Matatu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Matatu mjini Nairobi mwaka 2002 (bado bila kanda ya njano) ikibeba watu wengi

Matatu ni neno la kawaida nchini Kenya na Uganda la kutaja gari aina ya daladala linalotumika kama usafiri wa umma.

Jina "matatu" labda lilitokana na nauli ya sarafu tatu iliyokuwa kawaida kwa safari moja matatu yalipoanza.

Matatu huhudumia njia maalumu yenye namba yake.

Dereva anafanya kazi yake pamoja na msaidizi anayeitwa "manamba" mwenye kazi ya kukusanya pesa na kufungua au kufunga mlango.

Mara nyingi ni magari ya Kijapan yenye ruhusa ya kubeba abiria 14. Hadi mwaka 2003 matatu hayakufuata utaratibu huu wala taratibu nyingine. Ilikuwa kawaida kuingiza zaidi ya watu 20 katika gari moja lenye viti 15. Maafisa wa polisi ya barabarani (trafiki) walizoea kupokea rushwa za matatu kila siku, hivyo walishindwa kuwaambia neno.

Serikali mpya ya Rais Mwai Kibaki iliweza kubadilisha hali hiyo tangu mwaka 2003, hasa waziri wa usafiri John Michuki aliyelazimisha wenye matatu kukubali utaratibu ambao haukuwa mpya lakini ulipuuzwa miaka mingi hadi kusahauliwa isipokuwa wazee walikumbuka siku za kale.

Tangu mwanzo wa mwaka 2004 matatu yanatakiwa kuonyesha nje kanda ya rangi ya njano; dereva na manamba wawe na sare, kila kiti kinapaswa kuwa na kanda, na matatu kama mabasi yanatakiwa kuwa na "spidigavana" yaani chombo cha kukata mkasi wa gari likipita 80 km/h.

Utaratibu huu umeanza kuvurugika tena, lakini bado hali ni afadhali kuliko zamani, hasa idadi ya vifo imepungua.