Mwanzo (Biblia)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mwa)
Rukia: urambazaji, tafuta

Kitabu cha Mwanzo (pia: Kitabu cha kwanza cha Musa; kwa Kilatini Genesis) ni kitabu cha kwanza katika Biblia. Kwa asili kimeandikwa kwa Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa בְּרֵאשִׁית, Bereshit, ambalo ni neno lake la kwanza, lenye maana ya “mwanzoni”.

Pia ni kitabu cha kwanza cha Torati (au: Torah, maana yake sheria ya kidini ya Wayahudi), yaani vitabu vitano vya kwanza vya Agano la Kale (kwa Kigiriki Pentateuko). Wengine wanaviita vitabu vitano vya Musa kwa vile inafikiriwa kuwa ndiye mwandishi wa vitabu hivyo.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Yaliyomo

Utangulizi [hariri]

Safari ya Abrahamu kutoka Mesopotamia hadi Kanaani (Mchoro wa József Molnár, 1850).

Maana ya kitabu cha Mwanzo ni 'Asili', na jina hili linafaa kwa kitabu cha Biblia kinachosimulia habari za asili ya ulimwengu, ya binadamu, ya dhambi zao na njia ya Mungu ya kuwaokoa.

Kitabu cha Mwanzo kina sura hamsini. Katika sura 1 hadi 11, historia ya awali juu ya binadamu inasimuliwa. Sura 12 hadi 50 inahusu historia ya kale ya Waisraeli. Hasa zinataja hadithi juu ya wazee au mababu wao, kama Abrahamu, Isaka, Yakobo na Yosefu.

Pentateuko [hariri]

Waebrania walitaja Pentateuko kuwa 'sheria' tu (2 Nya 17:9; Neh 8:1-3, 18; Mt 5:17-19; 11:13; 12:5; Lk 24:44). Kiebrania ni lugha ya taifa la Israeli na ndiyo lugha asili ya sehemu kubwa ya Agano la Kale. Biblia ya Kiebrania iliyotafsiriwa katika lugha ya Kigiriki au Kiyunani, iliitwa Septuaginta maana yake “sabini” (ndiyo sababu kwa kifupi inaandikwa LXX), kwa vile inafikiriwa kuwa wataalamu sabini walifanya tafsiri hiyo. Katika tafsiri hiyo, kitabu cha Mwanzo kinaitwa Genesis, maana yake “asili” na vitabu vitano vya kwanza vinaitwa Pentateuko (Kiyunani: penta = tano; teuchos = kitabu), maana yake “Vitabu Vitano”.

Katika mapokeo ya Kiebrania na ya Kikristo ya tangu zamani, Musa anatambuliwa kuwa mwandishi wa Pentateuko (Neh 8:1; 13:1; Dan 9:11; Mk 12:26; Lk 16:29-31; Mdo 15:21).

Pentateuko yenyewe haisemi kwamba Musa alikuwa mwandishi wake, hata hivyo inataja kazi yake ya uandishi. Aliandika sheria ambayo Mungu aliwapa Waisraeli (Kut 24:4; 34:27; [Kum]] 31:9, 24), aliandika historia ya Israeli (Kut 17:14; Hes 33:2) naye alitunga nyimbo na mashairi (Kut 15:1; Kum 1:22,30).

Akiwa kiongozi wa taifa, Musa alijua habari za koo za kale, nyimbo za kale na habari nyingine za mapokeo ya kale zilizokuwa zimetunzwa kwa uangalifu na kukabidhiwa kutoka kizazi hadi kizazi, kwa njia ya maneno au kwa njia ya maandiko (Mwa 5:1; 6:9; 10:1; 11:10,27). Sawa sawa na waandishi wengine, Musa aliweza kutumia habari za asili mbalimbali, hasa pale alipoandika habari za mahali au matukio asiyoweza kuyaona mwenyewe (Mwa 26:33; 35:19-20; 47:26; Hes 21:14). Zaidi ya hayo alipokea mafunuo mengine kutoka kwa Mungu (mara nyingi alisema na Mungu moja kwa moja; Kut 3:4-6; 33:9-11; Kum 34:10), pia aliandika ripoti yake mwenyewe kuhusu matukio maalumu ya maishani mwake (Kut 17:14; 24:4; Hes 33:2; Kum 31:22-24).

Watu waliochunguza maandiko ya Biblia mara nyingine walihisi kwamba Pentateuko ilikamilika muda mrefu baada ya Musa. Wanafikiri hivi kwa sababu hamna ulinganifu wa mambo kama vile masimulizi mengine, majina yaliyotumiwa kwa Mungu, matumizi ya maneno na habari za mipango ya dini ya Israeli.

