Silika kadiri ya C. G. Jung

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kati ya michango mikubwa aliyoitoa Carl Gustav Jung, mwanasaikolojia wa Uswisi (1875-1961), mmojawapo ni kuainisha makundi mawili ya watu kadiri wanavyoelekeza nguvu za nafsi yao ndani mwao (wandani) au nje yao (wasondani).

Mndani[hariri | hariri chanzo]

Mndani anathamini ubora wa utendaji kuliko wingi wa vitendo. Anahitaji faragha ambapo atafakari mambo, ajue sababu zake na kuyapanga kichwani. Utafiti na msukumo wa ndani ni vya lazima kwake. Anawaza sana kabla hajatenda, kiasi kwamba pengine hatendi. Mbele ya matatizo anasema, “Hakuna haraka kuyatatua”. Mbele ya mahitaji ya watu anasitasita mpaka ajue ni ya kweli. Anapendelea kufuata dhamiri yake, kujitegemea katika shughuli, kusali na kufanya mambo peke yake. Kukutana na wengi kunamchosha. Hapendi kelele. Anafungamana na wachache ila kwa dhati. Kushirikiana na wengine kunamchanganya, na mbele ya wageni anaonekana mnyonge. Anajisetiri na kuficha hali yake isipokuwa kwa marafiki wa dhati. Kwake ni vigumu kushirikisha. Ni msikilizaji kuliko msemaji. Akisema kwa kawaida hazungumzii yale yanayomhusu. Akisimulia anapenda kuwa mwangalifu. Hakinai shughuli ileile hata akiifanya muda mrefu. Anapaswa kuangalia asijitafutie raha yake ya ndani, bila ya kujali wengine.

Msondani[hariri | hariri chanzo]

Msondani anavutwa zaidi kutenda na kujitolea kwa wengine. Tangu utotoni anaonyesha kuwa anahitaji utendaji, kuona matukio mengi na hata kuwa na kelele za kutosha. Daima anapenda kuwa kati ya watu na mambo. Anajihusisha mara na matukio mapya na kuitikia mahitaji ya watu. Anapenda kuona matokeo mazuri ya kazi zake, hatimaye anaweza akajivunia. Si mvumilivu kufanya kazi ndefu. Anazifanya haraka, pengine bila ya kufikiri. Anapenda mabadiliko na kuchoka upesi akibaki peke yake. Anasaidiwa na vitendo vya liturujia, sala ya kijumuia, kushirikisha mawazo juu ya Injili, kutoa maombi ya hiari. Kumbe ni vigumu kwake kujitafutia nafasi za sala ya moyo. Anapenda malimwengu na yanayoambatana na wengine, “unaonaje, unasemaje, unafanyeje?” Anajionyesha ni nani ulimwenguni, ni mwepesi kusema na kutambua mambo. Anapenda kujulikana, kuwa na marafiki wengi. Ni mcheshi, anasalimia upesi, anapenda kuchanganyikana na watu. Anajitambulisha kwa wageni kabla hao hawajajitambulisha. Yuko tayari kueleza maisha yake mara anapokutana na watu. Anapenda kujua wengine wanamuonaje. Anapenda kueleza kwa sauti kuliko kwa maandishi. Ni mvivu kujibu barua, lakini mwepesi kujibu simu.

Tofauti nyingine[hariri | hariri chanzo]

Watu wa makundi hayo yote mawili katika utendaji wana kawaida ya kutumia zaidi ama mawazo (mantiki), ama miguso (hisi za moyoni), ama hisi za nje (milango ya fahamu) ama machale (kuona mbali). Hivyo tunapata aina nane za silika (2x4).

