Nabii Ezekieli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Nabii Ezekieli alivyochorwa na (Michelangelo katika Cappella Sistina)

Kati ya manabii muhimu zaidi wa Israeli katika Agano la Kale, mmojawapo ni Ezekieli, aliyefanya kazi miaka 592-570 hivi K.K., kadiri ya ushahidi wa kitabu chake.

[hariri] Mazingira yake

Baada ya maangamizi ya Yerusalemu, polepole Wayahudi waliohamishiwa Babeli waliweza kujitafutia kazi (kwanza kilimo, halafu biashara), wakafaulu sana, hata wengine wakawa watumishi wa serikali.

Lakini upande wa dini walikuwa hatarini, kwa sababu imani ya Mwisraeli inategemea taifa, nchi na hekalu ambavyo vyote vilikuwa vimeharibika.

Kwa ajili yao Mungu akatuma tena manabii, hasa Ezekieli ambaye anaonekana kuwa alihamishwa tangu mwaka 598 K.K.

[hariri] Kazi yake

Akiwa kuhani, kama vile nabii Yeremia, katika kitabu chake alishughulika sana na hekalu na mambo ya ibada.

Upande mwingine alianzisha mtindo mpya wa kinabii ambao unaitwa wa Kiapokaliptiko (kilele chake ni Ufunuo wa Yohane) na ambao hauhusu tena matukio madogomadogo ya siasa, bali kwa njozi za ajabuajabu unaonyesha maana ya historia yote.

Katika maandiko ya namna hiyo njozi zinachukua nafasi kubwa na kwa mafumbo yake yanavutia ubunifu wetu ujitahidi kuelewa yaliyofichika katika mifano, tarakimu, rangi n.k.

Ezekieli alifundisha pia mambo mapya kama vile kwamba watu wanahitaji kufanywa upya hasa moyo na roho (11:17-20; 36:26) na kwamba Mungu anaamua kuwaokoa kabla hawajatubu ili jina lake litukuzwe katika watu wake: wokovu anaouleta hautegemei matendo mema ya binadamu, bali muungano wa Mungu na wale walioitwa kwa jina lake (16:58-63).

Hakuna kitabu kingine katika Biblia kinachosisitiza utukufu wa Mungu kuliko hicho.

Sura ya dini ya Uyahudi mpaka leo inategemea sana kazi aliyoifanya Ezekieli ya kukaza utekelezaji wa Torati hata pasipo uhuru wa kisiasa.

Vifaa binafsi
Maeneo ya wiki

Vibadala
Vitendo
Urambazaji
Vifaa
Lugha zingine