Nenda kwa yaliyomo

Antoine de Saint-Exupery

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Antoine de Saint-Exupéry kwenye mwaka 1942

Antoine de Saint-Exupery (* 29 Juni 1900 mjini Lyon; † 31 Julai 1944) alikuwa rubani, mwandishi na mshairi kutoka nchini Ufaransa.

Miaka ya kwanza

[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa katika familia tajiri ya Ufaransa ya kusini. Alipokuwa na umri wa miaka 12 alipata mara ya kwanza nafasi ya kuwa abiria katika ndege ndogo iliyoruka. Baada ya kutumia miaka kadhaa kusoma ubunifu na kutimiza utumishi wa kijeshi wa kisheria alichukua cheti cha rubani akaajiriwa na makampuni ya usafiri wa hewani na kuongoza ndege za mizigo na abiria.

Rubani na mwandishi

[hariri | hariri chanzo]

Pamoja na kuruka alianza pia kuandika hadithi na masimulizi. Sehemu ya miaka yake ya urubani alifanya katika makoloni ya Ufaransa barani Afrika alipokaa miaka kadhaa kwenye vituo vya jangwani. Wakati ule alitunga riwaya yake ya kwanza "Tarishi wa kusini" (Courier de Sud) inayosimulia safari ya mwisho wa rubani fulani pamoja na hadithi ya mapenzi yake yasiyofikia shabaha.

Mwaka 1929 alitumwa Argentina kuanzisha huduma ya utarishi wa usiku ambako marubani walisafirisha barua, magazeti na mizigo ya haraka wakati wa usiku. Hatari na maarifa ya miaka ile alitumia katika riwaya ya "Kuruka kwa usiku" (Vol de nuit, 1930) aliyopata tuzo muhimu na kumfanya kuwa mwandishi mashuhuri.

Saint-Exupery mwaka 1935 baada ya kuanguka na ndege yake katika jangwa la Misri.

Katika miaka iliyofuata alichanganya kazi mbalimbali kama rubani, mwanahabari kwa magazeti mashuhuri, mwandishi na mtangazaji wa bidhaa kwa ajili ya makampuni kadhaa. Mwaka 1938 alianguka kwa ndege yake nchini Guatemala akajeruhiwa. Katika miezi ya matibabu na kupona alitunga kitabu "Dunia ya binadamu" (Terres des Hommes) alipokusanya matini mbalimbali na mkusanyiko huu ulikuwa na ufanisi mkubwa: alipata tuzo ya "Grand Prix du Roman de l’Académie française" na kuuzwa mara nyingi.

Miaka ya vita na Mwana Mdogo wa Mfalme

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia alitoka katika Ufaransa iliyovamiwa na Ujerumani akakaa kwa muda Marekani. Hapo alitunga simulizi lililokuwa ufanisi wake mkuu "Mwana Mdogo wa Mfalme" (Le Petit Prince). Kwa namna ya hekaya ni hadithi ya rubani anayepaswa kufanya kituo cha dharura jangwani anapokutana na mvulana mdogo (mwana mdogo wa mfalme) kutoka asteroidi kwenye anga-nje. Hekaya hii imetafsiriwa kwa lugha zaidi ya 140 na ni kati ya vitabu vilivyotolewa mara nyingi zaidi duniani.

Mwisho wake

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kukimaliza kijitabu hiki alirudi Ulaya alipojiunga na jeshi la Ufaransa Huru lililopigana na Ujerumani likiwa pamoja na Wamarekani walioingia Ulaya Kusini kutoka Afrika ya Kaskazini.

Kikuku cha Saint-Exupery iliyopatikana mwaka 1988.

Mwaka 1944 aliruka juu ya mji wa Marseille kwa kusudi la upelelezi kutoka anga na kutoka safari hii hakurudi. Baadaye imejulikana ya kwamba ndege yake ilipigwa na kuangushwa na ndege ya Kijerumani.

Mwaka 1988 mvuvi Mfaransa alikuta kikuku chenye jina lake wakati wa kusafisha nyavu. Baadaye pia injini ya ndege yake ilipatikana majini karibu na ufuko.

Mwaka 1975 asteroidi 2578 ilipewa jina la Saint-Exupéry na tangu mwaka 2000 Kiwanja cha Ndege cha Lyon kinaitwa kwa jina lake.

Vitabu vyake kwa Kiswahili

[hariri | hariri chanzo]

Vitabu vyake kwa Kiingereza

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Antoine de Saint-Exupery kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.