Nenda kwa yaliyomo

Khalifa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Caliph)
Eneo la utawala wa makhalifa wakati wa mwisho wa Wamuawiya mw. 750

Khalifa, ni cheo cha kihistoria kwa ajili ya kiongozi wa umma (jumuiya ya Uislamu). Ni neno la Kiarabu خليفة khalīfah linalomaanisha "makamu". Khalifa ni kifupi chake cha خليفة رسول الله "khalifatu-rasul-i-llah" kinachomaanisha "Makamu wa mtume wa Allah/Mungu". Hivyo mana yake ni makamu au mfuasi wa Mtume Muhammad katika nafasi yake kama kiongozi wa Waislamu.

Cheo cha khalifa kilitumiwa pamoja na cheo cha "amīr-al-mu'minīn" ( أمير المؤمنين ) "Jemadari Mkuu wa wenye Imani (=Waislamu)".

Utaratibu wa uongozi wa khalifa ulianzishwa baada ya kifo cha Mtume Muhammad mwaka 632 na kuishia 3 Machi 1924 katika mapinduzi ya Atatürk.


Makhalifa wanne wa kwanza

[hariri | hariri chanzo]

Mtu wa kwanza aliyetumia cheo hiki alikuwa (Abu Bakr aliyeongoza ummah ya Waislamu baada ya kifo cha Mtume Muhammad mwaka 632. Alichaguliwa na viongozi wa Waislamu kwa sababu Muhammad hakumwacha mrithi wala maagizo kuhusu atakayemfuata kama kiongozi.

Abu Bakr alifuatwa na Umar ibn al-Khattab, Uthman ibn Affan na Ali ibn Abi Talib.

Hawa wanne ni viongozi katika historia wanaokubaliwa na mikondo karibu yote ya Uislamu kwa sababu walichaguliwa na wafuasi wa Mtume Muhammad wenyewe. Isipokuwa kikundi kidogo cha Wakhariji wanaokubali makhalifa wawili wa kwanza pekee. Washia[1] wanafundisha ya kwamba Ali angepaswa kuwa khalifa tangu mwanzo.

Baada ya kifo cha Ali Bin Abiy Twalib lilitokea farakano kati ya Waislamu: wachache waliwataka wana wa Ali kundelea kuongoza lakini walio wengi walimfuata Muawiya (mkuu wa jeshi la Waislamu huko Dameski) aliyepigana na Ali na mwanawe Hussain kijeshi na kushinda.

Wamuawiya, Waabbasi na Waosmani

[hariri | hariri chanzo]

Muawiya kama jemadari ya Waislamu wa Dameski alikuwa khalifa mwaka 661 baada ya kifo cha Ali. Tangu Muawiya hakuna khalifa tena aliyechaguliwa; Muawiya alimteua mwanawe Yazid amfuate. Tangu siku zile cheo cha Khalifa kiliendela ama kwa mfuasi aliyeteuliwa na mwenye cheo au kilinyanganywa kwa njia ya kijeshi.

Wafuasi wa Muawiya waliendelea kutawala hadi 750 walipopinduliwa na wafuasi wa Abbas mjomba wa mtume Muhammad. Mmuawiya mmoja tu aliweza kukimbia hadi sehemu ya Hispania iliyotekwa na Waarabu alipopokelewa kwa heshima na kuanzisha Ukhalifa wa Wamuawiya wa Cordoba uliodumu katika Hispania hadi 1031.

Harun ar-Rashid alikuwa mashuhuri kati ya makhalifa Waabbasi

Waabbasi

[hariri | hariri chanzo]

Waabbasi walitwala mjini Baghdad hadi mnamo mwaka 945. Khalifa mashuhuri hasa kati hao alikuwa Harun ar-Rashid aliyebadilishana mabalozi na Uchina na Kaisari Karolo Mkuu mnamo mwaka 802. Baadaye nguvu ya kitawala ilikuwa mkononi wa viongozi wa vikosi vya ulinzi wasiokuwa Waarabu lakini Wajemi au Waturuki. Mwaka 1258 Wamongolia walishambulia na kuharibu mji wa Baghdad na kumwua khalifa Al-Mustasim. Mjomba wake al-Mustansir aliweza kukimbilia Misri alipopewa cheo cha Khalifa na mtawala wa nchi Sultani Baibars. Makhalifa waliomfuata katika Misri walikuwa viongozi kwa jina tu waliowategemea kabisa watwala wa Misri.

Mwaka 1517 khalifa wa mwisho wa Waabbasi Al-Mutawakkil III alikamatwa na Waturuki Waosmani walipovamia Misri. Wakampeleka Istanbul kama mfungwa alipokabidhi cheo chake pamoja na simi na koti ya Mtume Mohammad kwa Sultani Selim I.

Waosmani

[hariri | hariri chanzo]

Watawala Waosmani hawakujali sana cheo cha khalifa. Walijiita hasa "Sultani" pamoja na vyeo vingine. Walitumia cheo cha khalifa hasa katika uhusiano na Waislamu nje ya dola lao. Kwa mafano wakishambulia nchi za Kiislamu kama Uajemi walijiita Khalifa wakidai utii kama wakuu wa Waislamu wote. Au wakishambuliwa na Austria au Urusi walitumia cheo cha khalifa kuita Waislamu wote kujiunga na jihad ya kivita.

Safari ya mwisho ya kutumia cheo cha khalifa kwa wito la jihad ya kivita ilitokea wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ambako Sultani Mehmed V alitumia tena cheo chake cha khalifa kuita waislamu wote wa dunia kujiunga na vita dhidi ya Uingereza.

Mwisho wa ukhalifa

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya vita cheo kilifutwa na bunge la Uturuki kwa mapendekezo ya Atatürk mwaka 1924.

Khalifa mbalimbali wa kihistoria

[hariri | hariri chanzo]

Nje ya ufuatano rasmi ya makhalifa kulitokea pia cheo cha khalifa katika maeneo mbalimbali kwa kushhindana na khalifa rasmi ni nani mwenye cheo cha kweli.

Mifano ni:

Majaribio ya kukufua ukhalifa

[hariri | hariri chanzo]

Tangu mwaka huu walijitokeza viongozi wa vikundi mbalimbali waliodai cheo cha khalifa lakini bila kukubaliwa na Waislamu wengi.

  • Mfano mmojawapo ni kundi la Mturuki Cemaleddin Kaplan aliyejitangaza [1994] kuwa khalifa. Alikuwa na wafuasi elfu kadhaa kati ya Waturuki nchini Ujerumani. Baada ya kifo chake mashindano juu ya cheo kilisababisha kuuawa kwa mfuasi mmoja na kikundi kilipigwa marufuku na serikali ya Ujerumani.
  • Kati ya Waislamu wenye mwelekeo mkali kuna mafundisho ya kwamba cheo cha khalifa kinapaswa kurudishwa kama utaratibu wa kisiasa cha kufaa. Mfano wake ni chama cha Hizb ut-Tahrir kilichopigwa marufu katika nchi zote.
  • Tarehe 29 Juni 2014 kiongozi wa kundi la Daish (Dola la Kiislamu katika Iraqi na Shamu) alijitangaza kuwa khalifa akidai Waislamu wote duniani kumtii. Tangazo la ukhalifa lilikuwa sababu kwa vikundi vingine vikali kama vile Al Qaida kuwa adui zake.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Khalifa kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. "History of Shia Islam", Wikipedia (kwa Kiingereza), 2022-11-08, iliwekwa mnamo 2023-02-26