Nenda kwa yaliyomo

Karl Peters

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Carl Peters)
Carl Peters (1856-1918)
Peters akitangazwa kama muumba wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani

Karl Peters au Carl Peters (27 Septemba 185610 Septemba 1918) alikuwa mpelelezi na mwanasiasa Mjerumani aliyeanzisha koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Utoto na masomo

[hariri | hariri chanzo]

Peters alizaliwa mwaka 1856 Neuhaus de Elb, ndani ya ngome ya Hannover, katika Ujerumani ya Kaskazini kama mtoto wa nane wa mchungaji wa Kilutheri.

Baada ya kumaliza shule ya sekondari, alisoma historia na falsafa kwenye vyuo vikuu vya Göttingen, Tübingen na Berlin. Akiwa chuoni alivutwa na mafundisho ya Udarwini wa Kijamii yanayotangaza kwamba ni haki na halali kama wenye nguvu duniani wanatawala na kukandamiza watu dhaifu.

Baada ya masomo yake ya historia alifanya kazi London (Uingereza) mnamo 1882/1883. Alijifunza mengi kuhusu himaya ya kikoloni ya Uingereza na utawala wake juu ya nchi nyingi.

Itikadi ya ukoloni

[hariri | hariri chanzo]

Peters alisikitika kuona Ujerumani haikuwa na koloni hadi wakati ule. Aliamini kwamba makoloni huongeza utajiri na enzi ya nchi yenye makoloni jinsi ilivyoonekana katika mfano wa utawala wa Kiingereza juu ya India. Alitaka kuwapatia Wajerumani nafasi waliyostahili machoni pake kati ya mataifa ya Ulaya.

Hadi wakati huo sehemu chache za Afrika zilikuwa makoloni ya Wazungu, isipokuwa Koloni ya Rasi (Afrika Kusini), pwani za Msumbiji na Angola, maeneo madogo ya Afrika ya Magharibi na Algeria. Wakati Peters alipokaa London, mfalme Leopold II wa Ubelgiji alianza kujenga himaya yake Kongo kuanzia mwaka 1878. Jitihada zake, ambazo alizifanya kama mtu binafsi kwa kujitangaza kama mfadhili wa binadamu, zilisababisha mashaka baina ya Ureno na Ufaransa zilizohofia upanuzi wa maeneo ya mfalme wa Ubelgiji katika sehemu ambako waliamini walistahili kipaumbele. Ureno ilifaulu kuvuta Uingereza upande wake, baada ya nchi hii kutazama kwa mashaka uvamizi wa Ufaransa katika Tunisia kwenye mwaka 1881. Uingereza ilihofia upanuzi wa Ufaransa kuwa hatari kwa usimamizi wake wa Mfereji wa Suez na njia ya baharini baina ya Uingereza na Uhindi iliyokuwa koloni tajiri la Uingereza.

Wakati uleule wafanyabiashara wa Hamburg na Bremen kaskazini mwa Ujerumani walikuwa na biashara nzuri na sehemu za pwani ya Afrika ya Magharibi lakini waliona jinsi gani Waingereza na Wafaransa walivyofanya mikataba na watawala Waafrika na kuzuia wanfanyabiashara wasio wa taifa lao. Hasa mapatano ya Sierra Leone baina ya Uingereza na Ufaransa ya mwaka 1883 yaliwashtusha wafanyabiashara Wajerumani, kwa sababu Uingereza na Ufaransa zilipatana hapa kuhusu "maeneo ya athira" katika Afrika ya Magharibi bila mawasiliano na nchi nyingine. Hapo wafanyabiashara kadhaa Wajerumani walianza kudai ulinzi kutoka serikali yao. Serikali chini ya Chansella Bismarck iliwahi kukataa maombi hayo lakini mwisho wa mwaka 1883 alimtuma mwakilishi pamoja na manowari aliyeelekea Afrika ya Magharibi kwa shabaha ya kufanya mikataba na watawala wenyeji pale ambako Waingereza na Wafaransa hawajafanya hivyo bado.

