangelische Kirche au DEK). Wakristo Wajerumani walimtaka kiongozi wao Ludwig Müller, aliyekuwa pia mshauri wa Hitler kwa masuala ya kidini, achaguliwe kuwa askofu mpya wa kanisa la kitaifa.

Hitler mwenyewe alimtaka pia Müller kuchaguliwa kuwa askofu wa kitaifa. Baada ya kushindwa kufikia shabaha yake alikasirika akaamuru uchaguzi mpya ya sinodi na mabaraza ya wazee kote Ujerumani.[8] [9] Usiku kabla ya uchaguzi, Hitler alihutubia Waprotestanti kupitia redio wawapige kura wagombea waliokuwa upande wake.

Wakristo Wajerumani walishinda asilimia 70 - 80 ya viti vyote katika mabaraza na sinodi, isipokuwa katika makanisa manne ya kieneo (Walutheri wa Bavaria, Walutheri wa Hannover na Wareformed wa Hannover, Walutheri wa Württemberg) na jimbo la Westfalia kwenye kanisa la Prussia, ambapo Wakristo Wajerumani hawakupata uwingi.

Ushindi huu wa uchaguzi uliwawezesha Wakristo Wajerumani kupata wajumbe wa kutosha katika sinodi ya kitaifa iliyoendesha uchaguzi wa Müller kuwa askofu wa kitaifa (Reichsbischof). [10] Chini ya usimamizi wa Müller kanisa la Prussia lilipitisha sheria ya kutengua wachungaji na watumishi wote wenye ukoo wa Kiyahudi na hata watumishi waliowahi kuoa wake wasiotazamwa kuwa Waarya (mtu yeyote mwenye wazazi wa babu/bibi Myahudi hakuwa "Arya" bila kujali dini yake mwenyewe) kufuatana na sheria za Wanazi.

Kanisa la Ungamo[hariri | hariri chanzo]

Jiwe la ukumbusho wa Sinodi ya pili ya Ungamo kwenye ukuta wa nje wa nyumba ya mkutano.

Sheria kuhusu Waarya kilisababisha hisia kati ya wachungaji. Chini ya uongozi wa Martin Niemöller, Ligi ya Dharura ya Wachungaji (jer. Pfarrernotbund) iliundwa, kwanza kwa kusudi la kusaidia wachungaji wenye asili ya Kiyahudi, lakini ligi hiyo ilibadilika kuwa mkusanyiko wa wapinzani dhidi ya kuingilia kwa Wanazi katika masuala ya kanisa. Uanachama wake uliongezeka [11] wakati pingamizi na maneno ya Wakristo Wajerumani viliongezeka. Msingi wa upinzani wa Ligi ya Dharura ya Wachungaji ulikuwa walichoona kama dharau ya ubatizo. Walitetea tofauti baina ya Wayahudi na Wakristo waliowahi kuwa Wayahudi wakiwaona kama Wakristo kamili bila kasoro yoyote. [12]

Mwanzoni Waprotestanti katika ligi ya dharura hawakupinga hatua zilizochukuliwa na Wanazi dhidi ya Wayahudi kwa ujumla, zilizoanza kutungwa na kutekelezwa tu polepole. [11] Hatimaye, Ligi ilibadilika na kuwa Kanisa la Ungamo.

Tarehe 13 Novemba 1933 mkutano wa Wakristo wa Ujerumani ulifanyika katika uwanja wa michezo huko Berlin, ambapo wasemaji walitangaza umoja wa Unazi na Ukristo, madai ya kuwafukuza wachungaji wote wasioshikamana na siasa ya Hitler,[13] kufukuzwa kwa Wakristo wote wenye asili ya Kiyahudi katika kanisa, kuondolewa kwa Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo likiwa "kitabu cha Kiyahudi", na kubadilisha mahubiri kuhusu Yesu anayepaswa kuonyeshwa kama shujaa aliyepinga athira mbaya ya Wayahudi.[14]

Habari za mkutano huo zilishtusha Wakristo wengi walioona hapa jaribio la serikali na chama cha utawala kuingilia masuala ya imani ndani ya kanisa.

Wakati Hitler, mwanasiasa kamili, alisita kutumia mabavu mno katika kipindi hicho cha mwanzo wa utawala wake, askofu Ludwig Müller aliwafukuza kazi na kuwahamisha wachungaji wanaoshikilia Ligi ya Dharura, na mnamo Aprili 1934 alitangaza kuondolewa kwa wakuu wa kanisa la Württemberg na wa Bavaria.

