Kiswahili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Swahili language)
Rukia: urambazaji, tafuta
Maeneo yenye wasemaji wa Kiswahili

Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye misamiati mingi ya Kiarabu inayozungumzwa katika eneo kubwa la Afrika ya Mashariki.

Lugha hii ina utajiri mkubwa wa misamiati, misemo, mithali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo. Kiswahili hutumika mashuleni na kuna vitabu vingi vilivyotungwa kwa kutumia lugha hiyo, vikiwa pamoja na vile vya hadithi, hekaya au riwaya.

Yaliyomo

Historia ya lugha[hariri]

Makala kuu ya: Historia ya Kiswahili

Lugha ilianza takriban miaka 800-1000 iliyopita katika mazingira ya vituo vya biashara vya pwani ambako wafanyabiashara kutoka Uarabuni, Uajemi na Uhindi walikutana na wenyeji Waafrika. Lugha kuu ya kimataifa ya biashara hiyo ilikuwa Kiarabu.

Inaonekana ya kwamba lugha mpya ilijitokeza wakati wenyeji wa pwani, waliokuwa wasemaji wa lugha za Kibantu, walipopokea maneno mengi hasa ya Kiarabu katika mawasiliano yao. Kwa hiyo msingi wa Kiswahili ni sarufi na msamiati wa Kibantu pamoja na maneno mengi ya Kiarabu. Imekadiriwa ya kwamba theluthi moja ya maneno ya Kiswahili yana asili ya Kiarabu.

Kando ya Kiarabu kuna pia athira ya lugha mbalimbali kama Kiajemi, Kihindi na Kireno. Wakati wa karne ya 20 maneno mengi yalipokewa kutoka Kiingereza.

Kwa karne nyingi iliandikwa kwa herufi za Kiarabu (سواحلي sawaHili au لغة سواحيلية lugha sawaHiliya).

Sarufi ya kwanza pamoja na kamusi iliandikwa mwaka 1848 na Dr. Ludwig Krapf huko Rabai Mpya / Mombasa.

Kiswahili kilikuwa na lahaja nyingi kutokana na lugha mbalimbali za Kibantu zilizochangia mle.

Tangu karne ya 19 lugha ilianza kuenea barani kwa njia ya biashara.

Wakati wa ukoloni wa Uingereza lugha ilisanifishwa kwa njia ya Kamati ya kimaeneo ya lugha ya Kiswahili kwenye msingi wa lahaja ya Unguja.

Wasemaji[hariri]

Hakuna hakika kuhusu idadi ya wasemaji wa lugha hiyo; idadi zinazotajwa zinatofautiana. Wasemaji wanaoitumia kama lugha ya kwanza wako labda kati ya milioni 7 hadi 10, na wasemaji wa lugha ya pili zaidi ya milioni 70. Idadi ya wasemaji wa lugha ya kwanza inakua, kwa sababu lugha inaenea katika maeneo ambapo lugha nyingine zilikuwa lugha kuu, na hasa katika miji ya Tanzania imekuwepo lugha kuu, badala ya lugha za kikabila.

Kati ya nchi ambapo Kiswahili kinatumika ni Tanzania, Kenya, Uganda, Kongo-Kinshasa, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Somalia na visiwa vya Bahari Hindi kama Visiwa vya Ngazija (Komoro).


kiswahili ni lugha yenye historia ndefu iliyoanzia kuandikwa na kusomwa kulingana na umri wa vyanzo vya maandiko au makala mbalimbali za Lugha ya kiswahili zilizoandikwa na wageni (waarabu,wajapan na wageni kutoka mataifa mengine) asili au chanzo cha lugha ni mchanganyiko wa lugha mbalimbali za kibantu na lugha za maifaita ya mwanzo yaliyofika Pwani ya afrika mashariki wakiwemo waarabu,waajemi,wahindi,wajapani kimsingi lugha ya kiswahili ina msamiati Mwingi wa lugha za kipatu(maeneno yanayoishia na irabu mfano kitenzi piga,kula, lima) pia inaeleweka kuwa kila lugha huwa na njia mbalimbali za kujiongezea msamiati wake ili kukidhi mahitaji ya wanaohusika kimatumizi ndio maana katika kiswahili kuna misamiati kutoka lugha mbalimbali za kigeni kama vile kiarabu,kiingereza,kijerumani,kihindi,kiajemi kijapan hii haitoshi kusema lugha ya kiswahili ina asili ya lugha fulani kutokana na idadi kubwa yamsamiati bila kuangalia viwango vingine vya lugha kama fonolojia,sintaksia,mofolojia na semantiki hitimisho tunapenda ieleweke kuwa asili ya lugha ya kiswahili si kiarabu wala kiajemi kwa kigezo cha msamiati bali asili ya lugha ya kiswahili ni lugha za kibatuntu kulingana na matamshi, muundo wa tungo, maumbo ya maneno na maana pamoja na usanifishaji uliofanywa na Waingereza mwaka 1928.

Lugha rasmi[hariri]

Kiswahili kimekuwa lugha rasmi katika nchi zifuatazo:

  • Kenya: ni lugha ya taifa lakini Kiingereza ni lugha rasmi ya kiutawala; Kiswahili ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kati ya wananchi wakikutana nje ya eneo lenye kabila moja tu; ni lugha inayofundishwa lakini si lugha ya kufundisha mashuleni; ni lugha inayotumika na polisi na jeshi, ni lugha ya kuhutubia wananchi mjini na kitaifa; sehemu za ibada makanisani zinatumia Kiswahili; kuna gazeti moja tu la Kiswahili; sehemu za programu redioni na kwenye runinga ni kwa Kiswahili. Lugha inachanganywa mara nyingi na Kiingereza na lugha za maeneo au za kikabila. Hata hivyo baada ya rasimu ya katiba mpya kupitishwa tarehe 4 Agosti 2010, Kiswahili sasa kitakuwa lugha rasmi, sawa na Kingereza.
  • Uganda: kimetangazwa kuwa lugha ya kitaifa tangu 2005; iliwahi kuwa lugha ya kitaifa wakati wa utawala wa Idi Amin; wakati wa ukoloni ilifundishwa mashuleni ikaelekea kuwa lugha rasmi pamoja na Kiingereza lakini matumizi haya yalipingwa hasa na Waganda hivyo Waingereza waliacha mipango hiyo. Ni lugha ya polisi na jeshi, hali ambayo imeleta ugumu kwa lugha kukubalika na wananchi wengi kutokana na historia ya utawala wa kijeshi Uganda; watu wengi bado hukumbuka hasa matusi ya wanajeshi waliowatesa wakisema Kiswahili. Lakini kuna maeneo ya Uganda ambako Kiswahili kinatumiwa na watu wengi kama lugha ya sokoni na barabarani. Wona UBC, WBS tv.

Lugha ya kwanza, lugha ya pili[hariri]

Kiasili Kiswahili kilikuwa lugha ya kwanza tu ya wakazi wa miji ya Waswahili kwenye pwani, katika sehemu za pwani pia kijijini. Baada ya kuenea kimekuwa lugha ya watu wengi mjini hasa Tanzania lakini pia Kenya.

Kimeenea zaidi kama lugha ya mawasiliano na biashara pale ambako watu wa makabila mbalimbali wanakutana. Pamoja na nchi zinazotajwa hapo juu Kiswahili kinatumika katika Kaskazini ya Msumbiji, Kusini kabisa ya Somalia, Mashariki ya Burundi. Maeneo ya mpaka wa Tanzania kuna pia wasemaji kadhaa huko Malawi na Zambia.

Tanzania na Kenya zilipokea wakimbizi wengi waliojifunza Kiswahili lakini hakuna uhakika kama bado kinatumika wakirudi Rwanda, Sudan au Somalia.

Kimataifa[hariri]

Lugha hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa jumla, na hasa Africa, kwa sababu ya kuenea kwake nchi mbali mbali, na kukusanya kwake watu wa makabila na nchi kadha wa kadha wakaweza kufahamiana kwa lugha moja, hasa ilivyokuwa ni lugha mojawapo katika lugha kubwa za Africa ambazo zinachukuwa mahala pa lugha za kigeni na Wakoloni, kama Kiarabu, Kiurdu, Kihebrania, Kireno na kadhalika.

