Mitholojia ya Kirumi
Mitholojia ya Kirumi ni jumla ya imani kuhusu miungu ya Roma ya Kale jinsi ilivyosimuliwa katika hadithi za kidini za utamaduni huu.
Yaliyomo |
Dini bila vitabu vitakatifu [hariri]
Dini ya Roma ya Kale haikuwa na msahafu au vitabu vitakatifu kama Biblia, Qurani au Veda. Hadithi zilizoonyesha imani kuhusu miungu zilisimuliwa katika familia, kuimbwa na washairi na baadaye tu kuandikwa na waandishi bila kuunda andiko maalumu la kidini.
Dini ya wakulima [hariri]
Kiasili Waroma wa kale walikuwa wakulima na hiyvo dini yao iliangalia miungu iliyowakilisha nguvu asilia na matukio muhimu katika mazingira yao kama Tellus (ardhi), Ops (mavuno), Ceres (mazao ya shambani). Waroma waliwaza nguvu hizi kama kimungu wakitafuta kuziathiri kwa kuzipa uso wa mungu fulani aliyeweza kuabudiwa.
Kupokea miungu ya majirani na mataifa yaliyoshindwa [hariri]
Lakini Waroma wa Kale waliathiriwa wenyewe sana na majirano yao walioitwa Waetruski waliowaletea habari nyingi za miungu ya Kigiriki na hivyo mawazo mengi yenye asili ya Kigiriki yaliingia katika dini ya Kiroma. Mara nyingi walijaribu kulinganisha miungu ya Kigiriki na miungu yao wenyewe kwa kusema kwa mfano mungu Ares wa Wagiriki ni yeye yule kama Mars wa Kiroma, ni tofauti ya lugha tu.
Baada ya kupanua milki yao kuwa Dola la Roma lililojumlisha mataifa kwenye mabara matatu ya Ulaya, Afrika na Asia waliimarisha mtindo huu uliowasaidia kuwatawala wale watu wengi wenyi tamaduni tofautitofauti. Walikubali miungu ya kila taifa kwa kuwaingiza katika dini yao ama kama jina tofauti ya mungu aliyekuwepo tayari kwao au kama nyongeza. Hii haikuwa vigumu mno katika imani yao iliyojua miungu mingi.
Miungu mikubwa na miungu ya nyumba [hariri]
Waroma waliabudu hasa miungu mikubwa 12 iliyosimamia mwendo wa dunia kwa jumla. Lakini katika maisha ya kila siku miungu inayoweza kuitwa midogo au miungu ya binafsi ilikuwa muhimu pia. Iliitwa Lares au Penati ilitazamiwa kama mapepo ya marehemu yaliyokaa karibu na au ndani ya nyumba ilhali haionekani. Kila asubuhi na wakati wa sikukuu fulani baba wa nyumba aliwatolea sadaka ndogo na sanamu zao zilikuwa na nafasi ya heshima katika nyumba.
Miungu mikubwa [hariri]
| Jina la Kigiriki | Jina la Kirumi | Maelezo |
|---|---|---|
| Aφροδίτη (Afrodítē) | Venus | Mungu wa kike wa upendo na uzuri. |
| Aπόλλων (Apóllōn) | Apollo | Mungu wa nuru na ushairi. |
| Άρης (Árēs) | Mars | Mungu wa vita. |
| Άρτεμις (Ártemis) | Diana | Mungu wa kike wa uwindo. |
| Αθηνά (Athēná) | Minerva | Mungu wa kike wa elimu na hekima. |
| Δημήτηρ (Dēmḗtēr)
Δήμητρα (Dḗmētra) |
Ceres | Mungu wa kike wa mimea na kilimo. |
| Διόνυσος (Diónysos) | Bacchus | Mungu wa divai. |
| Έρως (Érōs) | Amor | Mungu wa mapenzi. |
| ᾍδης (Ádēs) | Pluto | Mungu wa kuzimu na bwana wa waliokufa. |
| Ήφαιστος (Ḗfaistos) | Vulcanus | Mungu wa volkeno na uhunzi. |
| Ήρα (Ḗra) | Juno | Mungu wa kike wa ndoa na malkia ya miungu. |
| Ερμής (Ermḗs) | Mercurius | Mjumbe wa miungu. |
| Ἑστία (Estía) | Vesta | Mungu wa kike wa moto. |
| Ποσειδῶν (Poseidṓn)
Ποσειδώνας (Poseidṓnas) |
Neptunus | Mungu wa bahari. |
| Ζεύς (Zeús)
Δίας (Días) |
Iuppiter
|
Mungu wa radi na mfalme wa miungu. |