Brother Zeno
| Brother Zeno | |
|---|---|
| Jina la kuzaliwa | Zeno Andrea Lucas |
| Amezaliwa | Juni 28, 1946 Tanzania |
| Amekufa | Juni 27, 2017 (umri 70) Tanzania |
| Aina ya muziki | Muziki wa dansi |
| Kazi yake | mwimbaji/mtunzi wa nyimbo, mwanamuziki, mchambuzi wa muziki |
| Ala | Sauti, gitaa |
| Miaka ya kazi | Miaka ya 1970 - kifo |
Zeno Andrew Lucas (jina maarufu: Brother Zeno; 28 Juni 1946 – 27 Juni 2017) alikuwa mwanamuziki wa muziki wa dansi kutoka nchini Tanzania.
Ndugu Zeno, pia alikuwa mchambuzi mahiri wa muziki wa charanga. Zeno anahesabiwa kama mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Dar es Salaam Jazz Band B (iliyokuwa na mgawanyo wa A na B), bendi iliyokuwa ikiongozwa na Patrick Balisidya. Bendi hii ilipata umaarufu kwa kasi na kuonekana kuwa tishio kwa Dar es Salaam Jazz Band A chini ya uongozi wa Michael Enoch. Hatimaye, bendi B ilivunjwa, na baadhi ya wanamuziki wake wakaingizwa kwenye bendi A. Hata hivyo, Patrick Balisidya aliondoka na kuanzisha bendi maarufu ya Afro 70, ambayo ilifanya mapinduzi makubwa katika muziki wa dansi nchini Tanzania.
Baadaye, Brother Zeno alijiunga na Shirika la Bima la Taifa, ambako alitoa wazo la kuanzishwa kwa bendi ya shirika hilo, Bima Jazz Band. Pia alipewa jukumu la kuandaa na kutafuta wanamuziki wa kujiunga na bendi hiyo. Yeye mwenyewe alikuwamo kati ya waanzilishi wa kundi hilo, ambalo baadaye lilijipatia umaarufu mkubwa katika tasnia ya muziki wa dansi.
Kwa upande wa uchambuzi wa muziki, enzi hizo akiwa na Mzee wa Macharanga, Charles Hillary, kupitia Radio One, Zeno alikuwa na ufahamu mkubwa wa muziki kutoka Cuba. Ufahamu huu ulimfanya kuwa kipenzi cha watu waliothamini muziki wa charanga na mtindo wake wa kipekee.
Zeno alifariki tarehe 27 Juni, mwaka 2017 katika hospitali ya Temeke alipokuwa anauguzwa tatizo la moyo ambalo lilikuwa likimsumbua kwa takriban mwaka mmoja.[1][2]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Kifo cha Zenno katika blogu ya Soma Latest.
- ↑ HATIMAE MWANAMUZIKI MKONGWE BROTHER ZENNO AZIKWA mazishi ya Zeno katika blogu ya Tanzania Rhumba.
| Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Brother Zeno kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |