Wafiadini wa Otranto

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Masalia ya wafiadini katika kanisa kuu la Otranto, Italia.

Antonio Primaldo na wafiadini wenzake, maarufu kama Wafiadini wa Otranto, walikuwa wakazi 813 wa Otranto, leo katika wilaya ya Lecce, Italia kusini, waliouawa tarehe 14 Agosti 1480 kwa kushika imani ya Ukristo na kukataa kusilimu baada ya mji wao kutekwa na Waturuki chini ya Gedik Ahmed Pasha.

Walitangazwa na Papa Klementi XIV kuwa wenye heri tarehe 14 Desemba 1771, halafu na Papa Fransisko kuwa watakatifu tarehe 12 Mei 2013.

Sikukuu yao huadhimishwa tarehe 14 Agosti[1].

Historia[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 28 Julai 1480 jeshi la baharini la Kituruki likiongozwa na Gedik Ahmed Pasha, likiwa na meli 150 na askari 18,000, lilitua karibu na kuta za Otranto.

Ngome ya Otranto.

Baada ya mapigano ya siku 15, tarehe 11 Agosti, Gedik Ahmed alifaulu kuteka mji akaagiza wanaume wote kuanzia umri wa miaka 15 wauawe, watoto chini ya umri huo na wanawake wote wafanywe watumwa.

Inakadiriwa 12,000 waliuawa na 5,000 walitekwa utumwani.[2]

Baadhi ya walionusurika pamoja na wakleri walikimbilia kanisa kuu ili wasali pamoja na askofu wao mzee, Stefano Pendinelli.

Gedik Ahmed aliwaagiza waongokoe Islam, lakini alikataliwa kabisa, hivyo alivamia kanisa pamoja na askari zake akawaua wote aliowakuta ndani, wakiwa pamoja na Pendinelli, aliyehimiza wote kumuelekea Mungu kabla hajauawa na kukatwa vipandevipande, wakati kamanda alikatwakatwa akiwa hai.

Baada ya hapo kiongozi wa umati akawa Antonio Pezzulla, maarufu kama Il Primaldo, ambaye pia alikataa kusilimu.

Tarehe 14 Agosti Gedik Ahmed aliwafunga waliobaki na kuwapeleka kwenye kilima cha Minerva, ambapo zaidi ya 800 walikatwa kichwa mbele ya macho ya familia zao.

Primaldo alikuwa wa kwanza kuuawa - shahidi mmoja alisema mwili wake uliendelea kusimama baada ya kichwa kukatwa mpaka alipokufa wa mwisho wao, ingawa Waturuki walijaribu kuuangusha chini.

Kumbukumbu zinasema kwamba alipoona hayo, Mturuki mmojawapo, jina lake Bersabei, aliongokea Ukristo akauawa na askari wenzake.

Otranto ulitekwa tena na Waaragona chini ya mfalme Alfonso II wa Napoli.

Tarehe 13 Oktoba 1481 maiti zao zilipatikana hazijaoza, zikahamishimiwa katika kanisa kuu.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Martyrologium Romanum
  2. Paolo Ricciardi, Gli Eroi della Patria e i Martiri della Fede: Otranto 1480-1481, Vol. 1, Editrice Salentina, 2009

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • (Kiitalia) Paolo Ricciardi, Gli Eroi della Patria e i Martiri della Fede: Otranto 1480-1481, Vol. 1, Editrice Salentina, 2009
  • (Kiitalia) Grazio Gianfreda, I beati 800 martiri di Otranto, Edizioni del Grifo, 2007

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.