Ungamo la Imani la Barmen[hariri | hariri chanzo]

Mnamo Mei 1934, upinzani dhidi ya Wakristo Wajerumani ulikutana katika sinodi huko Barmen. Wajumbe walimshutumu Müller na uongozi wake na kutangaza kwamba wao na sharika zao ndio Kanisa la Kiinjili la kweli la Ujerumani. Ungamo la Barmen liliandikwa na Karl Barth, baada ya kushauriana na wachungaji wengine kama Martin Niemöller na sharika kadhaa. Lilithibitisha kwamba kanisa si "chombo cha serikali" na kwamba wazo la serikali kudhibiti kanisa lilikuwa mafundisho ya uongo. Ungamo hilo lilisema kwamba serikali yoyote - hata ile ya kiimla - lazima ina kikomo wakati inakabiliwa na amri za Mungu. Tamko la Barmen lilikuwa msingi wa Kanisa la Ungamo. [15]

Baada ya Ungamo la Barmen, kulikuwa na harakati mbili zilizopingana katika Kanisa la Kiprotestanti la Ujerumani:

  • harakati ya Wakristo Wajerumani na
  • Kanisa la Ungamo (Bekennende Kirche, BK)

Kanisa la Ungano lenyewe halikulenga kuangusha serikali ya Wanazi, bali ilikaza upinzani dhidi ya majaribio ya serikali kuamulia mambo ya ndani ya kanisa na imani.

Lakini idadi ya wafuasi wake ilikuwa waliotambua kwamba misingi ya Unazi ilikuwa pamoja na Upagani, na matendo mengi ya serikali ya Kinazi yalikuwa jinai kwa maadili ya Kikristo.

Baada ya Barmen[hariri | hariri chanzo]

Hali hiyo iliendelea kuwa tata baada ya Barmen. Ukosefu wa uwezo upande wa Müller katika masuala ya kisiasa haukumpendeza Hitler . [16] Mkutano wa Berlin ulileta aibu kwa chama cha Wanazi.

Hitler alijaribu kutuliza hali hiyo katika msimu wa 1934 kwa kuwaruhusu maaskofu wa Bavaria na Württemberg kuondoka tena katika nyumba zao walipowahi kubanwa. Alimchoka Müller na Wakristo Wajerumani akaondoa madaraka ya Müller haswa na Wakristo Wajerumani kwa jumla, akaunda Wizara mpya kwa ajili ya makanisa akamteua waziri mwenye uwezo mzuri zaidi wa kuongea na Wakristo.

Mwaka 1936 Kanisa la Ungamo, chini ya uongozi wa Niemöller, lilitoa barua kwa Hitler. Kwa lugha ya heshima ilipinga mielekeo ya serikali dhidi ya Ukristo, ililakamika kuhusu siasa ya kuwabagua Wayahudi na kudai serikali iache kuingilia mambo ya ndani ya kanisa.

Serikali ilijibu kwa:

  • kuwakamata wachungaji mia kadhaa
  • kumuua Dk. Friedrich Weißler, meneja wa ofisi na mshauri wa kisheria wa ofisi kuu ya Kanisa la Ungamo kambi ya wafungwa ya Sachsenhausen
  • kunyang'anya fedha za Kanisa la Ungamo
  • kupiga marufuku matoleo kwa ajili ya Kanisa la Ungamo

Waziri wa mambo ya kanisa aliwahutubia viongozi wa kanisa rasmi kwenye 13 Februari 1937 kwa maneno yafuatayo: Ukristo halisi ni sawa na "Ujamaa wa Kitaifa" na Ujamaa wa kitaifa ni kutenda mapenzi ya Mungu... Nimeambiwa kwamba Ukristo ni imani katika Kristo kama Mwana wa Mungu. Hii inanifanya nicheke... Ukristo hautegemei Imani ya Mitume lakini inawakilishwa na chama cha NSDAP... Wajerumani sasa wanaitwa na Kiongozi (=Hitler) kufikia Ukristo wa kweli. Kiongozi ndiye mjumbe wa ufunuo mpya".

Matokeo[hariri | hariri chanzo]

Baadhi ya viongozi wa Kanisa la Ungamo, kama vile Martin Niemöller au Heinrich Grüber, walipelekwa kwenye kambi za wafungwa. Wakati Grüber na Niemöller walinusurika, si wote waliokoka: Dietrich Bonhoeffer alinyongwa kwenye Aprili 1945. Hii iliwaacha Wakristo ambao hawakukubaliana na Wanazi bila uongozi.

