Clement George Kahama

Clement George Kahama (alifahamika pia kama Sir George; 1929 - 2017) alikuwa mwanasiasa na mwanadiplomasia nchini Tanzania[1].
Historia
[hariri | hariri chanzo]Alizaliwa mnamo Novemba ya mwaka 1929 mjini Karagwe, Mkoa wa Kagera. Alipata elimu katika shule ya Ihungu Sekondari na kisha shule ya Tabora Boys, kabla ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu huko chuo cha Loughborough cha Uingereza kati ya mwaka 1952 na 1954.
Alirejea Tanganyika na kuwa Meneja Mkuu wa Kwanza wa Ushirika wa Wakulima wa Bukoba (Bukoba Native Cooperative Union Ltd), shirika lililohusika na ununuzi, usindikaji na uuzaji wa kahawa, chai na mazao mengine ya kilimo. Wakati huo huo alihudumu kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.
Mwaka 1957, aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (LEGCO), akiwakilisha mkoa wa West Lake wa wakati huo (sasa Mkoa wa Kagera), na kuanzia mwaka 1958 alichaguliwa kuwa Mbunge wa mkoa huo. Katika miaka miwili kabla ya Uhuru, alihudumu kama Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Ushirika katika serikali ya mpito.
Katika miaka mitatu mara baada ya Uhuru tarehe 9 Desemba 1961, Sir George alihudumu kwanza kama Waziri wa Mambo ya Ndani kisha Waziri wa Biashara na Viwanda, Mawasiliano, Usafirishaji na Kazi. Kisha alianza kazi ya kwanza kati ya tatu nje ya nchi, akihudumu mwaka 1965 na 1966 kama Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani na pia katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya (EEC).
Alirejea Dar es Salaam na kwa miaka saba iliyofuata akawa Meneja Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), kampuni kubwa kabisa ya uwekezaji nchini Tanzania. Ilikuwa ni kipindi mara baada ya Azimio la Arusha na katika uongozi wake, mashirika 89 ya umma katika viwanda, kilimo, madini na biashara yaliundwa (baadhi yakishirikiana na makampuni ya kimataifa).
Kuanzia mwaka 1973 kwa kipindi cha miaka kumi, George Kahama alipewa jukumu la kupanga, kuendeleza na kujenga mji mkuu mpya wa taifa, Dodoma. Aliyatekeleza majukumu haya sambamba kama Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais na kama Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Makao Makuu (CDA). Ingawa ilikuwa ni kazi ngumu, leo hii mji mkuu mpya wa Tanzania unaofanya kazi ni ushahidi wa dhamira ya Sir George kutimiza maono ya Mwalimu Nyerere.
Baadaye, akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii mwaka 1983 na 1984, George Kahama alielekeza nguvu zake katika kuendeleza na kutangaza hifadhi za wanyama na mbuga za taifa zinazotambulika sana duniani kote. Kisha, kwa miaka mitano iliyofuata, alihudumu kama Balozi wa Tanzania mwenye mamlaka kamili (Ambassador Extraordinary and Plenipotentiary) katika Jamhuri ya Watu wa China, akiwa pia na mamlaka ya uwakilishi katika Vietnam, Korea Kaskazini, Hong Kong na Thailand. Kutoka Beijing alihamia Harare, ambapo mwaka 1989 na 1990 alikuwa Kamishna Mkuu wa Tanzania nchini Zimbabwe. Baadaye, kutokana na mageuzi ya kiuchumi nchini na juhudi za serikali ya Tanzania kufungua uchumi na kuvutia uwekezaji binafsi na wa kigeni, Sir George alirejeshwa Dar es Salaam mwaka 1990 kuanzisha na kuongoza Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC). Alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kwanza wa kituo hicho, chini ya Ofisi ya Rais.
Kati ya mwaka 1995 na 2000, Sir George aliendelea kuwa Mbunge wa Karagwe. Wadhifa wake wa mwisho katika baraza la mawaziri ulikuwa Waziri wa Ushirika na Masoko, nafasi aliyoshikilia kwa miaka mitano hadi alipostaafu rasmi siasa mnamo Novemba 2005.
Sir George alihudumu chini ya Marais watatu wa kwanza wa Tanzania (Julius_Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa.[2] [3] Alifariki Mnamo mwaka 2017, katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.[4]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]| Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Clement George Kahama kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |