Kumbukumbu la Sheria
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kumbukumbu la Sheria (pia: Kumbukumbu la Torati) ni kitabu cha tano katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na cha Agano la Kale katika Biblia ya Ukristo.
Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.
Yaliyomo |
[hariri] Majina
Kwa asili kimeandikwa katika lugha ya Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa Devarim, maana yake “maneno”, ambalo ni nomino ya kwanza katika kitabu hicho.
Maelezo yaliyomo ni kama marudio ya sheria iliyotolewa katika Mlima Sinai, kwa hiyo kitabu kimeitwa Kumbukumbu la Torati. Jina hilo linatokana na lile lililochaguliwa na waliotafsiri Agano la Kale mara ya kwanza katika lugha ya Kiyunani, kama miaka 200 hivi K.K. (tafsiri yao inaitwa Septuaginta).
Kwa lugha ya Kilatini kinaitwa Deuteronomium, maana yake “Sheria ya Pili”, kutokana na maneno ya Kigiriki 'deuteros' (maana yake ya pili), na 'nomos' (maana yake sheria).
Kwa kweli kinasisitiza sana uaminifu kwa sheria za Agano la Kale na pia tuzo na adhabu zitakazotolewa kufuatana na matendo ya Waisraeli, lakini pia upendo wa Mungu unaodai kurudishiwa.
Wengine wanakiita Kitabu cha Tano cha Mose (au Musa) kwa vile mapokeo yalimdhani kuwa mwandishi wa kitabu hicho. Siku hizi kitabu hicho cha mwisho cha Torati kinafikiriwa kuwa kiliandikwa kama miaka 600 baada ya Musa, ingawa kina namna ya hotuba alizoweza kuwatolea Waisraeli kabla hajafa. Vyote vitano pamoja kwa jina la Kigiriki vinaitwa Pentateuko.
[hariri] Yaliyomo
Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria kina sura thelathini na nne, ambazo karibu zote zinasimulia hotuba za Mose kwa Waisraeli. Mahali ni tambarare ya Moabu na wakati ni mwezi wa 11 katika mwaka wa mwisho wa matembezi ya Wanaisraeli.
- Hotuba ya kwanza (sura 1 hadi 4) yarudia matokeo muhimu ya matembezi ya jangwani ya watu wa Israeli. Inaeleza jinsi ilivyo muhimu kumtii Mungu. Kunya maonyo dhidi ya uasi.
- Hotuba ya pili (sura 5 hadi 26) ni sehemu kuu ya kitabu. Humo kuna marudio ya Amri Kumi, sheria kwa ajili ya maisha katika nchi ya ahadi na sura ya 20 ina sheria kuhusu vita.
- Hotuba ya tatu (sura 27 hadi 30) inajadili yale yatakayofuata kama watu hupuuza maagizo ya Mungu au kuyatekeleza. Mwishoni ahadi kati ya Mungu na wanaisraeli inarudiwa na Yoshua ateuliwa kuwa kiongozi mpya baada ya Musa.
Ni sura nne za mwisho tu zinazohusu mambo ya kihistoria: Yoshua kuteuliwa mwandamizi wa Mose kama kiongozi wa taifa (sura 31: Kumb 31:1-8 inasimulia jinsi Musa alivyomuachia Yoshua uongozi wa Waisraeli wote kwa kumwekea mikono = Hes 27:12-23), Mose kuimba wimbo wake wa mwisho (sura 32), baraka ya Mose kwa makabila 12 ya Israeli (sura 33), na mwishoni habari za kifo chake Mose (sura 34).
Musa alifikia mpakani mwa nchi takatifu asikubaliwe kuiingia kama adhabu ya makosa yake, ila alionyeshwa yote kutoka mlimani (Kumb 32:48-52) halafu akafariki (Kumb 34). Kazi aliyopangiwa iliishia huko, mwingine akampokea na kuendeleza ukombozi wa Kimungu. Binadamu wote ni vyombo tu vinavyotumika kwa muda fulani, halafu vinaweza kuachwa. Kumbe Mungu ndiye mtendaji mwenyewe ambaye hasinzii wala halali, bali anazidi kuwashughulikia watu wake. Kwa imani hiyo mtu anatakiwa kuwa daima tayari kuwaachia wengine nafasi yake.
