Nenda kwa yaliyomo

Charles Hillary

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Charles Hillary
Charles Hilary enzi ya uhai wake
Charles Hilary enzi ya uhai wake
Jina la kuzaliwa Charles Martin Hillary Nkwanga
Alizaliwa 22 Oktoba 1959
Alikufa 11 Mei 2025
Nchi Tanzania
Kazi yake Mwandishi wa habari
Watoto 2

Charles Martin Hillary Nkwanga (22 Oktoba 1959 - 11 Mei 2025) alikuwa mtangazaji mkongwe Mtanzania aliyefanya kazi na vituo vikubwa vya utangazaji vya redio na televisheni vya ndani na nje ya nchi yake na kufikia hadhi ya mtu mashuhuri. Mpaka anafariki, alikuwa na cheo cha Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu ya Zanzibar.[1]

Maisha ya awali

[hariri | hariri chanzo]

Maarufu zaidi kwa majina ya Charles Hillary na Mzee wa macharanga, alizaliwa Jang'ombe, Unguja, mwaka 1959.[2] Baba yake, Martin Hillary Nkwanga, alikuwa na asili ya Tanganyika (sasa Tanzania bara), kabila Mpogoro. Mwaka 1956 bwana Martin Nkwanga alikwenda kufanya kazi Pemba kama askari polisi. Mama yake Charles aliyeitwa Bi. Esther Faith Ally, alikuwa Muunguja.

Katika maisha yake ya utotoni, kulitoea tukio ambalo Hillary hakulisahau daima. Ilikuwa ni kunusurika kuuwawa kwa risasi mwaka 1964, siku chache baada ya Mapinduzi yaliyoung'oa utawala wa Sultani Zanzibar.[3]Hiyo ilikuwa mwaka mmoja baada ya kumaliza elimu yake ya awali (chekechea), 1963.

Charles alianza masomo yake ya msingi katika shule ya Haile Selassie iliyoko Zanzibar mwaka 1966. Mwaka 1968 Charles alihamia Dar Es Salaam alikoendelea na masomo yake ya shule ya msingi katika shule ya Ilala Mchikichini.[4]Wakati huo alikuwa akiishi na mama yake mdogo bi. Lucy Ally na mumewe bw. Charles Kisaka (ambao baadae walihama wakiwa na Charles kutoka Ilala Mchikichini kwenda kuishi Kijitonyama, Sinza, Dar Es Salaam).

Charles alipata elimu yake ya sekondari kwenye shule ya sekondari ya Kinondoni Muslim kuanzia mwaka 1976 hadi 1979.

Baada ya kuhitimu mafunzo yake ya uandishi wa habari, Charles alipata ajira yake ya kwanza kwenye iliyokuwa Redio Tanzania Dar Es Salaam (RTD) mwaka 1981.[5] Akiwa na kituo hicho, kipaji chake, sauti yake ya kitangazaji na lafudhi yake murua ya kimwambao, vilimtambulisha mapema kuwa ni bora. Akawa akitegemewa sana katika iliyokuwa Idhaa ya Biashara ambako mvuto wa mtangazaji ulikuwa muhimu sana. Kwenye Idhaa ya Taifa, alikabidhiwa kipaza sauti cha kutangazia mpira mapema kabisa.[6]

Mwaka 1994 Charles Hillary, Julius Nyaisanga (Uncle J.) na Mikidadi Mahmood (Brother Mickey) ambae alikuwa kiongozi wao, walipewa kazi ya kuiasisi na kuindesha iliyokuwa Radio One Sterio (sasa Radio One) na mmiliki wa kituo hicho, hayati Reginald Mengi. Charles alikuwa na mchango usio na kifani akiwa hapo. Ni katika redio hiyo ambako Charles alipewa jina maarufu la Mzee wa Macharanga.

Mwaka 2003 aliondoka nchini Tanzania kwenda Ujerumani alikofanya kazi na redio Deustche Welle (DW Radio). Miaka mitatu baadae, alijiunga na BBC London alikofanya kazi hadi 2015 alipoamua kurejea nchini mwake na kufanya kazi na Azam Media. Desemba 30, 2021 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi alimteua Charles Hillary kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano – Ikulu[7]

Mambo ya kukumbukwa nayo (urathi)

[hariri | hariri chanzo]

Baadhi ya mambo ambayo kwayo Charles atakumbukwa sana ni pamoja na; Kuwa mtangazaji mtanzania wa kwanza kutangaza mechi za Kombe la Dunia kwa Kiswahili akiwa uwanjani (tofauti na kuwa studio na kuangalia mechi kwenye runinga na kuitangaza)[8] Rekodi hiyo aliiweka wakati bara la Afrika nalo likiandikisha rekodi yake kwa mara ya kwanza ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo iliyofanyika Afrika Kusini mwaka 2010.

Charles ndiye aliyeanzisha kipindi cha Charanga time akiwa Radio One na kuufanya muziki huo kupanda chati na kufahamika sana Tz. Kuna aina ya vazi lililopata umaarufu na kuongeza biashara likijulikana kama "Charanga." Hapo hapo Radio One, alianzisha vipindi vya Nani Zaidi, Hizi Nazo, African panorama na hata Habari Nyepesi nyepesi, vilivyopendwa na kudumu kwa miongo mitatu.

Akiwa RTD Charles alipendwa sana na wasikilizaji wa matangazo ya moja kwa moja ya mpira wa miguu. Kadhalika kuisaidia idhaa ya biashara ya redio hiyo kufanya vizuri. Pia, Charles alikuwa msomaji mahiri wa taarifa za habari redioni na kupitia runinga. Sauti yake ya mamlaka na uwezo wa kutamka kiusahihi maneno ya Kiswahili viliwavutia sana wasikilizaji/watazamaji. Charles popote alipokuwa alitumia kipaji na ubunifu wake kuanzisha mambo ya kuifurahisha hadhira, mfano habari fupi za ucheshi.

Kuanzia 2015 aliporejea Tanzania akitokea London, alifungua milango na kutoa miito kwa watangazaji vijana ili awape miongozo mbambali ya kuwajenga kupitia uzoefu wake wa zaidi ya miaka 40 kwenye tasnia hiyo. Ukweli huu umeakisiwa kwenye salamu za pole zilizotolewa na Rais wa awamu ya sita wa JMT Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan.[9]

Hali kadhalika, Charles alikuwa akisifiwa na wanahabari kwa juhudi zake kwenye kukilinda Kiswahili dhidi ya changamoto zinazoikabili lugha hiyo. Alikosoa makosa mbalimbali hususan ya wazi na yanayoashiria kutojali kwa wafanya makosa hayo.

Kufariki dunia

[hariri | hariri chanzo]

Kifo cha Charles, ambaye hakuwa na tabia ya kujipata kama fulani katika jamii bali kujipambanua kama mtu wa watu[10], kilitangazwa mapema na Azam Media asubuhi ya Jumapili ya Mei 11, 2025 na kuwashtua wengi. Sababu ya mauti ilielezwa kuwa ni kuugua kwa ghafla majira ya alfajiri na kufariki njiani akiwa anawahishwa kuelekea hospitali ya Mloganzira kwa matibabu.