Kalenda
Kalenda ya Gregori | 2025 MMXXV |
Kalenda ya Kiyahudi | 5785 – 5786 |
Ab urbe condita (Roma ya Kale) | 2778 |
Kalenda ya Ethiopia | 2017 – 2018 |
Kalenda ya Kiarmenia | 1474 ԹՎ ՌՆՀԴ |
Kalenda ya Kiislamu | 1447 – 1448 |
Kalenda ya Kiajemi | 1403 – 1404 |
Kalenda za Kihindu | |
- Vikram Samvat | 2080 – 2081 |
- Shaka Samvat | 1947 – 1948 |
- Kali Yuga | 5126 – 5127 |
Kalenda ya Kichina | 4721 – 4722 甲辰 – 乙巳 |
Kalenda ni utaratibu wa kupanga wakati. Hupatikana kama orodha ya vipindi vya wakati kama vile siku, juma, mwezi na mwaka. Kalenda mbalimbali zimejua pia vipindi vya miaka kadhaa.
Kalenda inayotumika zaidi leo kimataifa ni kalenda ya Gregori iliyo muhimu kwa uchumi na biashara. Kuna pia nchi zinazotumia hasa kalenda zao za kitaifa au kalenda mbalimbali sambamba.
Hasa maisha ya kidini hupangwa kufuatana na kalenda maalumu. Kihistoria palikuwako na kalenda nyingi.
Migawanyo asilia ya wakati
[hariri | hariri chanzo]Mchana na usiku
[hariri | hariri chanzo]Kwa watu wengi duniani mabadiliko ya mchana na usiku ni utaratibu wa kwanza unaogawa wakati. Mchana na usiku pamoja inahesabiwa kama siku moja. Lakini kuna njia tofauti jinsi gani kuanza hesabu hiyo: asubuhi (mwanzo wa mchana) au jioni (mwanzo wa usiku) zilikuwa njia za kawaida za kuhesabu siku mpya. Tangu kupatikana kwa saa zinazoonyesha masaa hata gizani ni saa sita usiku (katikati ya usiku) inayoangaliwa kuwa mwanzo wa siku mpya.
Awamu za mwezi
[hariri | hariri chanzo]Awamu za mwezi huonekana vizuri kwa kila mtu. Kwa sababu hii awamu hizi zilikuwa mbinu unaoeleweka rahisi kupanga siku kwa vipindi. Kipindi kutoka mwezi mpya hadi mwezi mpya ni kipimo kinachopatikana katika kila nchi ni siku 29 1/2.
Majira kama msingi wa hesabu ya mwaka
[hariri | hariri chanzo]Majira au badiliko la vipindi vinavyorudi vya joto na baridi au vya ukame na mvua vilikuwa utaratibu mwingine ulioonekana kwa watu. Ila tu hesabu hii ilitegemea na mazingira na hali ya hewa katika eneo fulani.
Hasa katika nchi ambako majira yanatofautiana vikali na kufuata utaratibu wa kurudia hata mimea na wanyama hufuata mwendo wa majira. Katika mazingira kama hii imewezekana kutofautisha matokeo katika maisha kufuatana na idadi ya vipindi vya baridi au vya joto au vya mvua vilivyopita tangu tokeo fulani.
Mabadiliko ya mimea hutegemea mwendo wa jua na idadi ya mwanga pamoja na joto linalopatikana katika sehemu mbalimbali za dunia. Katika nchi karibu na ikweta tofauti hizi mara nyingi si kali sana na majira hazionekani vizuri isipokuwa majira ya mvua na ukame. Katika nchi hizi kalenda za kale mara nyingi zilitegemea nyota hasa Zuhura (Ng'andu) na mahali angani inapoonekana asubuhi au jioni kwa wakati fulani.