Peters aliporudi Ujerumani mwaka 1883 alijishughulisha, tena kwa nguvu, na siasa ya kudai koloni kwa Ujerumani. Alikuta shirika moja lililounganisha wanasiasa mbalimbali waliopenda kuunda koloni lakini Peters aliwapuuza akiwaona kama watu wanaoongeaongea badala ya kufanya kazi.

Kuanzisha Afrika ya Mashariki ya Kijerumani

[hariri | hariri chanzo]
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Machi 1884 Peters aliunda "Shirika la Ukoloni wa Kijerumani" (Gesellschaft für Deutsche Kolonisation). Peters na wenzake walitaka kununua au kwa namna yoyote kupata maeneo; waliangalia Amerika ya Kusini na pia Afrika Kusini. Waliandaa safari ya kuelekea nchi ya Washona (Zimbabwe) ambako habari za upatikanaji wa dhahabu zilienea. Wakiandaa safari yao walifahamishwa kwamba eneo hili lilikuwa tayari katika upeo wa athira ya Uingereza. Hivyo walibadilisha mpanga wakaamua kulenga Afrika ya Mashariki. Wakati huo himaya pekee iliyotambuliwa kimataifa ilikuwa Usultani wa Zanzibar. Kamati kuu ya shirika ilimpa Peters wito wa kupata maeneo katika Afrika ya Mashariki kwa imani ya kuwa utawala wa Zanzibar ni wa pwani tu.

Peters alipoandaa safari yake mataifa ya Ulaya yalikuwa yakiandaa mkutano wa Berlin kuhusu masuala ya Kongo. Mkutano huo, ulioanza Desemba 1884, ulisababishwa na mipango ya mfalme Leopold II wa Ubelgiji kujijengea himaya ya binafsi katika beseni la Kongo akigongana na shabaha za Ufaransa, Ureno na Uingereza.

Safari ya Usagara

[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 10 Novemba 1884 Peters alifika Unguja pamoja na wanakamati wawili ili aendelee kuzunguka kwenye bara. Serikali ya Kijerumani ya Chansella Bismarck haikukubali mipango yake kwa sababu iliogopa vurugu kwenye mkutano ulioitishwa tayari. Hivyo Peters alipofika kwenye ubalozi wa Ujerumani mjini Zanzibar alipokewa kwa barua kutoka Berlin iliyosema ya kwamba hawezi kutegemea msaada wowote kwani juhudi zake ziko nje ya siasa ya nchi.

Peters akimwogopa Sultani pamoja na Waingereza alivuka kwa siri kutoka Unguja kwenda bara. Alifaulu kutembelea masultani au machifu kadhaa waliotia aina ya sahihi kwenye karatasi walizoonyeshwa na Peters. Karatasi hizo ziliandikwa kwa lugha ya Kijerumani zikisema ya kwamba chifu fulani aliweka eneo lake chini ya mamlaka ya shirika la Kijerumani pamoja na kulipatia shirika hilo haki ya kutumia maeneo na malighafi yote.

Kuna hakika ya kwamba machifu hawakuelewa walichofanya kwa kuchora alama zao kwenye karatasi hizo; walifikiri kwamba wameahidiwa ulinzi kutoka kwa mtawala wa mbali ambaye labda siku moja atakuwa na faida kwao, lakini hawakuelewa kwamba walitoa kibali kwa wageni kutawala nchi.

Peters mwenyewe alisimulia jinsi alivyowapa machifu pombe kali hadi wakawa tayari kuchora alama zao kwenye karatasi walizoonyeshwa bila kuelewa maana yake.

Kwa njia hiyo katika muda mfupi kati ya tarehe 23 Novemba na 17 Desemba 1884 Peters alipata hati kutoka watu alioita machifu wa Usagara, Nguru, Useguha na Ukami kwa ajili ya shirika lake, jumla eneo la km² 140,000.

