Aidan Mtakatifu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Aidan Mtakatifu

Aidan wa Lindisfarne (pia huitwa Mtume wa Northumbria) alianzisha kituo cha utawa na kuwa askofu wake wa kwanza kwenye kisiwa cha Lindisfarne kule Uingereza. Alifariki kule Northumbria tarehe 31 Agosti 651.

Anaheshimiwa kama mtakatifu kwa kufufua Ukristo katika eneo la Northumbria. Alikuwa ametokea Ireland, na kabla hajafika Northumbria alikuwa mtawa katika kituo cha utawa kwenye kisiwa cha Iona katika nchi ya Scotland.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa enzi ya Warumi, Ukristo ulikuwa umeenea mpaka Uingereza, lakini kwa sababu ya kushindwa kwa Warumi, upagani ukaanza kurudi upande wa kaskazini wa Uingereza.

Oswald, mfalme wa Northumbria, mwaka 616 alilazimishwa kwenda uhamishoni katika kisiwa cha Iona ambako akabadili kuwa Mkristo na kubatizwa.

Mwaka 634 Oswald alirudishiwa ufalme wa Northumbria akaamua kuwaingiza katika Ukristo wananchi wake ambao wengi wao walikuwa wapagani. Ili kutekeleza lengo hilo aliwaomba watawa wa Iona wamtumie wamisionari, naye Aidan akafika mwaka 635.

Aidan alichagua kisiwa cha Lindisfarne kiwe makao makuu ya dayosisi yake kwa vile kilikuwa karibu na ngome ya kifalme kule Bamburgh.

Mwanzoni alikuwa mfalme Oswald mwenyewe aliyewatafsiria Aidan na watawa wake kwa vile walikuwa hawajajifunza lugha ya kale ya Kiingereza. Baada ya kifo cha Oswald mwaka 642, Aidan alisaidiwa na mfalme Oswine wa Deira, nao wakawa marafiki wa karibu sana.

Aidan alikuwa huwatembelea watu kijiji hadi kijiji, na kuongea nao kwa adabu na kujaribu katika maongezi hayo wavutwe na Ukristo.

Kufuatana na hadithi moja, mfalme alimpa Aidan farasi ili asihitaji kutembea kwa miguu lakini Aidan akatoa farasi kama zawadi kwa mtu maskini.

Aidan aliweza kuongea na watu na hivyo alifaulu kuwasaidia wananchi wengi wa Northumbria wawe Wakristo. Pia katika kituo chake cha utawa aliwafundisha wavulana kumi na wawili, wenyeji wa Northumbria, ili kuhakikisha kwamba kanisa la Uingereza liongozwe na Waingereza wenyewe.

Aidan alifuata tawi la Ireland la Ukristo, si mapokeo ya Kiroma. Hata hivyo tabia yake na bidii katika umisionari zilisababisha Papa Honorius I amheshimu.

Kituo cha utawa cha Lindisfarne kiliendelea kukua na kuanzisha makanisa na vituo vingine. Pia kilikuwa kama hazina ya ujuzi wa kitaalamu.

Baadaye, Beda Mhashamu aliandika wasifu ya maisha yake Aidan pamoja na miujiza yake yote.

Sikukuu yake Aidan Mtakatifu ni tarehe 31 Agosti.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Attwater, Donald and Catherine Rachel John. The Penguin Dictionary of Saints. 3rd edition. New York: Penguin Books, 1993. ISBN 0-14-051312-4.
  • Powicke, F. Maurice and E. B. Fryde Handbook of British Chronology 2nd. ed. London:Royal Historical Society 1961
Commons-logo.svg
Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]