Wanaotumia mawazo[hariri | hariri chanzo]

Wanaotumia mawazo katika kupima, kuchanganua, kupanga, kuchagua na kuamua mambo wanazingatia ukweli wa hakika (sheria na uthibitisho) kuliko msukumo wa moyo na maoni ya wengine. Ni wachambuzi: wanajitahidi kuelewa undani wa kila mada, kujua daima zaidi na kupata maelezo juu ya malengo na matazamio. Wanazingatia matokeo ya tafakuri yao. Wanapenda utaratibu na kupanga mambo. Wana msimamo kwa kuwa wanajua wanataka nini. Baada ya kuamua wanapenda kutekeleza. Wanapima mambo bila ya kujali utu, kwa kuwa kwao sheria na haki zinashika nafasi ya kwanza; hivyo pengine wanaumiza bila ya kujitambua. Wanaposema wanafuata mawazo yao, wanaeleza vizuri habari pamoja na rai zao na ni hodari kutoa hoja. Si wepesi kuonyesha wanavyohisi moyoni. Ajenda zao binafsi ni muhimu kwao. Hawana muda mwingi kwa mahitaji ya wengine. Hawana upendeleo, nao wenyewe wanataka kutendewa kwa haki. Wanaona vigumu kusifu na kupongeza, bali wako [[radhi kukosoa, kukemea na kushambulia wengine. Wanajihusisha na haki (stahili za watu) hata kuleta mapinduzi nchini. Wanafaa kuongoza (utawala na utekelezaji). Katika migongano wanajitafutia usalama. Katika michezo wanataka ushindi. Wanajiuliza, “Nitumie njia gani? Nipangeje mawazo yangu vizuri?”

Wanaotumia miguso[hariri | hariri chanzo]

Wanaotumia miguso wanazingatia hasa utu. Wanapokusanya maarifa wanapatwa na maono kuhusiana nayo. Wanaamua kufuatana na tunu zao. Mara nyingi wanaacha uamuzi uchukuliwe na wengine (“unichagulie”). Wanatawaliwa na hisi za moyo kuliko kufuata fikra na hoja. Wanajali na kushiriki miguso ya wengine. Wanapenda kuwafurahisha hata katika mambo yasiyo na maana. Ni hodari kushughulikia hali yao na hawapendi kuwaudhi: hivyo wanakimbilia masengenyo. Ni wapendevu, watulivu, wepesi kusamehe. Wanajitahidi kukwepa migongano na kutatua matatizo. Wanapendekeza umoja na hisia nzuri. Wanapenda kuthaminiwa na kupongezwa, hivyo hawana raha ikiwa wengine hawawajali, hawawaamini wala kuwakumbuka. Wanaelekea kusikitika na kuumia. Wako macho kuorodhesha wanaojitolea na kuchangia ustawi wa jamii, na kushauri kuhusu masuala hayo. Wanasema kwa kutumia mifano, hadithi na mang’amuzi yao. Wanajiuliza, “Nani ataguswa na uamuzi wangu?”

Wanaotumia hisi[hariri | hariri chanzo]

Wanaotumia hisi za nje katika kutambua hali halisi na utendaji ambao unahitajika na kuwezekana. Kwa kawaida ni hodari kuamua mambo na kutenda kadiri ya mazingira bila ya kusitasita. Kisha kuamua wanataka kutekeleza mara moja, wasiwe na raha mpaka uamuzi wao utimizwe. Ni hodari kwa kazi fupi. Hawapendi kuwaza hewani. Wanaamini mang’amuzi kuliko miguso. Kwao ni vigumu kujinyima matakwa ya milango ya fahamu. Wanapenda mno starehe na anasa, wanafuata tamaa za mwili. Wanathamini sana maoni na kusema ukweli. Hawaogopi kukabili wengine. Katika maelezo yao wanatumia maneno mengi na kufuata utaratibu. Wanajiuliza, “Hali ni ipi? Nifanye nini?”