Kukubaliwa na serikali ya Ujerumani

[hariri | hariri chanzo]

Peters alirudi Ujerumani mnamo Februari 1885 katika siku za mwisho za Mkutano wa Berlin. Aliomba barua ya ulinzi kutoka serikali kwa ajili ya maeneo aliyodai kuwa chini ya shirika la ukoloni. Chansella Mjerumani Bismarck aliendelea kumkatalia. Hati za Peters aliziita karatasi zenye michoro bila thamani ya watu weusi.

Lakini Peters alimtishia kuweka maeneo hayo chini ya ulinzi wa mfalme Leopold II wa Ubelgiji aliyekuwa tayari kupanua himaya yake ya Kongo iliyotambuliwa na serikali za Ulaya wakati wa mkutano. Kutokana na tishio hilo Bismarck alikubali, na Peters akapewa hati rasmi ya kifalme iliyoweka maeneo ya shirika la koloni chini ya ulinzi wa Dola la Ujerumani.

Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki

[hariri | hariri chanzo]

Sultani wa Zanzibar hakufurahishwa na habari hizo, akapinga kwa telegramu aliyotumia Berlin akidai kuwa Peters aliingia bila kibali na kufanya mikataba na machifu waliokuwa chini ya Zanzibar. Lakini baada ya kutoa barua za ulinzi Berlin iliona haja ya kusimama imara ikapeleka manowari 8 huko Zanzibar chini ya admeri Knorr. Sultani alikosa uwezo wa kushindana na jeshi hilo akakubali mikataba ya Peters na kwamba Wajerumani watumie bandari ya Daressalaam.

Wakati huo Peters mwenyewe alibaki Ujerumani na kuandaa upanuzi wa himaya ya shirika lake. Aliunda kampuni jipya la "Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki" lililochukua nafasi ya shirika la awali. Shirika lilituma maafisa kwa misafara mipya na kuongeza mikataba na machifu, na hivyo kuongeza eneo lililodaiwa na shirika.

Pia aliwasiliana na madhehebu ya Ujerumani ili kupata wamisionari ambao wasaidie malengo yake. Lakini itikio lao lilikuwa tofauti. Kwa mfano, tarehe 18 Aprili 1887 padri Andreas Amrhein, mwanzilishi wa Wabenedikto wamisionari wa Mt. Otilia, alimuandikia hivi Papa Leo XIII kuhusu mazungumzo yake na Peters: "Wao wanataka wamisionari kwa ajili ya faida yao wenyewe. Lakini nimeweka masharti: wamisionari wafanye kazi yao kwa uhuru wote, bila kupingwa kwa namna yoyote na wakoloni. Licha ya hayo naona kwamba wamisionari wataweza kuwalinda wenyeji wasinyonywe ovyo na wakoloni na wafanyabiashara" [1].

Mwaka 1887 Karl Peters alirudi Afrika kama mkurugenzi wa utawala wa kampuni. Aliingia katika majadiliano na Sultani Barghash ibn Sa'id kuhusu utawala wa pwani.

Baada ya kifo cha Bargash mwaka 1888 Peters alifaulu kumshawishi Sultani mpya Khalifa ibn Sa'id kulikodisha eneo lote la pwani kwa Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki.

Msafara wa Emin Pasha na kulenga Uganda

[hariri | hariri chanzo]

Peters alirudi Ujerumani alipoombwa kuongoza msafara mpya wa kumtafuta Emin Pasha katika eneo kati ya Uganda na Sudan. Emin Pasha alikuwa Mjerumani kwa jina la Dr. Eduard Schnitzer ambaye aliingia katika utumishi wa serikali ya Misri, kuwa Mwislamu na gavana wa jimbo la Ikweta katika Sudan ya Kimisri. Baada ya mapinduzi ya Mahdi mwaka 1885 mawasiliano kati ya Emin Pasha na serikali ya Misri ilikatwa; kamati mbalimbali ziliundwa Ulaya kwa shabaha ya kumwokoa.

