Australia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 19:05, 19 Oktoba 2015 na Moeng (majadiliano | michango) (update)
Australia


Australia ni bara pia ni nchi. Ni bara dogo kuliko yote duniani, na ni kisiwa kikubwa kuliko vyote.

Iko kusini kwa Indonesia na magharibi kwa New Zealand. Ikiwa na eneo la 7.682.300 km² ni bara dogo kabisa duniani, kama nchi ni ya sita kwa ukubwa. Mara nyingi visiwa vya New Zealand huhesabiwa kuwa sehemu ya bara la Australia. Vilevile Australia huangaliwa pamoja na visiwa vya Pasifiki katika orodha ya mabara ya dunia kama "Australia na Pasifiki".

Idadi ya wakazi ni 23,648,300 (mwaka 2014).

Jiografia

Hali ya hewa Australia kufuatana na Köppen classification.

Bara la Australia linakaa juu ya bamba la Australia likiwa na eneo la 7,617,930 km². Umbali kati ya magharibi na mashariki ni km. 4,000, na kati ya kaskazini na kusini umbali ni km. 3,700.

Kwa jumla ina pwani yenye urefu wa kilomita 34,218.

Australia huzungukwa na bahari ya Hindi, bahari ya Pasifiki na Bahari ya Kusini.

Bara linakaa kwenye sehemu imara ya bamba la Australia bila mipaka ya gandunia na kwa hiyo hakuna volkeno; matetemeko ya ardhi ni madogo tu.

Great Barrier Reef mbele ya pwani ya mashariki-kaskazini ni vipwa vya matumbawe vikubwa duniani; ina urefu wa kilomita 2,000.

Sehemu kubwa ya bara ni jangwa au maeneo yabisi sana. Takriban asilimia 40 ya eneo limefunikwa na matuta ya mchanga. Ardhi yenye rutuba iko kusini-mashariki na kona ya kusini-magharibi pamoja na hali ya hewa isiyo na joto kali. Hali ya hewa kaskazini ni ya kitropiki na hapa kuna misitu minene pamoja na savana na jangwa.

Sehemu kubwa ya uso wa nchi ni tambarare na majangwa. Kwenye pwani ya mashariki na pia upande wa magharibi kuna safu za milima inayopanda hadi kimo cha mita 2,200. Sehemu ya juu kabisa huitwa milima ya theluji au Alpi za Australia na mlima wa Kosciuszko unafikia kimo cha mita 2,229. Huko kuna barafuto za kudumu.

Sehemu ya duni iko kwenye beseni la ziwa Eyre iliyopo mita 17 chini ya usawa wa bahari. Tako la beseni hili mara nyingi ni kavu kabisa, panajaa mara chache tu baada ya mvua kubwa sana.

Mahali pakavu kabisa ni jangwa la Simpson lenye usimbishaji chini ya 200 mm kwa mwaka.

Sehemu kubwa ya bara haina watu. Wakazi wengi pamoja na miji yote wako kwenye pwani ya mashariki na kusini.

Uchumi katika maeneo yabisi ni hasa ufugaji wa kondoo milioni 130 na ng'ombe milioni 25.

Miji mikubwa ni Sydney (wakazi milioni 3.7), Melbourne (wakazi milioni 3.6), Brisbane (wakazi milioni 1.7), Perth (wakazi milioni 1.4) na Adelaide (wakazi milioni 1.1).

Mji mkuu, Canberra (wakazi milioni 308,700) ulijengwa kati ya Sydney na Melbourne kwa sababu miji hiyo miwili ilishindwa kukubaliana kati yao ni mji upi unaostahili kuwa mji mkuu.

Mito muhimu inaanza katika Alpi za Australia: ni Murray na Darling inayomwagilia beseni la Murray-Darling na hii ni eneo muhimu la kilimo cha Australia.

Mingine ni Mto Snowy na Mto Murrumbidgee, halafu mto Fitzroy (Queensland), mto Ord, mto Swan (Australia ya Magharibi), mto Derwent, mto Tamar (Tasmania) na mto Hawkesbury (New South Wales).

Ekolojia

Australia ilitengana na mabara mengine miaka milioni mingi iliyopita. Kwa sababu hiyo kuna aina nyingi za pekee za mimea na wanyama zisizopatikana penginepo duniani. Wanyama wa pekee ni kwa mfano kanguru na koala. Miti ya Australia kama vile mkalitusi imepelekwa kote duniani katika nchi zenye hali ya hewa ya kufaa.

Historia

Watu wa kwanza walifika Australia takriban miaka 50,000 iliyopita. Walitunza utamaduni wa wavindaji-wakusanyaji hadi kufika kwa ukoloni.

Hakuna habari kama watu wa Asia walifikia Australia lakini tangu karne ya 17 BK Waholanzi halafu Waingereza walifika kwa jahazi zao.

Australia ikawa mahali pa koloni la kigereza na wafungwa kutoka Uingereza walipelekwa hapa katika karne ya 19. Baadaye walifika pia walowezi huru.

Idadi ya Waustralia asilia imepungua sana kutokana na magonjwa mapya wakiambukizwa na Wazungu, pia walitendewa vibaya na kufukuzwa katika sehemu kubwa ya nchi yao.

Australia ilipata uhuru wake mwaka 1901 lakini inaendelea kumkubali malkia ya Uingereza kama Mkuu wa Dola akiwasilishwa na Gavana Mkuu. Mamlaka imo mikononi mwa waziri mkuu na serikali yake.

Serikali

Muundo wa utawala ni ya shirikisho. Kuna majimbo 6 ya kujitawala pamoja na maeneo ambayo yako moja kwa moja chini ya serikali ya shirikisho.

Lugha

Australia haina lugha rasmi, lakini 81% ya wakazi wanaongea Kiingereza cha Kiaustralia.

Dini

Katika sensa ya mwaka 2011, Wakristo walikuwa 61.1% ya wakazi wote, wakiongozwa na Wakatoliki (25.3%) na Waanglikana (17.1). 22.3% walisema hawana dini yoyote, na 9.4% hawakujibu swali la namna hiyo.

Tanbihi

Marejeo

Marejeo mengine

  • Denoon, Donald, et al. (2000). A History of Australia, New Zealand, and the Pacific. Oxford: Blackwell. ISBN 0-631-17962-3
  • Goad, Philip and Julie Willis (eds) (2011). The Encyclopedia of Australian Architecture Cambridge University Press, Port Melbourne, Victoria. ISBN 978-0-521-88857-8
  • Hughes, Robert (1986). The Fatal Shore: The Epic of Australia's Founding. Knopf. ISBN 0-394-50668-5.
  • Powell JM (1988). An Historical Geography of Modern Australia: The Restive Fringe. Cambridge, U.K.: Cambridge University Press. ISBN 0-521-25619-4
  • Robinson GM, Loughran RJ, and Tranter PJ (2000) Australia and New Zealand: economy, society and environment. London: Arnold; NY: OUP; 0340720336 paper 0-340720328 hard.

Viungo vya nje


Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.