Kilimo na mwanzo wa Kalenda
[hariri | hariri chanzo]Inaaminika ya kwamba tangu kuanza kilimo watu wameanza pia kushika kumbukumbu ya wakati. Katika nchi nyingi kupanda na kuvuna kunategemea mwendo wa majira yanayorudia. Kazi ya pamoja inahitaji mpangilio na lugha ya pamoja. Hapa ni mwanzo wa kalenda.
Aina za kalenda
[hariri | hariri chanzo]Kutokana na migawanyo asilia ya wakati zilitokea njia mbalimbali jinsi ya kupanga wakati katika kalenda. Kutokana na hapo kuna hasa kalenda ya mwezi, kalenda ya jua na kalenda ya lunisolar (=kalenda jua-mwezi) inayounganisha mwaka kufuatana na mwendo wa jua na vipindi halisi vya mwezi.
Kalenda za mwezi
[hariri | hariri chanzo]Kalenda hizi hufuata awamu za mwezi. Kutoka mwezi mwandamu (=mwezi mpya) hadi mwezi mwandamu unaofuata ni muda wa siku 29 na nusu. 12 za vipindi hivi ni takriban sawa na mwaka 1 yaani kipindi hadi kurudia kwa majira kama joto au baridi. Lakini kuna tofauti kati ya mwaka wa jua unaotawala kurudi kwa majira baada ya siku 365 ¼ na muda wa miezi halisi 12 mwenye siku 354 pekee.
Hii ni hasara ya kalenda ya mwezi ya kwamba baada ya miaka kadhaa hailingani tena na majira kwa hiyo ni vigumu kupanga kilimo kufuatana na kalenda hii. Lakini katika maeneo ya dunia ambako majira si muhimu vile kalenda za mwezi zinaendelea kutumiwa. Mfano maarufu wa kalenda ya mwezi ni kalenda ya Kiislamu; hapo kipindi cha „mwezi kinalingana kabisa na awamu za mwezi angani na baada ya miezi 12 ya aina hii mwaka mpya mwenye muda wa siku 354.3 unaanza tena. Ilhali mwaka huu una upungufu ya siku 11-12 kulingana na mwaka wa jua sikuu zake „zinatembea“ kutoka majira hadi majira; katika mazingira ya jangwa ya Uarabuni ulikotokea kilimo na majira hayakuwa muhimu vile.
Kalenda ya Jua
[hariri | hariri chanzo]Nchi nyingi za dunia zinategemea kilimo. Kilimo hufuata majira ya hali ya hewa. Majira haya hutawaliwa na jua yaani na kiasi cha mwanga na nishati zinazofika dunianikutoka kwa jua na hii inabadilika kutokana na umbali wa jua unaobadilika katika mwendo wa dunia kuzunguka jua letu. Mwendo huu wa dunia kuzunguka jua unachukua siku 365 ¼ kwa hiyo watu katika tamaduni mbalimbali baada ya kugundua muda huu walitunga kalenda zilizoshika mwendo huo.
Kalenda hizi zinaweza kugawiwa kwa namna mbalimbali lakini mara nyingi zinatumia vipindi 12. Vpindi hivi vinaweza kuitwa „mwezi“ lakini havina uhusiano tena na awamu halisi za mwezi.
Kalenda ya jua maarufu ni kalenda ya Gregori iliyokwa kalenda ya kimatifa hasa.
Kalenda jua-mwezi (lunisolar)
[hariri | hariri chanzo]Kalenda jua-mwezi zinalenga kuunganisha mwaka wa jua na mwendo wa majira kwa pande mmoja na awamu halisi za mwezi kwa upande mwingine.
Kwa hiyo kalenda hizi zinatumia vipindi vya mwaka vya mwezi yaani miezi halisi 12. Kila baada ya miaka 2 – 3 kuna mwaka mrefu mwenye miezi 13. Kwa njia hii upungufu wa mwaka wa mwezi kulingana na mwaka wa jua unasawazishwa.
Mifano mashuhuri wa hesabu hii ni kalenda ya Kiyahudi na Kalenda ya Kichina.