Peters alifika tena Afrika ya Mashariki mwaka 1889 akaanza msafara wake mnamo Juni 1889 kutoka Witu kwenye pwani ya Kenya iliyokuwa eneo lindwa chini ya Ujerumani. Bila ya Peters wala watu wengine kujua, Emin Pasha hakuwa na haja yoyote ya kuokolewa, lakini kwa hiari yake alikuwa tayari safarini kuelekea Bagamoyo pamoja na mpelelezi Mwingereza Henry Morton Stanley. Lakini Peters, mbali ya kumtafuta Emin Pasha, alikuwa na shabaha yake mwenyewe: kupanua eneo la shirika lake. Kote alikopita alifanya mikataba mipya na machifu na masultani wa kikabila, kwa mfano na chifu wa Kavirondo (Kisumu) tarehe 1 Februari 1890.

Hayo yote aliyafanya ingawa alijua kwamba serikali za Ujerumani na Uingereza ziliwahi kupatana kuhusu maeneo ya Afrika ya Mashariki zilipolenga kutafuta masilahi yao bila kuingiliana. Msafara wa Peters ulipita kabisa katika eneo lililoahidiwa kwa Uingereza. Lakini kufuatana na mapatano ya mkutano wa Berlin wa 1885 utawala wa nchi ya Ulaya katika Afrika ulitambuliwa mradi nchi iweze kuonyesha utawala wake halisi. Kumbe Waingereza hadi kupita kwa Peters walikuwa hawajachukua hatua zozote za kujenga utawala wao katika sehemu za Kenya.

Mkataba na Buganda

[hariri | hariri chanzo]

Kilele cha juhudi za Peters kilikuwa mapatano na Kabaka Mwanga II wa Buganda ya Machi 1890. Mwanga hakupendezwa na wamisionari Waingereza na Wafaransa walioshindana kati yao ili kuwa na athari kubwa huko Buganda. Labda kwa matumaini ya kwamba huyu mfalme wa Ujerumani asiyejulikana kwake atakuwa msaada dhidi ya siasa za Waingereza lakini atakuwa mbali mno asiweze kuleta hasara, Kabaka alitia sahihi kwenye mapatano ya urafiki na ulinzi kati ya Ujerumani na Buganda. Tendo hilo lilitekelezwa na Karl Peters bila kibali wala ujuzi wa serikali yake nyumbani.

Peters alirudi kutoka Buganda kuelekea pwani. Tarehe 20 Juni 1890 huko Mpwapwa alikutana na Emin Pascha aliyekuwa tayari njiani kurudi kwake Ikweta. Mwezi Julai 1890 Peters alifika Bagamoyo.

Jinsi alivyowatenda Waafrika

[hariri | hariri chanzo]

Katika msafara huo tabia za Peters zilionyesha jinsi alivyodharau Waafrika. Aliamini na kuandika kwamba Mwafrika hutawaliwa kwa kiboko tu. Kwake Mwafrika hakuwa mtu kamili. Akijiona mwenyewe ni bwana ambaye wenyeji wanapaswa kumtumikia, aliwadharau.

Alipopitia Ugogo alimkasirikia Mgogo aliyecheka alipomtazama akinyoa ndevu zake, akaamuru apigwe kiboko. Tendo hilo liliwasababisha Wagogo kuchukua silaha, ikawa vita ambapo watu wakauawa kwa wingi.

Watu waliosafiri naye na kumjua walisimulia jinsi alivyowapiga mara nyingi mahamali au watumishi wake, hata akapewa nao jina “mkono damu”.

Mwisho wa himaya ya Peters na shirika la ukoloni

[hariri | hariri chanzo]

Uasi kwenye pwani dhidi ya utawala wa shirika

[hariri | hariri chanzo]

Wiki chache tu baada ya Peters kuanzisha safari yake ya kumtafuta Emin Pasha, utawala wa shirika lake uliporomoka vibaya. Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki lilianza kutekeleza mapatano na Sultani wa Zanzibar kuhusu utawala wa pwani mnamo Agosti 1889.

Kushushwa kwa bendera ya Sultani na kupandishwa kwa bendera ya shirika kulishtusha wenyeji wengi. Maafisa Wajerumani wa shirika walionyesha ukali wakidai utawala juu ya bandari. Hayo yote yalisababisha mara moja ghasia. Wenyeji wakaongozwa na watu kama Abushiri na Bwana Heri. Uasi ulianza Pangani na kuenea kote pwani na kuwa vita kabisa. Shirika lilishindwa kupambana na upinzani huo wa wenyeji.

