Nenda kwa yaliyomo

Bernardo wa Clairvaux

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Bernard of Clairvaux)
Picha ya zamani ya Bernardo wa Clairvaux
Picha ya zamani ya Bernardo wa Clairvaux
Filippino Lippi, Bikira Maria kumtokea Mt. Bernardo wa Clairvaux

Bernardo wa Clairvaux (Fontaine-lès-Dijon, Ufaransa, 1090 - Ville-sous-la-Ferté, Ufaransa, 20 Agosti 1153) alikuwa padri, abati na mwenezaji mkuu wa urekebisho wa Citeaux wa shirika la Benedikto wa Nursia.

Aliongoza kwa hekima wamonaki wenzake katika njia za amri za Mungu kwa maisha, mafundisho na mifano yake mwenyewe. Lakini pia alisafiri kote Ulaya ili kurudisha amani na umoja akaangaza Kanisa lote kwa maandishi na mahubiri yake motomoto[1].

Aliitwa “Babu wa mwisho” kwa sababu alitetea na kustawisha teolojia ya mababu wa Kanisa wakati wa kujitokeza teolojia mpya ya shule.

Ndiye mtu muhimu zaidi wa karne ya 12 katika Kanisa Katoliki, ambalo linamheshimu kama mtakatifu (alivyotangazwa na Papa Alexander III mwaka 1174) na mwalimu wa Kanisa (alivyotangazwa na Papa Pius VIII mwaka 1830).

Ni msimamizi wa wakulima.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 20 Agosti[2].

Nyumba alimozaliwa Bernardo
Bernardo akihimiza kwenda vitani

Bernardo alizaliwa huko Fontaine-lès-Dijon, leo nchini Ufaransa, mwaka 1090. Alikuwa mtoto wa tatu kati ya saba waliozaliwa na Teshelino na Aleta, wote wa koo bora za watawala wadogo wa ufalme wa Borgogne (leo nchini Ufaransa).

Alisoma hasa lugha na hoja kwa Wakanoni wa kanisa la Nôtre Dame de Saint-Vorles, karibu na Châtillon-sur-Seine.

Kisha kurudi katika ngome ya baba yake huko Fontaines, mwaka 1111 alitawa pamoja na ndugu zake 5 na jamaa na marafiki kadhaa katika nyumba ya Châtillon, mpaka mwaka uliofuata akajiunga pamoja na wenzake 30 na monasteri ya Cîteaux (karibu na Dijon), iliyoanzishwa miaka 15 ya nyuma na Roberto wa Molesmes. Wakati huo ilikuwa chini ya Stefano Harding, abati wa tatu.

Urekebisho huo ulishika kwa bidii sana mashauri ya Kiinjili, hasa ufukara, bila kulemewa na mapokeo mengi ya ziada yaliyofuatwa katika monasteri ya kawaida.

Mwaka 1115, alipokuwa na miaka 25 tu, Stefano Harding alimtuma kuanzisha monasteri mpya, hivyo alihamia pamoja na wamonaki wenzake 12 katika mkoa wa Champagne, walipozawadiwa shamba kubwa karibu na mto Aube, wakaliita Clairvaux, yaani bonde angavu.

Akiwa hivyo na nafasi ya kutekeleza umonaki alivyouona yeye, alifaulu kuunganisha sala na masomo na utendaji mkubwa. Akiangalia hali ya monasteri nyingi, alisisitiza haja ya kuishi kwa kiasi katika chakula, mavazi na majengo na ya kushughulikia mafukara.

Kwa muda mfupi Abasia ya Clairvaux ikawa kivutio kikubwa kwa miito ya utawa hata ikaweza kuanzia mwaka 1118 kutuma wamonaki wake kuanzisha sehemu nyingine kama vile huko Trois-Fontaines, Fontenay, Foigny, Autun, Laon. Bernardo alipokufa abasia za urekebisho wa Citeaux zilikuwa 343, ambazo 66 kati yake zilianzishwa au kurekebishwa naye, kutoka Hispania hadi Siria, kutoka Italia visiwani hadi Uswedi. Mbali ya kuwa mahali pa kuishi kidini, zilikuwa pia vyuo vya kilimo na ufundi.

Kipindi kilichotangulia mwaka 1130 Bernardo aliandikiana sana na watu wa kila aina. Mbali ya barua hizo nyingi, alitoa hotuba nyingi na vitabu mbalimbali.