Wengine wanafikiri maandiko mbalimbali baadaye yaliunganishwa kuwa kitu kimoja.

Wakati wa majadiliano hayo yote watu wengine wanasahau kwamba, jambo muhimu si jinsi Pentateuko ilivyoandikwa, bali ujumbe wake. Biblia ni kitabu ambacho umoja wake uko wazi, na ujumbe wake ni Neno la Mungu lililo hai (Neh 8:8, 14; 9:3; Yoh 5:39, 46; Mdo 28:23).

Kitabu cha Mwanzo [hariri]

Watafsiri wa Septuaginta ndio waliotumia jina la 'Mwanzo' (Genesis) kwa kitabu cha kwanza katika Biblia. Waebrania walikiita kutokana na maneno yake ya kwanza yaani 'Hapo Mwanzo'. Lakini makusudi hasa ya kitabu hiki si mwanzo na asili ya kila kiumbe kadiri ya sayansi, bali ni uhusiano ambao Mungu anautaka na watu wanaoishi katika dunia yake.

Adamu alipoumbwa na Mungu alikuwa hana dhambi. Baadaye alianguka katika dhambi, na tangu wakati huo matokeo mabaya yalirithiwa na wanadamu wote. Mwanadamu aliyeasi alistahili na alipokea hukumu ya Mungu, lakini hata hivyo hukumu hiyo siku zote ilichanganywa na neema. Mungu hakuwaangamiza wanadamu, bali alishughulika nao, ili atengeneze njia ya wokovu itakayokuwa wazi kwa watu wote. Mpango wake ulikuwa kumchagua mtu mmoja (Ibrahimu) ambaye kutokana na wazao wake angejenga taifa kubwa la Israeli, na katika taifa hilo angeonyesha mapenzi yake kwa wanadamu, na mwisho amlete Mwokozi wa ulimwengu (Yesu).

Kitabu cha Mwanzo, licha ya kuonyesha jinsi mwanadamu alivyomwasi Mungu na kuanguka katika hukumu yake, pia kinaonyesha jinsi Mungu alivyoanza kutekeleza mpango wake mkubwa wa wokovu kwa wanadamu. Baada ya taarifa ya ahadi za Mungu alizomwahidia Ibrahimu za kumfanya kuwa taifa kubwa na kuwapa watu wa taifa hilo nchi ya urithi katika Kanaani, pia kinaonyesha jinsi ahadi hizo kuhusu taifa na nchi hiyo zilivyoanza kutimizwa.

Muhtasari [hariri]

  • 1:1-2:3 Habari za uumbaji
  • 2:4-4:26 Siku za kwanza za mwanadamu
  • 5:1-32 Vizazi vya Adamu mpaka Nuhu
  • 6:1-9:29 Uovu wa mwanadamu na hukumu ya Mungu
  • 10:1-11:26 Vizazi vya Nuhu mpaka Abramu
  • 11:27-15:21 Abramu aingia nchi ya ahadi
  • 16:1-25:18 Abramu na mrithi aliyeahidiwa
  • 25:19-28:9 Isaka akabidhi urithi
  • 28:10-36:43 Yakobo aimarisha familia
  • 37:1-50:26 Kukua kwa ukoo wa Israeli na kuhama kwenda Misri

Marejeo [hariri]

Vitabu vya ufafanuzi [hariri]

  • McKeown, James (2008). Genesis. Eerdmans. 
  • Towner, Wayne Sibley (2001). Genesis. Westminster John Knox Press. 

Vingine [hariri]

  • Davies, G.I (1998). "Introduction to the Pentateuch", in John Barton: Oxford Bible Commentary. Oxford University Press. 

Viungo vya Nje [hariri]

Commons-logo.svg
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo Kutoka Walawi Hesabu Kumbukumbu Yoshua Waamuzi Ruthu Samueli I Samueli II Wafalme I Wafalme II Mambo ya Nyakati I Mambo ya Nyakati II Ezra Nehemia TobitiDK YudithiDK Esta Wamakabayo IDK Wamakabayo IIDK Yobu Zaburi Methali Mhubiri Hekima DK SiraDK Wimbo Bora Isaya Yeremia Maombolezo BarukuDK Ezekieli Danieli Hosea Yoeli Amosi Obadia Yona Mika Nahumu Habakuki Sefania Hagai Zekaria Malaki - Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.