Leo, imekuwa inatumiwa katika kusambaza habari katika vituo mbali mbali ulimwenguni kama vile Sauti ya Amerika, BBC, Deutsche Welle, Monte Carlo, na nchi nyenginezo za Uchina na Urusi na Irani na kwengineko. Aidha, imekuwa ni mojawapo ya lugha muhimu zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini Marekani, Uingereza, Ulaya, Urusi, Uchina, na barani Afrika.

Maendeleo ya Kiswahili[hariri]

Lugha ina maendeleo: inaweza kukua, kukwama au kufa. Athira nyingi hutokea bila mpangilio pale ambako wasemaji wanapokea maneno mapya, wanaacha kutumia maneno mengine au hubadilisha kawaida ya matamshi au sarufi. Haya yote hutokea pia katika uwanja wa Kiswahili.

Kuna mzaha unaosimuliwa hasa Tanzania: Kiswahili kilizaliwa Unguja, kilikua Tanzania Bara, kikafa Kenya na kuzikwa Uganda. Hali halisi Kiswahili kina maendeleo yake katika nchi hizo zote labda zaidi Kongo. Lakini itategemea pia juhudi za serikali kama umoja wa lugha utatunzwa kwa sababu kuna athari nyingi kutoka lugha za kila eneo zinazoingia katika ukuzi wa Kiswahili kwa namna zinazotofauitiana.

Taasisi zinazokuza Kiswahili[hariri]

Kuna taasisi zinazolenga kukuza na kuimarisha Kiswahili kama vile Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na idara za Kiswahili katika vyuo vikuu vingine vya Kenya na pia Uganda.

Nchini Tanzania kuna Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ilhali nchini Kenya kuna Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). BAKITA na CHAKITA pamoja na wawakilishi kutoka Uganda wanaandaa kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki (BAKAMA).

Uchunguzi wa Kiswahili huendelea pia katika idara za vyuo vikuu vingi duniani, kwa mfano katika Institute National des Langues et Civilisations Orientales, mjini Paris, Ufaransa. Matumizi yake ni kwa njia ya lahaja za Kingwana.

Kamusi za Kiswahili[hariri]

Makala kuu ya: Kamusi za Kiswahili

Kati ya shughuli muhimu ni kazi ya kukuza msamiati wa Kiswahili yaani kutafuta maneno mapya au kupanusha matumizi ya maneno yaliyopo ili kutaja mambo ya maisha ya kisasa yaliyobadilika. Kutunga kwa kamusi za Kiswahili hupanusha elimu hiyo.

Tazama pia[hariri]

Marejeo[hariri]

  • Ashton, E. O. 1944. Swahili Grammar (Including Intonation). London: Longmans.
  • Hinnebusch, T. J. 1979. "Swahili". Katika: T. Shopen (mhariri) Languages and Their Status, uk. 209-293. Cambridge, Massachusetts: Winthrop.
  • Hinnebusch, T. J., and S. M. Mirza. 1979. Kiswahili: Msingi wa Kusema, Kusoma na Kuandika. Lanham, MD: University Press of America.
  • Nurse, D. and Hinnebusch, T. J. 1993. Swahili and Sabaki: A Linguistic History. Berkeley and Los Angeles: University of California Press.
  • Ohly, Rajmund, Warsaw: Wydawnictwa Uniwersytetu warszawskiego,
    • Język suahili,
      • Ⅰ. Zarys gramatyki ⅠⅠ. Wybór tekstów, 1969 ;
      • Teksty suahili w piśmie arabskim wraz z ćwiczeniami i wprowadzeniem metodologicznym, 1972,
    • Literatura suahili, 1972.
  • Ohly, R., Kraska-Szlenk, I., and Podobińska, Z., Język suahili, Warsaw: Wydawnictwo Akademickie Dialog, 1998.
  • Wald, B. 1987. "Swahili and the Bantu Languages". Katika: B. Comrie (mhariri) The World's Major Languages, uk. 991-1014. New York: Oxford University Press.
  • Whiteley, W. 1969. Swahili: The Rise of a National Language. London: Methuen.
  • Zawawi, S. 1971. Kiswahili Kwa Kitendo: An Introductory Course. New York: Harper & Row.

Viungo vya nje[hariri]