Bad (ziara)

Ziara ya Bad ilikuwa ziara ya kwanza ya tamasha la peke yake la mwimbaji wa Marekani Michael Jackson. Tamasha lilizinduliwa ili kusaidia kusukuma maumzo ya albamu yake ya saba ya Bad (1987). Ziara hiyo ya dunia iliyokuwa na maonyesho 123 ilianza Septemba 12, 1987 nchini Japani, na kuhitimishwa Januari 27, 1989 nchini Marekani. Ziara ilidhaminiwa na mtengenezaji wa vinywaji baridi Pepsi. Iliingiza jumla ya dola za Kimarekani milioni 125, na kuifanya kuwa ziara ya pili kwa mapato makubwa zaidi katika miaka ya 1980 baada ya ziara ya Pink Floyd ya Momentary Lapse of Reason, na kupata rekodi mbili mpya katika Guinness World Records kwa kuwa ziara iliyoingiza mapato makubwa zaidi katika historia na ziara iliyohudhuriwa na hadhira kubwa zaidi. Iliteuliwa kuwania tuzo ya "Tour of the Year 1988" katika tuzo za kwanza za International Rock Awards.[1]
Mwishoni mwa ziara hiyo, Jackson alitoa taarifa hadharani kwamba alikusudia iwe ya mwisho kama msanii anayefanya ziara, kwani alikuwa na mipango ya kujiingiza kwenye utengenezaji wa filamu;[2] hata hivyo, ilifuatiwa na ziara ya Dangerous World Tour mwaka 1992–1993 na ziara ya HIStory World Tour mwaka 1996–1997. Isipokuwa kwa maonyesho mawili kule Hawaii wakati wa ziara ya HIStory Tour, hii ingekuwa mara pekee ambayo Jackson angefanya ziara nchini Marekani kama msanii kujitegemea.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Mnamo Juni 29, 1987, meneja wa Jackson, Frank DiLeo, alifanya mkutano na waandishi wa habari mjini Tokyo kutangaza kwamba Jackson angeanza ziara yake ya kwanza ya tamasha kama msanii wa kujitegemea. Iliashiria matamasha yake ya kwanza tangu ziara ya Victory Tour mwaka 1984 ambayo alitumbuiza na kaka zake kama akina Jackson 5. DiLeo alisema ziara hiyo ingeanza na mzunguko wa Japani kwa sababu ya mashabiki vindakindaki wanaopatikana katika nchi hiyo.[3] Katika taarifa ya maandishi, Jackson, ambaye alikuwa akimalizia albamu ya Bad huko Los Angeles, aliahidi matamasha yenye "kusisimua na kufurahisha".[4] Mtengenezaji wa vinywaji baridi Pepsi, ambaye Jackson na kaka zake walikuwa na mkataba naye wenye thamani inayokadiriwa kuwa dola milioni 5 kwa mwaka, alidhamini ziara hiyo. Mauzo ya kinywaji hicho nchini Japani yaliongezeka mara mbili wakati wa msimu wa joto kufuatia tangazo hilo, yakisaidiwa na kampeni ya matangazo iliyotoa tiketi za bure na zawadi 30,000.[5] Msafara mzima ulielekezwa kutoonekana wakinywa bidhaa kutoka kwa mpinzani Coca-Cola hadharani. Mtoto wa Marlon Brando, Miko, alijiunga na ziara hiyo kama msaidizi wa utayarishaji.[6]
Majaribio ya bendi ya kusindikiza ya Jackson, na mazoezi yaliyofuata, yalifanyika katika kituo cha Leeds kule North Hollywood. Mpiga kinanda Rory Kaplan, ambaye alikuwa amepiga kwenye ziara ya Victory Tour, alikuwa kwenye ziara na Chick Corea Elektric Band alipoombwa na katibu wa Jackson kujiunga na kundi lake kama msimamizi wa muziki, ombi ambalo Kaplan alilikubali.[7] Jackson alikusudia kuwajumuisha wanamuziki wengine wawili ambao walikuwa sehemu ya bendi ya Victory Tour, mpiga ngoma Jonathan Moffett na mpiga gitaa David Williams. Hata hivyo, wote wawili walikuwa kwenye ziara na Madonna wakati huo na hivyo hawakupatikana. Jackson alitaka muziki jukwaani uwe na sauti kama rekodi za asili, na akamuomba Chris Currell, ambaye alikuwa amepiga kinanda cha vionjo cha Synclavier kwenye albamu ya Bad, akipige mubashara. Currell alifanya mipango ya kuwa na mifumo mitatu kamili: miwili ya kushughulikia muziki jukwaani na mmoja kwa ajili ya chumba chake cha hoteli ili Jackson arekodi mawazo wakati akisafiri, pamoja na seti iliyofunguliwa kwa ajili ya vipuri ikiwa kuna tatizo, na mtaalamu wa muda wote. Currell alikadiria Synclaviers pekee ziligharimu dola milioni 1.4. Kwa kuwa yeye kimsingi alikuwa mpiga gitaa na si mpiga kinanda, alinunua gitaa la kudhibiti la SynthAxe MIDI ili kuchochea ishara kwenye kompyuta iliyoendesha Synclavier. Maonyesho ya majaribio yalirekodiwa na kuonyeshwa kwa Jackson nyumbani kwake jioni. Bendi ilikuwa na wiki mbili tu za kufanya mazoezi kule Leeds kabla ya mazoezi ya utengenezaji wa maelekezo maalumu katika Universal Studios kwa wiki nyingine tatu, ingawa hakuna utengenezaji kamili kwa ukamilifu wake uliofanyika hadi onyesho la kwanza.[7]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Halstead, Craig; Cadman, Chris (Julai 2003). Michael Jackson The Solo Years. England: New Generation Publishing. uk. 85. ISBN 978-0755200917.
{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Why Michael Jackson Stopped Performing at His Peak? | the detail". YouTube. Januari 20, 2022.
{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Jackson set for his first solo world tour". Desert Dispatch. Juni 30, 1987. uk. 9. Iliwekwa mnamo Februari 10, 2023 – kutoka Newspapers.com.
{{cite news}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Michael Jackson sets new concert tour dates". The Daily Advertiser. Julai 5, 1987. uk. 28. Iliwekwa mnamo Februari 12, 2023 – kutoka Newspapers.com.
{{cite news}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Jones, Terril (Septemba 20, 1987). "Jackson tour gives boost to Pepsi sales in Japan". Daily Record. uk. D14. Iliwekwa mnamo Februari 10, 2023 – kutoka Newspapers.com.
{{cite news}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Kaplan, Lisa Faye (Julai 9, 1987). "Brando's son is behind the 'Bad' concerts". Mount Vernon Argus. uk. C1. Iliwekwa mnamo Februari 12, 2023 – kutoka Newspapers.com.
{{cite news}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - 1 2 Darter, Sibyl (Machi 1989). "Rory Kaplan" (PDF). After Touch. Juz. 5, na. 3. ku. 10–11. Iliwekwa mnamo Februari 18, 2023.
{{cite magazine}}: CS1 maint: date auto-translated (link)