Katika maneno yake yote ya kukumbukwa ni hasa yale ya 6:4-9 ambayo Mwisraeli yeyote anayakariri kila siku katika sala na kuyashika neno kwa neno.
Maneno mengine muhimu sana yapo 26:5-10: ni kama kanuni ya imani ambayo Mwisraeli alikuwa anaiungama mbele ya Mungu wakati wa kumtolea malimbuko ya ardhi. Hivyo alikuwa akikiri amepewa yote na Bwana, halafu akaweza kuyafurahia mavuno.
[hariri] Mazingira
Baada ya kupokea sheria katika Mlima Sinai, Waisraeli walikuwa jangwani kwa muda wa karibu miaka 40, wakitangatanga kati ya Sinai na Kanaani.
Katika muda huo watu wote waliokuwa na umri wa miaka 20 na zaidi walipoondoka Mlima Sinai walikufa, na kizazi kipya kilikuwa kimepata umri wa kutosha.
Kwa hiyo Musa alirudia kueleza sheria kwa watu wa kizazi hicho, kabla hawajavuka Yordani na kuingia Kanaani.
Maelezo hayo yalitolewa katika majuma mawili ya mwisho wa maisha ya Musa, Waisraeli walipokaa katika nchi tambarare ya Moabu, wakifanya maandalizi ya mwisho ya kuingia Kanaani (Hes 22:1; 35:1; Kum 1:1-5).
[hariri] Kurekebisha sheria na kuthibitisha agano
Kitabu cha Kumbukumbu si marudio tu ya maagizo na amri zilizotolewa hapo awali, bali kina maelezo mengi ya ziada. Kinataja upya amri za sheria, lakini kinatia mkazo zaidi katika maneno mengine. Sheria zilizoandikwa katika vitabu vya Kutoka, Walawi na Hesabu zilitoa amri kama madai ya moja kwa moja tu, lakini kitabu cha Kumbukumbu, kwa sababu hakikutaka kutoa mafundisho juu ya vitabu vile tu, kinaongeza kueleza kwamba uhusiano wa Waisraeli na Mungu wao lazima uwe zaidi kuliko sheria na madai ya haki tu. Uwe uhusiano wa kiroho wenye upendo na baraka.
Hali ya kitabu hiki ni ya mfano wa mhuburi kuliko wa mtoaji wa sheria, na wasomaji wake au wasikilizaji wake ni watu kwa jumla, kuliko makuhani na waamuzi tu (Kum 8:5-6; 10:12-13).
Kitabu kinasisitiza kwamba, watu watimize amri za Mungu ili kumjua na kumpenda Mungu wao zaidi, si kwa sababu tu wamedaiwa kuzitimiza katika maagano (Kum 6:3, 5-9; 7:7-8,11).
Agano ni msingi wa kitabu, lakini uhusiano baina ya Mungu na watu wake katika agano hilo ulitakiwa uwe wa upendo. Upendo mkuu wa Mungu kwa watu wake usababishe upendo wa kumtii Yeye (Kum 5:6-7; 6:1-3).
Kwa neema yake Mungu alichagua Israeli kuwa taifa lake akawaahidi kuwapa nchi ya Kanaani iwe nchi yao hasa (Kum 7:6-7; 8:1; 9:4-5).
Kama watu walitaka kufurahia baraka za agano hilo katika ushirika wa upendo na Mungu, walipaswa kujua sheria yake na kuitimiza. Kizazi kilichotangulia kiliapa kuwa na uaminifu katika agano kwa Mungu huko Sinai (Kut 24:7-8), lakini walikosa vibaya sana. Wakati huo kizazi kipya kilipokuwa tayari kuingia Kanaani, agano lilithibitishwa. Musa alirudia maneno yote ya sheria, na watu waliahidi upya kuitii (Kum 26:17-18).
[hariri] Hati za agano hapo kale
Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kina mambo mengi yanayofanana na hati za maagano jinsi yalivyofanyika katika nchi za maeneo yale hapo kale, ambapo bwana mkubwa fulani alifanya mapatano na watu waliokuwa chini yake au waliomtegemea. Maagano kama hayo hayakutokana na majadiliano ya makundi mawili yaliyokuwa sawa, bali yalikuwa kadiri ya hati ya mapatano yaliyoandaliwa na yule mkuu au mfalme fulani tu, yakitangaza mamlaka yake juu ya watu na kupanga kanuni za maisha yaliyowapasa. Watu hawakuwa na njia yo yote ila kukubali masharti ya mkuu au ya mfalme wao.
Kwa kawaida hati ya agano ilianza kwa utangulizi wa historia ambapo mkuu alijieleza akiorodhesha mambo yote aliyowafanyia watu wake. Kisha ikafuata orodha ya masharti ya maagano yaliyowekwa juu ya watu. Kwanza, watu walionywa kuwa waaminifu na watiifu kwa mkuu wao, na baadaye walionywa wasianzishe fitina yo yote kwa njia ya kufanya mapatano na mfalme mwingine. Baada ya masharti yale ya msingi, amri na sheria zake zilielezwa kinaganaga zilizohusika na matakwa ya sehemu ile.
Kwa kawaida katika hati hizo mashahidi walitajwa. Pia zilieleza faida ambazo zingetokana na utii wa watu na adhabu ambazo zingetokana na uasi. Kisha hati yake ilifungiwa na kutunzwa kwa usalama katika patakatifu pa watu waliohusika, ili iweze kusomwa wakati wote, na hapo iweze kupata nyongeza zake kama zilitakiwa.
Mara nyingine hati ilimalizwa kwa kujumlishwa muhtasari wa maagizo na masharti maalumu, au kwa ahadi kwamba maagano hayo yaendelee kwa muda wote ambao watu wangeendelea kuwa waaminifu na watiifu kwa masharti yake.
Kuhusu agano baina ya Mungu na Israeli alama nyingi za namna hiyo zinaonekana katika maandiko ya sheria zilizoandikwa katika vitabu vya Kutoka, Kumbukumbu la Torati na katika kitabu cha Yoshua. Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kimeandikwa kwa mtindo ulioelezwa hapo juu.
Licha ya mpangilio wa kitabu kwa jumla kufanana na hati za maagano kama zilivyoandikwa katika nchi zile wakati ule, hata mambo mengi yanayoshughulikiwa katika maagano hayo yanaonekana sehemu mbalimbali katika kitabu hicho.
[hariri] Muhtasari
1:1-4:43 Utangulizi wa historia
4:44-11:32 Maagizo ya msingi kuhusu agano
12:1-26:19 Amri zote zatajwa kinaganaga
27:1-30:20 Masharti ya agano
31:1-34:12 Siku za mwisho za Musa
[hariri] Viungo vya nje
Kitabu cha Kumbukumbu la Torati katika Biblia (Union Version)
Mwanzo Kutoka Walawi Hesabu Kumbukumbu Yoshua Waamuzi Ruthu Samueli I Samueli II Wafalme I Wafalme II Mambo ya Nyakati I Mambo ya Nyakati II Ezra Nehemia TobitiDK YudithiDK Esta Wamakabayo IDK Wamakabayo IIDK Yobu Zaburi Methali Mhubiri Hekima DK SiraDK Wimbo Bora Isaya Yeremia Maombolezo BarukuDK Ezekieli Danieli Hosea Yoeli Amosi Obadia Yona Mika Nahumu Habakuki Sefania Hagai Zekaria Malaki - Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.