Tangu mwaka 1130 alianza kushughulikia masuala mengi mazito ya Kanisa na ya Upapa. Kwa ajili hiyo ilimbidi aondoke utawani mara nyingi zaidi na zaidi hata kusafiri pengine nje ya Ufaransa, pia kwa kuanzisha monasteri za wanawake.

Maisha yake yote Bernardo akawa mtetezi shujaa wa imani sahihi na wa mamlaka ya Kanisa.

Katika maandishi yake ya kupinga uzushi, alimlenga hasa Abelardo, msomi mahiri aliyebuni namna mpya ya kufanya teolojia akitumia zaidi mantiki na hoja za falsafa. Kisha kupata hukumu ya Sinodi ya Sens ya mwaka 1140 dhidi ya baadhi ya mafundisho ya Abelardo, hatimaye alifaulu kupatana naye kwa msaada wa Petro Mhashamu wa Cluny.

Zaidi tena alipinga Wakatari, waliodharau ulimwengu wa maada pamoja na mwili wa binadamu, na hivyo walimkosea shukrani Muumba wa vyote.

Kinyume chake aliwajibika kutetea Wayahudi dhidi ya mashambulizi yaliyowapata mara nyingi zaidi na zaidi.

Miaka hiyohiyo Bernardo aliandika vitabu vyake maarufu zaidi, kama vile Hotuba juu ya Wimbo Ulio Bora.

Alipatanisha Wakristo (na watawala wao) waliokuwa wanagombana. Vita vya msalaba vya mwaka 1147 vilifanikiwa kuungwa mkono na watu wa Ufaransa na Ujerumani kutokana na mahubiri yake.

Miaka ya mwisho alilazimika kupunguza safari zake, hivyo alipata nafasi zaidi kwa maandishi yake, akiyapitia upya na kuyaongeza.

Kitabu cha pekee cha mwaka 1145 ambacho kinaitwa “Kuzingatia” alikiandika kwa ajili ya mwanafunzi wake Bernardo Pignatelli ili kumuongoza katika majukumu yake mapya alipochaguliwa kuwa Papa kwa jina la Eugene III. Humo unajitokeza pia mtazamo wa dhati juu ya fumbo la Kanisa ambao kupitia fumbo la Kristo unaishia kuzama katika fumbo la Utatu.

Mwishoni mwa mwaka 1152 alikuwa ameishiwa nguvu, lakini alisafiri hadi Metz ili kutuliza fujo za mji huo.

Alipokuwa akirudi Clairvaux, akariki Ville-sous-la-Ferté, tarehe 20 Agosti 1153.

Njia ya sala ya Bernardo

[hariri | hariri chanzo]

Bernardo hakuelekea ujuzi unaotokana na mantiki, bali ule unaopatikana kwa kuzama katika mafumbo kwa sala ya kumiminiwa. Kwake ndiyo njia pekee ya kumfahamu kweli Mungu na kufikia amani na heri ya kuwa naye.

Hivyo, akipinga teolojia ya shule iliyokuwa inaanzaanza, alishikilia mapokeo ya Biblia, ya mababu wa Kanisa, ya liturujia na ya umonaki, pia kwa lengo la kulinda imani sahili ya waamini wa kawaida.

Kwake upendo mkubwa zaidi na zaidi ndio lengo pekee la teolojia, alivyoeleza katika kitabu “Kumpenda Mungu”. Safari hiyo ya roho ina hatua mbalimbali ambazo alizifafanua kinaganaga na ambazo zinakamilika katika ulevi wa upendo usiosemeka.

Tangu hapa duniani mtu anaweza kufikia muungano huo na Neno wa Mungu ambao Bernardo aliuita “arusi ya kiroho”. Hapo Neno anaitembelea roho, anakomesha ndani yake dalili za mwisho za ukaidi, anaiangaza, anaiwasha na kuigeuza.

Fikra zetu kuhusu mafumbo ya Mungu ziko katika hatari ya kugeuka zoezi la bure la akili zisipotegemea imani ya dhati iliyolishwa na sala hasa katika uhusiano wa dhati na Bwana: ndiyo “ujuzi wa watakatifu” ambao unatolewa na Roho Mtakatifu na kuhitajiwa na teolojia.

“Ni lazima tuendelee kumtafuta Mungu huyo, asiyetafutwa bado vya kutosha, lakini inaweza kuwa rahisi zaidi kumtafuta na kumpata katika sala kuliko katika mijadala”. Mtume Yohane, aliyeegama kichwa chake kifuani pa Yesu, anabaki kielelezo cha mwanateolojia na cha mwinjilishaji bora.