Hapo serikali ya chansella Bismarck iliingilia kati na kutuma manowari pamoja na wanajeshi waliokomesha upinzani wote. Maeneo ya shirika yaliwekwa chini ya serikali ya Ujerumani kama koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Utawala wa shirika la Peters ulikwisha.

Mkataba wa Helgoland-Zanzibar kuingilia kati

[hariri | hariri chanzo]

Karl Peters aliporudi pwani mwezi Julai 1890 alipokea habari hizo pamoja na habari za Mkataba wa Helgoland-Zanzibar wa tarehe 1 Julai 1890 kati ya serikali za Uingereza na Ujerumani zilimoelewana juu ya mipaka ya maeneo yao katika Afrika. Waingereza walikuwa wameshtushwa na matendo ya Peters ya kulenga Uganda. Serikali mpya ya Ujerumani ya chansella Caprivi iliona kuwa uhusiano mzuri na Uingereza ni muhimu kuliko kuongeza makoloni yaliyotazamwa na sehemu ya wanasiasa Ujerumani kwa mashaka.

Katika mkataba huo Wajerumani walikubali kuwa maeneo ya Uganda, Zanzibar na nchi kaskazini kwa mstari kati ya Ziwa Viktoria (Nyanza) na mlima Kilimanjaro pamoja na Witu yawe chini ya athira ya Uingereza. Waingereza waliahidi kwamba watamshawishi Sultani wa Zanzibar kuwapatia Wajerumani pwani ya sehemu iliyoitwa baadaye "Tanganyika". Mapatano mengine yalihusu mipaka kati ya maeneo ya Waingereza na Wajerumani huko Afrika ya Magharibi na kisiwa cha Helgoland katika Bahari ya Kaskazini.

Peters aliona safari yake ilikuwa bure kabisa. Alisikitika na kufoka dhidi ya wanasiasa huko Berlin. Aliporudi Ujerumani tena alijiunga na wengine waliodai siasa kali ya ukoloni akawa mmojawapo wa waanzilishi wa "Jumuiya ya Wajerumani Wote" (Alldeutscher Verband). Jumuiya hiyo ilitangaza utaifa mkali, chuki dhidi ya mataifa majirani na Wayahudi, dhaurau dhidi ya watu wenye rangi tofauti na madai ya kuwa Ujerumani ilistahili maeneo makubwa zaidi katika Ulaya na katika mabara mengine.

Unyama wa Peters Kilimanjaro na kufukuzwa kwake

[hariri | hariri chanzo]

Kamishna wa Kaisari

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Peters kurudi Berlin sehemu ya wanasiasa na magazeti walimshangilia na kumsheherekea kama shujaa wa kitaifa aliyezuiwa na waoga serikalini waliothamini uhusiano na watu wa nje kama Waingereza kuliko masilahi ya taifa.

Mwaka 1891 serikali iliamua kutumia maarifa ya Peters kwa kumpa cheo cha "Kamishma wa Kaisari katika eneo la Kilimanjaro". Kazi yake kuu ilikuwa kuelewana na Waingereza kuhusu mpaka kamili kati ya sehemu za Wajerumani na Waingereza. Pia alikuwa mkuu wa utawala wa kikoloni wa eneo hilo.

Mapenzi na mauti

[hariri | hariri chanzo]

Akiwa mwakilishi wa Ujerumani Kilimajaro, Peters alikuwa na mabinti wenyeji aliowatumia kama wapenzi wake. Usiku wa tarehe 18 Oktoba 1891 Peters alimkuta binti Yagodja akilala pamoja na Mabruk, mtumishi wa kiume. Peters alikasirika mno akaita mara moja kamati ya mahakama akiwa yeye mwenyewe mwenyekiti. Mabruk alihukumiwa anyongwe. Yagodja alikimbia lakini akakamatwa mnamo Januari 1892 akapigwa viboko na kunyongwa naye.