Wachache wa Kanisa la Ungamo walihatarisha uhai wao kusaidia Wayahudi kujificha kinyume cha sheria huko Berlin wakati wa vita. Walikusanya pesa na vitambulisho vilivyobadilishwa na waghushi na kupewa Wayahudi waliojificha ili waweze kupita kama raia halali wa Berlin. [17] Washiriki kadhaa wa Kanisa la Ungamo walikamatwa na kuhukumiwa kwa sehemu yao katika kuunda vitambulisho vya kughushi, pamoja na Franz Kaufmann aliyepigwa risasi, na Helene Jacobs, ambaye alifungwa jela.

Baada ya Vita Kuu ya Pili, Azimio la Hatia la Stuttgart lilikuwa tangazo lililotolewa mnamo 19 Oktoba 1945 na Baraza la Kanisa la Kiinjili la Ujerumani (Evangelische Kirche in Deutschland au EKD), ambapo ilikiri hatia ya kutokufaa kwake kwa kupingana na Wanazi na utawala wao. Iliandikwa haswa na washiriki wa zamani wa Kanisa la Ungamo.

Angalia pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Germany. Berkley Center for Religion, Peace, and World Affairs. Jalada kutoka ya awali juu ya 12 October 2013. Iliwekwa mnamo 2011-12-29. See drop-down essay on "Unification, World Wars, and Nazism"
  2. Holocaust Encyclopedia p. 427, chini ya asilimia 0.9 za wakazi wote wa Ujerumani
  3. Mara nyingi eneo la kanisa lililingana na mikoa ya serikali.
  4. Spenkuch, Jörg L.; Tillmann, Philipp (January 2018). "Elite Influence? Religion and the Electoral Success of the Nazis". American Journal of Political Science 62 (1): 19–36. doi:10.1111/ajps.12328. Archived from the original on 2018-03-25. Retrieved 2021-04-09 – via Wiley Online Library. 
  5. BEKANNTE MITGLIEDER DER CVJM/YMCA BEWEGUNG INTERNATIONAL (Wanachama mashuhuri wa harakati ya YMCA kimataifa) (de). Jalada kutoka ya awali juu ya 25 April 2012. Iliwekwa mnamo 2011-11-20. “Wilhelm Busch (*1897; † 1966), ...Wakati wa utawala wa Wanazi imani yake na juhudu za Kanisa la Ungamo vilifikisha mara kadhaa gerezani.”
  6. Busch, Wilhelm (1987). Jesus our destiny. Inter Publishing Service. p. 5. ISBN 0-86347-024-6. .Wakati wa utawala wa Wanazi imani yake na juhudu za Kanisa la Ungamo vilifikisha mara kadhaa gerezani. 
  7. Hitler alikuwa mkuu wa serikali ("chansella") mnamo 30 Januari 1933.
  8. Barnett p. 34.
  9. Katiba mpya ya kanisa la DEK la kitaifa ilikubaliwa na bunge la Ujerumani mnamo tarehe 14 Julai 1933. Shirer p. 237.
  10. Kershaw pp. 487–88.
  11. 11.0 11.1 By the end of 1933 the League already had 6,000 members. Barnett p. 35.
  12. Barnett p. 35.
  13. Msemaji mkali zaidi alikuwa Dr. Reinhardt Krause, kiongozi wa Wakristo Wajerumani katika mkoa wa Berlin; alidai kufutwa kwa Agano la Kale na kutoa mahubiri juu ya Yesu yanayolingana na mahitaji ya Ujamaa wa Kitaifa. Kulikuwa pia na maazimio ya kutaka wachungaji wote wale kiapo kwa Hitler, makanisa yote kukubali sheria ya Waarya na kutenga Wayahudi, watoto na wajukuu wao katika kanisa. Hotuba ya Krause ilikuwa kali kiasi kwamba hata Müller alimsimamisha baadaye kama kiongozi wa kimkoa. Shirer p. 237.
  14. Barnett pp. 34–35.
  15. Barnett p. 7.
  16. Baada ya makosa ya kisiasa ya Müller, serikali ya Wanazi ilianza kukazia utengano wa kanisa na serikali. Viongozi wa Wanazi Frick na Göring walimtazama Müller kuwa "mborongaji" na hata kamishna wa serikali katika kanisa la Prussia alimtazama mtu asiyeweza kutegemewa. Barnett p. 36.
  17. See generally Schonhaus.