Wanaotumia machale[hariri | hariri chanzo]

Wanaotumia machale katika kutambua mambo wanapendelea yale ya kutarajiwa (hata kama ni ndoto za mchana) kuliko yaliyopo sasa hivi. Wanapendelea mambo magumu na yasiyojulikana, hata yakiwa juu ya uwezo wao. Wanapenda kuvumbua vyote vinavyowezekana na kutabiri yatakayotokea (faida, hasara n.k.). Wanapata mawazo ghafla na kama kwa kuota. Wana matazamio makubwa, tena wanapenda kuvuka malengo, lakini kabla hawajayafikia, wanayarukia mengine. Hivyo wanafanya mambo mbalimbali kwa wakati mmoja. Hawapendi kufanya yaleyale daima, bali kufanya au kujifunza mapya. Ni hodari kuzua mambo, kuanzisha, kuleta mabadiliko katika yote. Wanaweza kuhamasisha watu ili nao wapate mawazo mapya na kuona mambo yanayowezekana. Hawaridhiki na ukweli unaoeleweka, wanatafuta ule uliofichika au sababu zake (“huyu ni hivi kwa sababu...”). Wanapendelea kutumia hadhiti, ndoto, mithali, mifano, mafumbo, vitendawili, maono, alama n.k. kuliko kusema kwa hakika na wazi. Ni kama wanatafuta njia ya kujieleza. Wanapepesa macho huku na huku wagundue lolote. Mitazamo yao juu ya watu na mambo ni ya jumla, hivyo mara nyingi wanashindwa kupata picha kamili kwa kugundua kasoro au sifa ndogondogo. Hawawezi kuongoza. Wakifanya kazi wanaifanya kwa bidii hasa. Wanajiuliza, “Mambo gani yanawezekana katika maisha yangu?”

Umuhimu wa kuwa na silika mchanganyiko[hariri | hariri chanzo]

Kila silika ina sifa na kasoro. Tunahitaji kufikia uwiano fulani ndani mwetu kwa kujifunza toka kwa wenzetu. Vilevile katika jamii silika tofauti zinatakiwa kukamilishana. Kumbe mara nyingi tunapuuzia mtazamo na vipawa vya wengine; matokeo yake tunaishi na kufanya kazi kwa kukwaruzana. Sababu ya kwanza ni kutojielewa wala kuelewa watu na maelekeo yao. Basi, silika moja ikitaka kutawala bila ya kujali wengine, inajitafutia hoja hata za kidini, kumbe ni suala la saikolojia tu: k.mf. kuhusu kuacha mlango wazi kwa wageni au kuufunga.

Hivyo mtu wa mawazo anamhitaji anayefuata miguso ili kutabiri miguso ya wengine (watajisikiaje), kubembeleza, kupatanisha, kushawishi, kutangaza mambo, kuuza, kusadikisha na kuamsha shauku na bidii.

Upande wake, anayetumia miguso anamhitaji mtu wa mawazo ili kuchanganua, kutofautisha, kupanga, kupima matukio, kufuata sheria na mwongozo, kutambua makosa kabla ya kutenda, kutambua kasoro zilizopo ili kusonga mbele, kutaarifu yanayotakiwa kuarifiwa, kuwa imara mbele ya upinzani, kuongoza kwa msimamo, kufukuza watu kazini kama ni lazima.

Vilevile anayefuata hisi za nje anamhitaji mtu wa machale ili kusoma alama za nyakati zijazo, kuona namna ya kujiandaa kwa kesho, kuangalia mahitaji mapya, kukabili magumu kwa bidii kuleta uwezekano mpya, kuwa na shauku, kutambua heri ijayo. Upande wake, mtu wa machale anamhitaji mtu anayefuata hisi ili kuangalia kila kitu, kusoma mawazo ya wengine, kuzingatia masharti yote ya [[mkataba, kujua kinachohitajika sasa hivi, kuzingatia tunaishi leo si kesho, hivyo furaha ya sasa ni muhimu, kutunza kumbukumbu, kukabili matatizo, kusubiri na hatimaye kuleta matokeo ya kufaa.