Aidani wa Lindisfarne

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Aidan Mtakatifu)
Mtakatifu Aidani katika dirisha la kioo cha rangi.

Aidani wa Lindisfarne (Ireland, 590 hivi - Northumberland, Uingereza, 31 Agosti 651) ndiye aliyeanzisha kituo cha utawa na kuwa askofu wake wa kwanza kwenye kisiwa cha Lindisfarne.

Kabla hajafika huko alikuwa mtawa katika kwenye kisiwa cha Iona katika nchi ya Uskoti.

Mtu mpole sana, mwenye moyo wa ibada na unyofu katika uongozi, tangu kale anaheshimiwa na Wakatoliki, Waorthodoksi na Waanglikana kama mtakatifu kwa kufufua Ukristo katika eneo hilo lote hata akaitwa Mtume wa Northumberland[1].

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 31 Agosti[2].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa Dola la Roma, Ukristo ulikuwa umeenea mpaka Uingereza, lakini kwa sababu ya kushindwa kwa Warumi, Upagani ukaanza kurudi upande wa kaskazini wa Uingereza.

Oswald, mfalme wa Northumberland, mwaka 616 alilazimishwa kwenda uhamishoni katika kisiwa cha Iona ambako akabadilika kuwa Mkristo na kubatizwa.

Mwaka 634 Oswald alirudishiwa ufalme wake akaamua kuwaingiza katika Ukristo wananchi wake ambao wengi wao walikuwa Wapagani. Ili kutekeleza lengo hilo aliwaomba watawa wa Iona wamtumie wamisionari, naye Aidani akafika mwaka 635.

Aidani alichagua kisiwa cha Lindisfarne kiwe makao makuu ya dayosisi yake kwa vile kilikuwa karibu na ngome ya kifalme kule Bamburgh ili kuinjilisha vizuri zaidi nchi yote.

Mwanzoni alikuwa mfalme Oswald mwenyewe aliyewatafsiria Aidan na watawa wake kwa vile walikuwa hawajajifunza lugha ya Kiingereza cha Kale. Baada ya kifo cha Oswald mwaka 642, Aidani alisaidiwa na mfalme Oswine wa Deira, nao wakawa marafiki wa karibu sana.

Aidani alikuwa huwatembelea watu kijiji hadi kijiji, na kuongea nao kwa adabu na kujaribu katika maongezi hayo wavutwe na Ukristo.

Kufuatana na hadithi moja, mfalme alimpa Aidani farasi ili asihitaji kutembea kwa miguu lakini Aidan akatoa farasi kama zawadi kwa mtu maskini.

Aidani aliweza kuongea na watu na hivyo alifaulu kuwasaidia wananchi wengi wa Northumberland wawe Wakristo. Pia katika kituo chake cha utawa aliwafundisha wavulana kumi na wawili, wenyeji wa Northumberland, ili kuhakikisha kwamba Kanisa la Uingereza liongozwe na Waingereza wenyewe.

Aidani alifuata tawi la Kiselti la Ukristo, si mapokeo ya Kiroma. Hata hivyo tabia yake na bidii katika umisionari zilisababisha Papa Honorius I amheshimu.

Kituo cha utawa cha Lindisfarne kiliendelea kukua na kuanzisha makanisa na vituo vingine. Pia kilikuwa kama hazina ya ujuzi wa kitaalamu.

Baadaye, Beda Mhashamu aliandika wasifu wa maisha ya Aidani pamoja na miujiza yake yote.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Attwater, Donald and Catherine Rachel John. The Penguin Dictionary of Saints. 3rd edition. New York: Penguin Books, 1993. ISBN 0-14-051312-4.
  • Powicke, F. Maurice and E. B. Fryde Handbook of British Chronology 2nd. ed. London:Royal Historical Society 1961

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.