Mbele ya hoja kali zilizozidi kutolewa katika mihadara ya shule, Bernardo alisisitiza kwamba Yesu tu ni “asali kinywani, wimbo sikioni, shangilio moyoni… Lishe yote ya roho ni kavu isipolainishwa na mafuta hayo; haina ladha isipotiwa chumvi hiyo. Unachoandika hakininogei nisiposoma Yesu ndani yake”.

Ndiyo sababu mapokeo yamemuita “Doctor Mellifluus”, yaani “Mwalimu mtamu kama asali”, kwa jinsi masifu yake kwa Kristo yalivyobubujika kwa utamu.

Pamoja naye alimmiminia sifa Bikira Maria, kiasi kwamba miaka 150 hivi baada ya kifo chake, Dante Alighieri alimtia mdomoni maneno haya: “Bikira Mama, binti wa Mwanao, mnyenyekevu na mkuu kuliko viumbe, shabaha maalumu ya mpango wa milele”.

Bernardo hakuwa na shaka: ni kwa njia ya Maria kwamba tunamuendea Yesu (kwa Kilatini, “Per Mariam ad Iesum”). Ndiyo sababu alihimiza, “Katika hatari, katika huzuni, katika shaka, umfikirie Maria, umuitie Maria. Yeye asiache kamwe midomo yako, asibandukane kamwe na moyo wako; na ili uweze kupata msaada wa sala zake, usisahau kamwe mfano wa maisha yake. Ukimfuata, huwezi kusita; ukimuomba, huwezi kukata tamaa; ukimfikiria, huwezui kukosea. Akikutegemeza, hutajikwaa; akikulinda, huna la kuogopa; akikuongoza, hutaanguka kamwe; akiwa upande wako, utafikia lengo lako”.

Kulingana na mapokeo, Bernardo alishuhudia kwamba Maria yuko chini ya Kristo, lakini pia alisisitiza nafasi ya pekee aliyonayo katika mpango wa wokovu, kutokana na jinsi alivyoshiriki kikamilifu sadaka ya Mwanae.

Alimuambia hivi wakati wa kuhubiri, “Mama mwenye heri, kweli upanga ulichoma roho yako!… Ukali wa uchungu ulichoma roho yako kwa ndani hivi kwamba ni haki tukuite mfiadini, kwa sababu ndani mwako ushiriki wa mateso ya Mwanao unazidi kabisa kwa ukali mateso ya kimwili ya kufia dini”.

Katika vitabu vingi, hasa vya ufafanuzi wa Biblia, alivyoviandika, unajitokeza upendo hai uliomuongoza daima kama alivyoandika, “Upendo ndio nguvu kuu ya maisha ya kiroho”.

Sala yake

[hariri | hariri chanzo]

Bwana, mema yangu ni kukaa katika tabu, mradi wewe uwe nami.

Ni bora kuliko kutawala pasipo wewe, kula karamuni pasipo wewe, kujitukuza pasipo wewe.

Bwana, mema yangu ni kukukumbatia wewe katika tabu, kuwa nawe katika tanuri, kuliko kubaki pasipo wewe, hata kama ingekuwa mbinguni.

Kwangu kuna nini zaidi mbinguni, nami natamani nini zaidi ya wewe duniani?

Moto unatakasa dhahabu na jaribio la tabu linatakasa waadilifu.

Humo, Bwana, u pamoja nao; humo unakaa kati ya wale waliokusanyika kwa jina lako, kama zamani na vijana watatu.

Maandishi

[hariri | hariri chanzo]
Meditatio super Salve Regina, 1495
  • De consideratione libri quinque ad Eugenium III
  • De diligendo Deo
  • De gradibus humilitatis et superbiae
  • De Gratia et libero arbitrio
  • De laude novae militiae ad Milites Templi
  • De laudibus Virginis Matris
  • Contemplatio Passionis
  • Expositio in Canticum Canticorum
  • Meditatio super fletus Virginis
  • Sermones
  • Sermones de tempore
  • Sermones super Cantica Canticorum
  • Epistola ad Raymundum dominum Castri Ambuosii
  • Sermo de miseria humana
  • Tractatus de interiori domo seu de conscientia aedificanda
  • Varia et brevia documenta pie seu religiose vivendi
  • Visio contemplativa

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]