Kikingaradi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mfumo wa kikingaradi


Kikingaradi ni kifaa kinachofungiwa juu ya nyumba, minara au majengo marefu mengine. Kwa kawaida ni nondo nene ya metali ambayo inaunganishwa na waya inayoishia kwenye pao la metali lililochimbwa ardhini.

Kazi ya kikingaradi ni kuvuta radi kwake na kuifishi ardhini bila kupita ndani ya jengo. Radi ina kiwango kikubwa cha chaji ya umeme ndani yake na inaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwenye kitu kinachopigwa naye. Pale ambako radi inatokea chaji yake inatafuta njia ya haraka ya kuingia kwenye ardhi kwa shabaha ya kutoa chaji yake. Hapo mara nyingi radi inatafuta vilele vya majengo au pia miti ambayo ni kama sehemu ya juu ya uso wa ardhi. Kuachiliwa kwa chaji katika jengo au mti kunaweza kuleta uharibifu. Mkondo wa umeme unaopatikana wakati wa kuachilia chaji unasababisha halijoto kali inayosababisha moto. Kama kuna unyevu ndani ya ukuta wa jengo unyevu huu unaanza kuchemka mara moja na kuwa mvuke kwa ghafla kunachosababisha mlipuko.

Hapo kikingaradi ni njia ambako umeme unaweza kupita na kufika ardhini haraka bila kutafuta njia ndani ya jengo. Ilhali radi daima inatafuta njia ya haraka ya kuachilia chaji yake ardhini kikingaradi kinatengenezwa kwa metali inayopitisha umeme haraka zaidi kuliko jengo lenyewe. Kwa sababu hii metali inayochaguliwa kwa kikingaradi ni kwa kawaida shaba, aloi za shaba au alumini, kwa kwa sababu metali hizi zina ukinzani mdogo kwa mkondo wa umeme. Shaba ni bora kuliko alumini lakini bei yake ni juu zaidi.


Historia[hariri | hariri chanzo]

Nyaya za kikingaradi kwenye sanamu ya mapambo iliyopo juu ya bunge la Bavaria
Kikingaradi juu ya paa ya nyumba

Mnamo katikati ya karne ya 18 wataalamu katika Ulaya na Marekani walianza kuelewa tabia za umeme. Walianza kuhisi ya kwamba uhusiano ulikuwepo baina ya umeme na radi. Mnamo 1750 Benjamin Franklin huko Pennsylvania, Marekani[1] aliandika juu ya radi kuwa umeme akapendekeza kuithibitisha kwa kupandisha kishada wakati wa ngurumo na kuona umeme kwenye kamba yake ya kushikilia. Kutokana na majaribio haya alibuni pia kikingaradi kilichowekwa mara ya kwanza kwenye nyumba yake mwenyewe, halafu mwaka 1752 kwenye ikulu ya Pennsylvania.

Mwnazoni kikingaradi kilienea polepole. Sababu muhimu ilikuwa hofu ya kuwa mtambo ungevuta radi kwake na hivyo kuongeza hatari badala ya kuipunguza.

Baada ya kuonekana kinasaidia kweli uenezaji wake umeendelea. Siku hizi kuna nchi nyingi zenye masharti ya kuweka kikingaradi kwenye majengo maalumu hasa kama jengo fulani ni jengo kubwa katika mazingira yake, limeinuliwa juu ya kimo cha miti au majengo jirani au kama liko juu ya mlima.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. wakati ule ilikuwa bado koloni ya Uingereza hadi vita ya uhuru tangu 1776