Ukuta wa Maombolezo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mlima wa Hekalu ya Yerusalemu wakati wa Herode
Wayahudi wakisali mbele ya Ukuta wa Maombolezo
Ukuta wa Maombolezo
Papa Fransisko kwenye Ukuta wa Maombolezo.
Ukuta wa Maombolezo

Ukuta wa Maombolezo (KWA Kiebrania: הכותל המערבי - hakotel hama'ariv "ukuta wa magharibi") katika mji wa kale wa Yerusalemu ni patakatifu pa dini ya Uyahudi.

Ukuta wa hekalu la pili[hariri | hariri chanzo]

Ukuta huo ni mabaki pekee yanayoonekana ya hekalu la Yerusalemu la pili jinsi lilivyopanuliwa na mfalme Herode Mkuu kuanzia mwaka 20 KK.

Hekalu hilo lilibomolewa na Waroma mwaka 70 BK wakati wa vita ya Waroma dhidi ya Wayahudi.

Ukuta si sehemu ya hekalu lenyewe bali ulikuwa ukuta wa pembeni wa uwanja uliotengenezwa kwa vifusi kwenye mlima wa hekalu.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Jina la "Ukuta wa Maombolezo" limetokana na desturi ya Wayahudi kuonyesha huzuni yao juu ya kuharibiwa kwa hekalu hasa wakisali mahali hapa. Asili ya jina inaaminiwa kuwa lugha ya Kiarabu, halafu likaingia katika lugha nyingi. Kwa Kiebrania ukuta huitwa "ukuta wa magharibi" tu na hata jina hili limeenea katika lugha mbalimbali.

Umuhimu katika imani ya Kiyahudi[hariri | hariri chanzo]

Wayahudi huheshimu mahali hapa kwa sababu ni sehemu ya hekalu la Yerusalemu la mwisho tena sehemu ya mabaki haya yaliyo karibu na Patakatifu pa Patakatifu pa hekalu lile.

Wengi wao huamini ya kwamba Patakatifu pa Patakatifu palikuwa mahali pa kuwepo kwa Mungu duniani ya mlango wa mbinguni ni juu yake. Hivyo ukuta wa magharibi ni sehemu ya karibu na mlango huu.

Wayahudi wamehiji kwenda Yerusalemu kwa karne nyingi kwa kusudi la kusema sala hapahapa.

Kuna desturi ya kale ya kuandika maombi kwa karatasi na kuweka karatasi hizi kati ya mawe ya ukuta.

Fitina juu ya ukuta[hariri | hariri chanzo]

Wayahudi walikataliwa kwa muda mrefu kupanda juu ya mlima wa hekalu.

Baada ya Yerusalemu kuharibiwa mara ya pili na Waroma (70), na baada ya hao kushinda vita vya pili dhidi ya Wayahudi mwaka 135 eneo la hekalu pamoja na mji wote likakataliwa kwa Wayahudi.

Baada ya utekaji wa Waarabu kulikuwa na vipindi ambapo Wayahudi waliruhusiwa kutembelea mlima wa hekalu na vipindi vingine ambapo walikataliwa. Hivyo desturi ya kusali mbele ya ukuta wa magharibi ilianza.

Tangu takriban miaka 500 marabi wengine walianza kufundisha ya kwamba Myahudi asitembee kwenye mlima kwa sababu kuna hatari ya kuingia katika sehemu takatifu bila ya kutakaswa awali; hasa sehemu za Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu ziliruhusiwa kwa makuhani tu au hata kuhani mkuu pekee. Leo kuna tangazo lenye onyo la Rabi Mkuu wa Israel mbele ya geti la kuingia kwenye eneo la mlima wa hekalu linalosema Myahudi asiingie. Ila tu si marabi wote wanaokubali.

Siku hizi kuna usalama mkali kama kwenye uwanja wa ndege: wote wanaoelekea ukutani wanapita kwenye geti wanapochekiwa wakipaswa kufungua mifuko yote. Watu wote wanaruhusiwa kuingia ila tu wanaume wanaombwa kuvaa kofia kufuatana na desturi ya Kiyahudi.