Nyenje-miti

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Cicadidae)
Nyenje-miti
Nyenje-miti akijilisha mtini (Platypleura capensis)
Nyenje-miti akijilisha mtini (Platypleura capensis)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo kama wadudu, nge, buibui)
Nusufaila: Hexapoda (Arithropodi wenye miguu sita)
(bila tabaka): Dicondylia (Wadudu walio na mandibula zenye condyle mbili)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Nusungeli: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda ya juu: Paraneoptera
Oda: Hemiptera (Wadudu mabawa-nusu)
Nusuoda: Auchenorrhyncha
Oda ya chini: Cicadomorpha (Wadudu kama nyenje-miti)
Evans, 1946
Familia ya juu: Cicadoidea (Nyenje-miti)
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Familia 2 na nusufamilia 6 zilizopo bado:

Nyenje-miti ni wadudu wa familia ya juu Cicadoidea katika oda Hemiptera. Wadudu wengine wanaoitwa nyenje wamo katika familia ya juu Grylloidea (Orthoptera). Nyenje-miti ni wadudu wakubwa kiasi (hadi sm 7) wenye macho yaliyobaidika sana, vipapasio vifupi, mabawa manne kama viwambo na sehemu za kinywa za umbo la mrija wenye ncha kali ili kutoboa gome la miti. Wanajulikana kwa sauti yao kubwa sana.

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Nyenje-miti ni wadudu wakubwa ambao husikika kwa milio ya uchumba ya madume. Wanasifika kwa kuwa na pingili tatu kwenye tarsi zao na kuwa na vipapasio vifupi vilivyo na vitako vyenye umbo la koni na pingili tatu hadi sita pamoja na seta kwenye ncha. Auchenorrhyncha hutofautiana na wadudu mabawa-nusu wengine kwa kuwa na sehemu za kinywa zinazotokana na sehemu ya chini ya kichwa, viwambo tata vya kuzalisha sauti na mfumo wa kuunganisha mabawa ambao unajumuisha ukingo uliopindwa chini wa nyuma ya bawa la mbele na lisani iliyotokeza juu kwenye bawa la nyuma. Nyenje-miti huruka dhaifu na tunutu wao hawana uwezo wa kuruka kabisa. Sifa bainifu nyingine ni matohozi ya miguu ya mbele ya tunutu kwa maisha ya chini ya ardhi.

Mdudu mpevu ana urefu wa jumla wa sm 2 hadi 5 katika takriban spishi zote, ingawa mkubwa kabisa, nyenje-malkia (Megapomponia imperatoria), ana urefu wa mwili wa karibu na sm 7 na upana wa mabawa yake ni sm 18-20. Nyenje-miti wana macho yaliyotokeza na kubaidika sana kwenye pande za kichwa. Vipapasio vifupi vimetokeza kati ya macho. Pia wana oseli ndogo tatu zilizopo juu ya kichwa kwenye pembetatu kati ya macho mawili makubwa. Hiyo inatofautisha nyenje-miti na wana wengine wa Hemiptera. Sehemu za kinywa zinaunda rositro (rostrum) ndefu na kali wanayoingiza katika mti au mmea ili kujilisha. Chini ya labro (mdomo) kuna muundo mkubwa kama pua ulio sehemu kubwa ya mbele ya kichwa. Misuli ya kufyonza imo ndani yake.

Toraksi (kidari) ina pingili tatu na ina misuli yenye nguvu ya mabawa. Ina jozi mbili za mabawa kama viwambo yanayoweza kuwa mangavu au yenye mavundevunde au rangi. Vena za mabawa hutofautiana kati ya spishi na zinaweza kusaidia katika kitambulisho. Pingili ya tatu ya toraksi ina jozi ya operkulo (operculum) upande wa chini ambazo zinafunika timpano (tympanum) na zinaweza kupanua upande wa nyuma na kuficha sehemu za fumbatio. Hiyo ina pingili ambazo zile za nyuma zina viungo vya uzazi ndani yao, na kwa majike ina kwenye ncha yake oviposito kubwa iliyo na makali kama msumeno. Pingili ya kwanza ya fumbatio inabeba jozi ya timpano, viwambo ambavyo vinakamata sauti. Kwa madume kuna aina mbili zaidi za viwambo: timbali (tymbal) zinazofunikwa kwa kunyanzi linalotokana na pingili ya pili ya fumbatio, na viwambo vilivyokunjwa, aina zote mbili chini ya operkulo. Timbali zinafanywa kutetemeka na msuli wa timbali na kwa hivyo hutoa sauti. Kisha sauti huongezewa na kifuko cha hewa ndani ya mbele ya fumbatio ambacho hutumika kama chumba cha kuvuma.

Spishi kadhaa za Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

  • Brevisiana niveonotata
  • Ioba leopardina
  • Iruana meruana
  • Koma bombifrons
  • Oxypleura polydorus
  • Oxypleura spoerryae
  • Paectira feminavirens
  • Paectira fuliginosa
  • Paectira jeanuaudi
  • Platypleura argus
  • Platypleura gowdeyi
  • Platypleura kenyana
  • Platypleura longirostris
  • Platypleura marsabitensis
  • Platypleura rothschildi
  • Pycna hecuba
  • Strumoseura nigromarginata
  • Ugada nutti

Picha[hariri | hariri chanzo]