Hesabu ya mwaka
[hariri | hariri chanzo]Kalenda zote hutumia hesabu inayoanza kwenye tarehe fulani ya chanzo.
Kalenda ya kimataifa (=Kalenda ya Gregori) huanza hesabu yake katika mwaka ulioaminiwa kuwa mwaka wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo na hesabu hii huitwa baada ya Kristo. Hesabu hii imefikia baada ya mwaka 2010.
Kalenda ya Kiislamu huanza hesabu yake katika mwaka wa hijra yaani kuondoka kwa Muhamad kutoka Maka kwenda Madina. Hesabu hii imefika zaidi ya miaka 1430.
Kalenda ya Kiyahudi inaanza hesabu katika mwaka ulioaminiwa kuwa uumbaji wa dunia na leo imefikia hesabu ya zaidi ya miaka 5770.
Kalenda za Kisasa
[hariri | hariri chanzo]Hata leo hii kuna kalenda mbalimbali zinazotumiwa duniani. Kalenda inayotumiwa zaidi kimataifa ni kalenda ya Gregori inayohesabu miaka tangu Kristo kuzaliwa. Kalenda hii imepokea muundo wake kutoka kalenda ya Roma ya Kale hasa miezi na idadi ya siku zao.
Kalenda nyingine inayotumiwa katika nchi kadhaa ni kalenda ya Kiislamu inayohesabu miaka tangu hijra ya Muhamad; kalenda hii hutumiwa na Waislamu wote kwa kukadiria sikukuu zao hata wakitumia menginevyo kalenda ya Gregori.
Kalenda nyingine ni kalenda kama ile ya Kichina, ya Kihindi na kadhalika zinazotumiwa kwa makadirio ya sikukuu katika dini au utamaduni wao lakini kwa maisha ya kawaida watu wengi wanatumia kalenda ya Gregori.
Nchi kadhaa huwa pia na namna ya pekee za kalenda kwa mfano Ethiopia hufuata kalenda yake inayohesabu tangu kuzaliwa kwake Kristo lakini kwa tofauti ya hesabu ya miaka 7 na miezi 3; ina miezi 13. Kalenda ya Uajemi huhesabu miaka tangu hijra lakini tofauti na Waislamu wengi hutumia mwaka wa jua si mwaka wa mwezi kwa hiyo kuna tofauti ya takriban miaka 40 hivi.
Wiki
[hariri | hariri chanzo]Hesabu ya wiki haifuati kalenda ni kipindi cha siku 7 kinachorudia mfululizo bila kujali mwisho au mwanzo wa mwaka. Asili yake iko katika Mashariki ya Kati hasa Babeli ikasambazwa kupitia imani ya Uyahudi na Ukristo. Inaanza kwa siku ya Jumapili inayotazamiwa kidini kama siku ya kwanza ya uumbaji wa dunia na kwa wakristo pia siku ya ufufuo wa Yesu unaotazamiwa kama uumbaji wa pili. Kwa kusudi la kupanga maisha na hasa kazi wiki za mwaka zinahesabiwa kuanzia 1 - 52; hapo wiki ya kwanza na wiki ya mwisho kwa kawaida si kamili kwa sababu siku kadhaa zimo katika mwaka uliotangulia au kufuata.
Tangu kuenea desturi ya wikendi yaani mapumziko ambako wengi hawafanyi kazi siku za Jumapili na Jumamosi kalenda nyingi huonyesha siku ya kwanza ya wiki ambayo ni Jumatatu kama chanzo cha wiki ya kazi.
Mpangilio wa wiki kama hesabu ya siku ya kupumzika na siku za kazi umeenea kote duniani hasa kwa ofisi za serikali ingawa katika nchi nyingi watu maskini hawana nafasi za kupumzika mara kwa mara.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Kalenda ya Gregori
- Kalenda ya Juliasi
- Kalenda ya Kiislamu
- Kalenda ya Kiyahudi
- Kalenda ya Jua
- Kalenda ya Mwezi
- Mwaka wa Jua
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kalenda kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |