Mbeya (mji)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Jiji la Mbeya
Jiji la Mbeya is located in Tanzania
Jiji la Mbeya
Jiji la Mbeya

Mahali pa mji wa Mbeya katika Tanzania

Majiranukta: 8°53′24″S 33°25′48″E / 8.89000°S 33.43000°E / -8.89000; 33.43000
Nchi Tanzania
Mkoa Mbeya
Wilaya Mbeya Mjini
Idadi ya wakazi
 - Wakazi kwa ujumla 541,603
Mkowa wa Mbea

Jiji la Mbeya ni mji mkubwa kusini-magharibi mwa Tanzania wenye hadhi ya jiji na msimbo wa Posta 53100.

Mbeya ni kitovu cha Nyanda za Juu za Kusini ambazo ni eneo la uzalishaji wa mazao mengi.

Ni makao makuu ya mkoa wa Mbeya.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Mji umeenea katika bonde kati ya safu za milima ya Mbeya na milima ya Uporoto. Mlima mkubwa unaoonekana kutoka mjini ni Mlima wa Mbeya (Mbeya Peak) wenye urefu wa m 2818.

Eneo la mji ni kati ya m 1600 kitovuni na m 1900 au zaidi juu ya UB kwenye mitelemko ya mlima Loleza.

Hali ya hewa haina joto kali kutokana na kimo. Wakati wa Juni-Julai halijoto wakati wa usiku inaweza kushuka chini hadi 0 °C, mlimani hata chini zaidi.

Mvua zinaanza mwezi Novemba hivyo ni wakati wa kupanda. Kwa kawaida mvua zinasimama tena Januari-Februari na kunyesha kwa wingi Machi-Aprili.

Uti wa mgongo wa mji ni barabara kuu ya TANZAM inayounganisha sehemu za nje kati ya Uyole na Mbalizi.

Kitovu kipya cha mji kinahamishwa kwenda kata ya Foresti iliyoko kando ya barabara kuu.

Station Road huko Mbeya sehemu ya kale ya mjini.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Jina la Mbeya limetokana na neno la Kisafwa "Ibheya" ambayo maana yake ni chumvi, kwani miaka mingi wafanyabiashara walikuwa wanafika mahali hapo kubadilishana mazao yao kwa chumvi.

Mlima mkubwa ulio karibu ulijulikana kwa jina la "Mbeya"[1] wakati wa ukoloni wa Kijerumani, na mji ulipokea baadaye jina kutokana na mlima huu.

Mji wa kisasa wa Mbeya ulianzishwa na wakoloni Waingereza mnamo mwaka 1927. Wakati ule dhahabu ilianza kupatikana mlimani karibu na Mbeya hadi Chunya.

Historia inavyoonekana katika jiografia ya Mbeya[hariri | hariri chanzo]

Mji ulianzishwa katika sehemu zinazoitwa bado Uhindini, Uzunguni na Majengo. Mji ulipangwa kufuatana na kawaida ya miji wa kikoloni ya Afrika ya Mashariki kuwa na sehemu tatu:

Makanisa ya kale kama ishara ya historia[hariri | hariri chanzo]

Mahali pa makanisa ya kale panaonyesha ugawaji huu wa kihistoria:

  • Kanisa la Anglikana lililokuwa dhehebu rasmi la Uingereza lipo chini ya Uzunguni na karibu na ofisi za kiserikali (zinazoelekea siku hizi kuhamishwa kwenda Foresti) kama Mkuu wa Mkoa na mahakama. Kanisa hili ni jengo dogo kwa sababu lilipangwa kwa kundi dogo la maafisa na wafanyabiashara pamoja na wakulima Waingereza wa Mbeya.
  • Kanisa la mjini la Moravian, ambalo ni dhehebu la Kikristo asilia la Mbeya liko Majengo iliyokuwa sehemu kwa Waafrika. Kati ya Waingereza hawakuwepo Wamoravian.
  • Kanisa Kuu Katoliki lilihudumia Wazungu wachache, hasa Waeire, kati ya wakoloni pamoja na Wahindi kutoka Goa na pia Waafrika: kwa hiyo iko kati ya Uzunguni na Uhindini karibu na Majengo.

