Nenda kwa yaliyomo

Agustín Laje

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Agustín Laje Arrigoni (alizaliwa 16 Januari 1989) ni mwandishi wa kihafidhina kutoka Argentina, mchambuzi wa kisiasa, na mhadhiri. Pia ni mwanzilishi na rais wa kituo cha tafakuri cha kihafidhina kiitwacho Fundación Libre.[1]

Maisha ya awali na elimu

[hariri | hariri chanzo]

Laje alianza masomo yake katika taaluma ya uhandisi wa mifumo katika chuo kikuu cha Instituto Universitario Aeronáutico [es]. Akiwa chuoni, alichapisha kazi yake ya kwanza Los mitos setentistas: Mentiras fundamentales sobre la década del 70.[2] Kitabu hicho kilimpa fursa ya kupata ufadhili wa masomo kuhusu mbinu za kupambana na ugaidi katika kituo cha William J. Perry Center for Hemispheric Defense Studies, kilichopo chuo kikuu cha National Defense University jijini Washington, D.C., taasisi ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani.[3]

Aliporejea Argentina mwaka 2011, aliacha masomo ya uhandisi. [4] Laje ana shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa kutoka Universidad de Córdoba na shahada ya uzamili ya Falsafa kutoka Universidad de Navarra, Uhispania.

Mnamo 2013, Laje alichapisha Cuando el relato es una farsa: la respuesta al relato kirchnerista, akiwa na mwandishi mwenza Nicolás Márquez, ambapo walikosoa mtazamo wa Kirchnerism kuhusu udikteta wa mwisho nchini Argentina. Kitabu hicho kilipingwa vikali na mashirika ya haki za binadamu na yale yanayounga mkono mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, kiasi cha kufanikisha kughairiwa kwa uwasilishaji wake huko Bahía Blanca.[5]

Mnamo 2016, akiwa na Márquez, walichapisha kitabu El libro negro de la nueva izquierda: Ideología de género o subversión cultural. Ndani yake, walikosoa wimbi la tatu la ufeministi na kile wanachokiita "itikadi ya kijinsia", ambayo wanaitazama kama chombo cha Umaksi wa Kitamaduni. Kitabu hicho kilizua utata mkubwa, ikiwa ni pamoja na dai kwamba harakati kali za wanawake zinaunga mkono ukatili dhidi ya watoto. Kutokana na hayo, mwigizaji na mtangazaji Malena Pichot alifanya mahojiano naye kupitia kipindi cha redio, na kusababisha mjadala uliosambaa mitandaoni. Pia, Laje alishiriki mjadala na mtangazaji Patricia del Río kupitia kituo cha redio cha Peru, RPP.

Uwasilishaji wa kitabu hicho katika Maonesho ya 44 ya Vitabu mwaka 2018 ulipingwa na mashirika ya haki za binadamu pamoja na makundi ya kijamii na kisiasa, yaliyosema kuwa waandishi wa kitabu hicho walieneza ujumbe wa chuki, kukanusha ukweli wa kihistoria, na ubaguzi wa kijinsia.[6]

Mitazamo ya kisiasa

[hariri | hariri chanzo]

Laje anajitambulisha kama paleolibertarian, minarchist, na mpinzani wa ufeministi. Ana pinga vikali uavyaji mimba, hata katika visa vya ubakaji, pamoja na euthanasia, na hivyo kujitokeza kama mwanaharakati wa uhai. Mitazamo yake imetajwa na vyombo vya habari vya mrengo wa kushoto kuwa ya kihafidhina na ya mrengo mkali wa kulia.[7] Mara kadhaa, amekuwa akishtumiwa kwa ubaguzi wa kijinsia na chuki dhidi ya mashoga na watu wa jinsia tofauti, ingawa amekanusha madai hayo kwa kusema kuwa hana chuki kwa mtu yeyote.[8]

Kwa mujibu wa Laje, itikadi ya kijinsia ni mkusanyiko wa mawazo yanayopinga sayansi, yanayolenga kupotosha ukweli wa kibaiolojia wa jinsia kwa madhumuni ya kisiasa. Kwa mtazamo wake, tofauti kati ya mwanaume na mwanamke ni hali ya asili, siyo tu muundo wa kijamii.[9]

  1. "Fundación LIBRE – Centro de Estudios Libertad y Responsabilidad". On Think Tanks.
  2. "Presentan el libro "Los mitos setentistas"". lanueva.com. Iliwekwa mnamo 2 Desemba 2023.
  3. "About The Perry Center". William J. Perry Center. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 24 Mei 2021. Iliwekwa mnamo 6 Machi 2025.
  4. "¿Qué esconde el paro de mujeres en México?… 'El feminismo aprovecha astutamente la violencia': Agustín Laje". primeralinea.mx. Iliwekwa mnamo 2 Desemba 2023.
  5. "Suspenden la presentación de un libro por repudio de la comunidad". andaragencia.org. Iliwekwa mnamo 2 Desemba 2023.
  6. "Escrache en la Feria del Libro: un freno a la derecha". ANRed - Agencia de Noticias Redacción.
  7. Ziegler, Gloria. "Ultraconservadores y negacionistas intentan frenar la ampliación de derechos en Argentina". Ojo Público. Iliwekwa mnamo 1 Desemba 2023.
  8. "Protestan en Querétaro contra Agustín Laje por promover homofobia, transfobia y misoginia". Códice Informativo. 22 Juni 2019. Iliwekwa mnamo 1 Desemba 2023.
  9. "Laje: Los defensores de ideología género en RD trataron de aniquilarme". Iliwekwa mnamo 2 Desemba 2023.
Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Agustín Laje kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.