Nenda kwa yaliyomo

Brice Clotaire Oligui Nguema

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rais wa Gabon, Brice Clotaire Oligui Nguema

Brice Clotaire Oligui Nguema (alizaliwa 1975) ni mwanajeshi na mwanasiasa kutoka nchini Gabon ambaye ni Rais wa sasa wa nchi hiyo tangu Aprili 2025, baada ya kushinda uchaguzi wa kwanza uliofanyika kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya 2023 yaliyomuondoa madarakani Ali Bongo Ondimba[1].

Maisha ya awali

Oligui Nguema alizaliwa katika mkoa wa Haut-Ogooué, eneo linalohusishwa pia na familia ya Bongo. Alipata elimu ya kijeshi nchini Morocco katika Chuo cha Jeshi cha Meknes na alihudumu katika Jeshi la Gabon kwa miaka mingi kabla ya kuingia rasmi katika siasa.

Kazi ya kijeshi

Kabla ya kushika uongozi wa kisiasa, Oligui alikuwa kiongozi wa Kikosi Maalum cha Ulinzi wa Rais (GSPR). Pia alihudumu kama balozi mdogo wa kijeshi katika ubalozi wa Gabon jijini Washington, D.C., nafasi iliyommweka katikati ya masuala ya usalama wa taifa na diplomasia ya kijeshi.[2]

Mnamo 2019, aliteuliwa kuongoza kikosi cha Republican Guard, kikosi maalum kinachohusika na ulinzi wa rais na taasisi muhimu za serikali, akimrithi Jenerali Grégoire Kouna. Katika kipindi chake, alianzisha kampeni kali ya kukabiliana na ufisadi ndani ya jeshi na serikalini, kwa kufuatilia mali zisizoelezeka za maafisa wa serikali na kuhakikisha nidhamu ndani ya vikosi.[3]

Uwezo wake wa kiuongozi, umahiri wa kiintelijensia ya kijeshi na ushawishi mkubwa ndani ya vikosi vilimfanya kuwa kiongozi tegemezi katika operesheni za kijeshi, ikiwemo mafunzo ya kisasa kwa wanajeshi ambao waliongoza moja kwa moja mapinduzi ya mwaka 2023.

Mapinduzi ya kijeshi ya 2023

Mnamo Agosti 30, 2023, Oligui aliongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Ali Bongo, saa chache baada ya tangazo la ushindi wa Bongo katika uchaguzi uliolalamikiwa kwa wizi wa kura.[4] Mapinduzi hayo yalifanikisha kuondoa familia ya Bongo kutoka madarakani baada ya zaidi ya miaka 50 ya utawala.[5]

Urais

Baada ya kipindi cha mpito kilichoongozwa nayeye kama kiongozi wa kijeshi, Gabon ilifanya uchaguzi wake wa kwanza mnamo Aprili 12, 2025 ambapo Oligui alishinda kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura.[6]

Alianza rasmi kazi kama Rais wa Gabon mnamo 3 Mei 2025. Katika utawala wake, Oligui alianzisha chama cha siasa kiitwacho Union Démocratique des Bâtisseurs (UDB) na kuongoza mchakato wa kuandika katiba mpya iliyopitishwa Novemba 2024.[7]

Tazama pia

Marejeo

  1. "Gabon swears in former military chief as president, signalling return to constitutional order". AP News (kwa Kiingereza). 2025-05-03. Iliwekwa mnamo 2025-07-21.
  2. "Brice Oligui Nguema: Gabon's new leader promising a fresh start". BBC News (kwa Kiingereza). 30 Agosti 2023.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. "Who is Brice Oligui Nguema, the general named as Gabon's transition leader?", Reuters (kwa Kiingereza), 2023-08-31, iliwekwa mnamo 2025-07-21
  4. Gabon coup: Army seizes power from Ali Bongo and puts him in house arrest (kwa Kiingereza (Uingereza)), 2023-08-30, iliwekwa mnamo 2025-07-21
  5. Gabon coup: Army seizes power from Ali Bongo and puts him in house arrest (kwa Kiingereza (Uingereza)), 2023-08-30, iliwekwa mnamo 2025-07-21
  6. Obangome, Gerauds Wilfried; Dione, Ngouda (2025-04-13), "Gabon's leader Nguema elected president with 90.35% of vote, interior minister says", Reuters (kwa Kiingereza), iliwekwa mnamo 2025-07-21
  7. Au Gabon, le général Brice Oligui Nguema se taille une Constitution sur mesure (kwa Kifaransa), 2024-10-25, iliwekwa mnamo 2025-07-21