Alexander Kerensky
Alexander Fyodorovich Kerensky (4 Mei 1881 – 11 Juni 1970) alikuwa mwanasiasa, mwanasheria, na kiongozi wa mapinduzi kutoka nchini Urusi. Anajulikana zaidi kwa kuongoza serikali ya mpito ya Urusi na Jamhuri ya Urusi kama waziri mkuu kwa muda wa miezi mitatu, kuanzia mwisho wa mwezi Julai hadi mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka 1917.[1]
Baada ya mapinduzi ya februari ya mwaka 1917 yaliyomwondoa madarakani Mfalme wa Urusi wa kipindi hicho, Nikola II (kwa Kirusi: Nikolay II), Kerensky alijiunga na serikali mpya ya muda iliyoundwa. Kwanza alikuwa Waziri wa Sheria, kisha akawa Waziri wa Vita, na baada ya mwezi Julai akachaguliwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo. Alikuwa pia kiongozi wa kundi la wanasiasa wanaotetea haki za wafanyakazi (Trudoviks) ndani ya Chama cha Kimapinduzi cha Kijamii. Wakati huohuo, alikuwa kiongozi mkuu msaidizi kwenye Baraza la Petrograd(Petrograd Soviet),baraza kuu la wawakilishi wa wafanyakazi na askari, nafasi iliyompa nguvu kubwa ya kimaamuzi. Kipindi chake cha uwaziri mkuu kilijawa na changamoto kubwa kutokana na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Licha ya kwamba wananchi wengi walitaka Urusi ijitoe kwenye vita hivyo, Kerensky alilazimisha Urusi iendelee kupigana. Serikali yake ilianza kuwakamata na kuwakandamiza watu wote waliopinga vita, jambo lililofanya wananchi wamchukie sana.
Kerensky aliongoza nchi hadi yalipotokea mapinduzi ya oktoba mwaka 1917. Katika mapinduzi hayo, kundi la wakomunisti "Mabolshevik" likiongozwa na Vladimir Lenin liliipindua serikali ya Kerensky na kuchukua madaraka. Baada ya kupinduliwa, Kerensky alitoroka Urusi na kwenda kuishi ukimbizini katika miji ya Paris na New York. Akiwa huko, alifanya kazi ya utafiti katika taasisi ya "Hoover",kituo kikubwa cha utafiti wa sera za umma na maktaba ya kihistoria kwenye Chuo Kikuu cha Stanford huko California.[2]
Alifariki dunia mjini New York tarehe 11 Juni 1970, akiwa na umri wa miaka 89. Viongozi wa Makanisa ya Kiorthodoksi ya Urusi na Serbia walikataa kuupokea mwili wake ili kuuzika kidini. Walifanya hivyo kwa sababu alikuwa mwanachama wa kikundi cha siri cha wajenzi huru (Freemason), na pia waliamini yeye ndiye aliyesababisha nchi kuvurugika hadi wakomunisti (Mabolshevik) wakashika nchi.[3] Kutokana na mzozo huo, mwili wake ulisafirishwa kwa ndege hadi jijini London na kuzikwa kwenye Makaburi ya "Putney Vale" nchini Uingereza, ambayo hayakuwa na ubaguzi wa madhehebu ya dini.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]| Makala hii kuhusu wakimbizi au masuala ya ukimbizi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Alexander Kerensky kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |