Vitabu vya hekima
Miongoni mwa aina za vitabu vya Biblia vipo vile vinavyojulikana kama vitabu vya hekima. Kati ya vitabu hivyo, Agano la Kale lina Methali , Kitabu cha Yobu, na Mhubiri, ingawa hata baadhi ya Zaburi na sehemu za vitabu vingine pia vinaweza kuhesabiwa kuwa ni maandiko ya hekima. Tena, kati ya Deuterokanoni, Kitabu cha Yoshua bin Sira na Kitabu cha Hekima ni vitabu vya hekima.
[hariri] Maana ya vitabu hivyo
Kadiri ya Biblia, Mungu alitumia aina mbalimbali za watu, kama vile wahubiri na walimu, ili kuwafundisha na kuwaongoza watu wake.
Alitumia ma[kuhani]] ili katika kuendesha ibada wafundishe na kuangalia sheria yake (Law 10:8-11; Kum 33:10; Mal 2:7), na manabii ili walete ujumbe wa kufunulia makusudi yake na kuwageuza watu waache dhambi zao na kumtii Mungu (Eze 2:3-5; Amo 3:1, 7-8; Mik 3:8).
Pia alitumia walimu wa hekima. Watu hao wenye hekima walikuwa miongoni mwa walimu maalumu katika Israeli (Yer 18:18; Isa 29:14). Hawakujidai kuwa wamepata mafunuo kutoka kwa Mungu, bali walieleza mambo ya maisha ya kila siku kama watu wenye imani, wakawafundisha wengine njia iliyo bora (Mhu 12:9-10).
Maandiko ya Biblia yanayotokana na walimu wa hekima yanaonyesha kwamba watu wenye hekima waliweza kutazama mambo ya maisha kwa namna mbalimbali, hata mwalimu yuleyule aliweza kutafakari mambo muhimu akiangalia sehemu tofauti. Kwa mfano, mwandishi wa Mithali anakubali kwamba kanuni za kawaida si lazima zifae kwa kila jambo (Mit 26:4-5), ambapo waandishi wa Ayubu na Mhubiri wanatambua kwamba, ingawa kuna hali ya pekee au isiyo ya kawaida, kanuni za kawaida bado ni msingi wa mafundisho ya hekima (Ayu 28:20-28; Mhu 7:1-13).
Walimu wa hekima walikuwa wachaji wa Mungu waliotazama maisha pamoja na ugumu na furaha yote, ili wawasaidie watu wa Mungu watambue makusudi ya maisha waliyopewa na Mungu. Ingawa waliweza wakatambua maisha ya baada ya kufa (Ayu 19:26), lengo lao kuu lilikuwa kushughulika na mambo yanayowakabili watu katika maisha ya sasa.
[hariri] Utunzi wa vitabu hivyo
Pengine ni wakati wa kurudi toka uhamisho wa Babeli kwamba, baada ya muda mrefu wa mapokeo ya sauti, vilianza kuandikwa vitabu hivyo (Mithali, Ayubu) na vinginevyo (Wimbo Ulio Bora, Zaburi nyingi). Ingawa vinafanana na vile vya makabila ya jirani, vinafikiria maisha kwa mwanga wa imani katika Mungu aliye mmoja, hasa kwa kuzingatia uzima na kifo, uchungu, mwenendo, heri n.k.
Mithali ndicho kitabu kinachotuletea mawazo ya zamani zaidi na ya kwamba Mungu anamtuza mwadilifu na kumuadhibu mwovu hapa duniani. Kitabu cha Ayubu kinakataa mtazamo huo kwa kuonyesha hali halisi, yaani kuwa duniani mara nyingi mwadilifu ndiye anayeteseka; hata hivyo binadamu hawezi kujua ni kwa nini: basi amuachie Mungu na kumuabudu katika fumbo lake (42:1-6). Wimbo ulio Bora haumtaji Mungu wala dini: ulihusu mapenzi ya wachumba, lakini ukaja kufafanuliwa kama mapenzi ya Mungu na Israeli wanaotafutana ili kuungana kabisa. Zaburi, ambazo zilitungwa na kurekebishwa polepole kwa muda unaokaribia miaka elfu, yaani muda ule wote uliotumika kutunga vitabu vingine vyote vya Agano la Kale, ndizo sala za kishairi au nyimbo ambazo katika hali ya sifa, ibada, shukrani na dua zinajumlisha Biblia nzima.
Halafu chini ya utawala wa Kiyunani, unabii ulipokuja kwisha (1Mak 9:27), badala yake yalitolewa maandiko ya kiapokaliptiko (hasa kitabu cha Danieli ambacho ni kama Kitabu cha Ufunuo cha Agano la Kale), hadithi (Kitabu cha Yona, Kitabu cha Tobiti, Kitabu cha Esta, Kitabu cha Yudith) na vitabu vingine vya hekima (Mhubiri, Yoshua bin Sira, Hekima). Humo tunaona maendeleo ya ufunuo, hasa kwa sababu Wayahudi wengi walianza kusadiki ufufuko wa wafu na mengineyo.
Mhubiri alisisitiza ubatili wa malimwengu yote (1:1-11) akimuunga mkono mwandishi wa Ayubu: mang’amuzi yanaonyesha matarajio ya kidunia hayana maana (8:10-17). Yoshua bin Sira alikabili pia masuala hayo (15:11-16:23), akituelekeza tutafute jibu katika siku ya mwisho. Kitabu cha Hekima kinakisiwa kuwa cha mwisho kuandikwa kabla ya Yesu kwa kuwa kilitungwa miaka 50 tu K.K. huko Misri katika lugha na utamaduni wa Kiyunani. Kina mpango mzuri sana na kutoa jibu wazi kuhusu suala la haki ya Mungu kwa waadilifu na waovu, kikifundisha uzima wa milele (2:23-3:10) hata kuliko kilivyowahi kufanya kitabu cha Danieli (12:1-4).