Mji uliendelea kupanuka pande zote. Barabara kuu ya TANZAM inaunganisha sehemu za nje kati ya Uyole na Mbalizi.

Siku hizi sehemu kubwa ya wakazi ni Wakristo, hasa wafuasi wa Kanisa Katoliki, Kanisa la Moravian na Kanisa la Kilutheri. Makundi makubwa mjini ni Wasafwa (wenyeji) na Wanyakyusa waliohamia kutoka Rungwe. Wanyakyusa ndio waliotangulia kuleta Ulutheri mjini.

Kuna pia msikiti mkubwa na hekalu la Wahindu.

Mawasiliano[hariri | hariri chanzo]

Kituo cha reli ya TAZARA Mbeya
Treni ya TAZARA kwenye kituo Mbeya

Mbeya ni njiapanda ya njia mbalimbali muhimu: Barabara kuu ya lami kutoka Dar es Salaam (km 850) hugawanya hapa kwenda MalawiMsumbiji kupitia Tukuyu/Rungwe, na kwenda ZambiaAfrika Kusini kupitia Tunduma/Mbozi.

Vilevile njia ya reli ya TAZARA hupita Mbeya kuelekea Zambia. Kuna ghala kubwa kwa ajili ya mizigo ya Malawi inayofikishwa kwa reli kutoka Dar es Salaam bandarini ikihamishwa kwa malori kwenda Malawi.

Mbeya imekuwa na uwanja wa ndege mdogo usiokuwa na huduma ya kawaida kwa muda mrefu. Lakini kuna mipango ya kujenga uwanja mpya huko Songwe zipatazo km 40 kufuata njia ya kwenda Zambia.

Tangu miaka ya 1990 kitovu cha mji kinahamishwa kutoka eneo la zamani kwenda karibu na barabara kuu ya Dar es Salaam – Zambia.

Wakazi[hariri | hariri chanzo]

Mbeya ni mji wa nne kwa ukubwa nchini Tanzania. Idadi ya wakazi imehesabiwa kuwa 385,279 katika sensa ya mwaka 2012. Katika sensa ya mwaka 2022 walihesabiwa 541,603 [2]. Wengine 300,000 hivi wanaishi katika mazingira karibu na Mbeya mjini.

Kwa asili Mbeya ilikuwa eneo la Wasafwa. Siku hizi sehemu kubwa ya wakazi wanaweza kuwa mchanganyiko wa Wasafwa pamoja na makabila ya Wanyakyusa kutoka wilaya za Rungwe na Kyela, Wanyiha kutoka Mbozi, Wandali kutoka Ileje na Wakinga kutoka Makete.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Uchumi wa Mbeya mjini umetegemea kilimo cha mazingira yake na biashara.

Viwanda mbalimbali vilianzishwa, lakini havikufaulu sana. Kuna viwanda kwa mfano Zana za kilimo, Highland Soap, Mbeya Textiles. Mbeya Ceramics iliporomoka kitambo.

Elimu[hariri | hariri chanzo]

Pamoja na shule za sekondari kuna taasisi kadhaa za elimu ya juu kama vile:

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Wajerumani waliandika "Mbeja" wakitamka "j" kama "y", linganisha Kamusi ya Koloni za Kijerumani, makala "Usafua"
  2. https://www.nbs.go.tz

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Kata za Jiji la Mbeya - Tanzania

ForestGhanaIdudaIganjoIganzoIgawiloIlemiIlombaIsangaIsyesyeItaganoItendeIteziItijiIwambiIyelaIyungaIziwaKalobeMaangaMabatiniMaendeleoMajengoMbalizi RoadMwakibeteMwasangaMwasenkwaNondeNsalagaNsohoNzovweRuandaSindeSisimbaTembelaUyole


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mbeya bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Mbeya (mji) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.