Katika hasira yake Peters aliamuru hata kijiji cha binti huyo katika eneo la Rombo kichomwe moto. Wachagga wa Rombo walichukua silaha na kujihami. Hasira ya Peters ilisababisha vita vya miezi kadhaa, vijiji vingi viliharibika na watu kufa.

Kesi dhidi yake

[hariri | hariri chanzo]

Mnamo Aprili 1892 gavana Mjerumani von Soden mjini Daressalaam alipokea barua kutoka kwa mmisionari Mwingereza Smythies alimoandika sababu za vita Kilimanjaro kuwa ni unyama wa Peters. Von Soden alifanya utafiti akatuma taarifa juu ya matendo ya Peters kwenda Berlin. Gavana aliandika ya kwamba kwa maoni yake adhabu za kifo hazikuwa za haki, kwa sababu Peters alitumia madaraka yake vibaya kwa kiburi na kisasi cha binafsi.

Awali serikali ya Berlin ilipendelea kutochukua hatua dhidi ya Peters. Gavana von Soden aliona aibu ya kuwa Peters alitenda maovu hayo wakati ana wajibu kwa ajili ya koloni, lakini hakuwa na uwezo wa kumwondoa madarakani kwa sababu ya cheo chake Peters. Von Soden alimsisitizia kuacha cheo chake hadi mwishoni Peters akajiuzulu mwaka 1893.

Mambo yalibadilika baada ya wabunge wa upinzani katika "Reichstag" kupata habari za Peters na kuuliza maswali bungeni. Peters aliitwa arudi Berlin akapewa kazi wizarani. Kamati ya nidhamu ilifungua kesi dhidi yake na kumfanyia utafiti.

Peters alipoona mambo yanaweza kwenda vibaya aliomba kupumzika, akahamia London. Kamati ya nidhamu iliamua tarehe 24 Aprili 1897 kuwa Peters alikosa. Alifutwa katika utumishi wa serikali pamoja na kupoteza haki za pensheni (malipo ya uzeeni). Mahakama kuu ya nidhamu ilirudia tamko hilo vikali zaidi Peters alipokata rufaa.

Maisha yake baada ya kuondolewa katika utumishi wa serikali

[hariri | hariri chanzo]

Alipokaa tena London Peters aliunda makampuni ya kutafuta dhahabu Kusini mwa Afrika kwa jina la Dr. Carl Peters Estates and Exploration Co. na South East Africa Ltd. akasafiri mara sita kwenda Zimbabwe, Msumbiji na Afrika Kusini.

Mwaka 1905 Kaisari Wilhelm II, aliyekuwa mshabiki wa Peters, alimpa haki ya kutumia tena kwa heshima yake cheo cha “Kamishna wa Kaisari”.

Mwanzoni mwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia alirudi Ujerumani kwa sababu makampuni yake katika himaya ya Uingereza yalinyimwa nafasi kama mali ya adui. Kaisari alimsaidia tena kwa kumpa pensheni kutoka makisio yake binafsi.

Karl Peters aliaga dunia kabla ya mwisho wa vita tarehe 10 Septemba 1918. Hakukumbukwa sana isipokuwa na vikundi kadhaa vilivyodai Ujerumani irudishiwe makoloni yake iliyonyang’anywa baada ya vita.

Tangu mwaka 1933 serikali ya Adolf Hitler ilimkumbuka na kumheshimu ikimtambua kama mtangulizi wa itikadi yake. Barabara na viwanja katika miji mbalimbali vikapewa jina lake.

Mwaka 1936 Adolf Hitler alitamka kwa amri ya pekee kuwa hukumu dhidi ya Peters ifutwe na mjane wake apewe pensheni yake.

Baadaye barabara zilizoitwa kwa jina la Peters zilibadilishiwa jina kwa sababu miji kadhaa iliona ni aibu kutunza kumbukumbu yake kwa njia hiyo.

  1. Kanisa katika Tanzania, V2, Kitabu cha Mwalimu, Ndanda Mission Press, 1975, uk 22.


Nchi za Afrika Bara la Afrika
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira