Anna Elisha Mghwira

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Anna Elisha Mghwira (23 Januari 1959 - 22 Julai 2021[1]) alikuwa mwanasiasa wa Tanzania. Aliwahi kuwa mwenyekiti wa Alliance for Change and Transparency (ACT) aliyegombea urais wa nchi katika uchaguzi mkuu mnamo mwaka 2015.

Baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, alihamia chama cha CCM mnamo mwaka 2017.

Maisha ya awali na elimu[hariri | hariri chanzo]

Anna Elisha Mghwira alizaliwa tarehe 23 Januari 1959 katika Hospitali ya Mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji - Kitongoji cha Irao katika Manispaa ya Singida-Mjini. Miaka yake ya mapema alikuwa mtoto wa nyumbani kwa sababu ya matatizo ya kiafya yaliyomchelewesha kutembea. [2] Alijiunga na shule ya msingi ya Nyerere katika miaka ya 1968- 1974. Kisha akasoma shule ya Sekondari Ihanja kutoka 1975 hadi 1978 kabla ya kujiunga na Seminari ya Kilutheri kwa masomo ya A-level 1979 hadi 1981. Alipata shahada yake ya kwanza katika theolojia kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipoongeza shahada ya sheria (LLB) mnamo 1986. Kwenye Chuo Kikuu cha Essex huko Uingereza aliendelea kusoma shahada ya uzamili ya sheria (LLM) mnamo mwaka 2000.

Mghwira alifanya kazi kwa mashirika ya kimataifa na ya Kitanzania yanayoshughulikia uwezeshaji wanawake, maendeleo ya jamii na wakimbizi. [3]

Maisha ya siasa[hariri | hariri chanzo]

Baba yake alikuwa diwani kupitia TANU. [4]

Anna alijiunga na umoja wa vijana wa chama hicho. mnamo mwaka 1970 alipunguza kazi yake ya kisiasa ili aweze kuzingatia masomo yake na familia.

Mnamo mwaka 2009 alirudi katika siasa na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA. Bi Mghwira alishikilia nyadhifa tofauti kama katibu wa wilaya wa chama na baadaye mwenyekiti wa wilaya wa chama.

Mnamo mwaka 2012, alishindwa na Joshua Nassari katika uteuzi wa Chadema kwa uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki. Alifanikiwa kugombea kiti cha Bunge la Afrika Mashariki mwaka huo huo, bila kuchaguliwa.

Mnamo Machi 2015, alihama Chadema kwenda chama kipya cha ACT-Wazalendo, ambapo baadaye aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kitaifa wa chama wakati wa mkutano mkuu wa kwanza wa chama. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka ule aligombea urais wa Tanzania.

Mwaka 2017 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro akaacha ACT-Wazalendo akahamia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Former Kilimanjaro RC Anna Mghwira dead at 62. Jalada kutoka ya awali juu ya 2021-07-23. Iliwekwa mnamo 2021-07-23.
  2. "Female Candidate Stories – Anna Elisha Mghwira". Retrieved on 2021-01-01. Archived from the original on 2016-12-20. 
  3. "Profile - Anna Mghwira, ACT-Wazalendo". Retrieved on 2021-01-01. Archived from the original on 2015-10-27. 
  4. "PROFILE: Anna Mghwira". Retrieved on 2021-01-01. Archived from the original on 2017-12-29.