Kanisa la Wamaroni
Kanisa la Wamaroni (jina rasmi: Kanisa la Kisirya la Kimaroni la Antakya; kwa Kiaramu ܥܕܬܐ ܣܘܪܝܝܬܐ ܡܪܘܢܝܬܐ ܕܐܢܛܝܘܟܝܐ ʿīṯo suryaiṯo māronaiṯo d'anṭiokia; kwa Kiarabu الكنيسة الأنطاكية السريانية المارونية al-kanīsa al-antākīyya al-seryānīyya al-mārwnīyya; kwa Kilatini Ecclesia Maronitarum) ni moja ya Makanisa Katoliki ya Mashariki, yaani ni Kanisa linalojitegemea kisheria ndani ya umoja wa Kanisa Katoliki.
Yaliyomo |
Historia [hariri]
Mzizi wake ni katika Kanisa la Kisirya la Kiorthodoksi kwenye nchi za Syria na Lebanoni ya leo, kwa hiyo katika utamaduni wa Wakristo wenye lugha ya Kiaramu ya magharibi.
Kanisa hilo lilianza katika mvutano juu ya maamuzi ya Mtaguso wa Kalsedonia wa mwaka 451 yaliyokataliwa na Wasirya wengi. Wafuasi wa mmonaki Maroni, mwanzilishi wa monasteri maarufu katika karne ya 4, walisimama upande wa maazimio ya huo mtaguso mkuu ingawa walikuwa Wasirya ambao wengi wao walipinga maazimio la mtaguso. Kwa hiyo Wamaroni waliteswa na wenzao wakawa kundi la Wasirya waliosimama upande wa Kanisa la Kigiriki la Kiorthodoksi.
Katika mabishano yaliyofuata ndani ya Kanisa la Kigiriki Wamaroni waliamua kukaa kando, wakawa jumuiya ya pekee na kutafuta hifadhi yao kwenye milima ya Lebanoni.
Wakati wa vita za misalaba Wamaroni walielewana vizuri na Wakatoliki kutoka Ulaya wakatafuta ushirikiano nao. Hapo walikubali uongozi wa Papa wa Roma na kuwa Kanisa pekee la Ukristo wa Mashariki lililopo lote chini ya Papa.
Hali ya leo [hariri]
Linatunza liturujia, teolojia na maisha ya kiroho ya mazingira hayo kulingana na tapo lililoanzishwa na Maroni. Hadi leo sehemu za liturujia ziko kwenye lugha ya Kisirya au Kiaramu ya magharibi lakini kwa jumla Kanisa na pia jumuiya ya Wakristo wake hutumia Kiarabu.
Patriarki wake anachaguliwa na Sinodi ya maaskofu wa Kanisa hilo, halafu anamuomba Papa wa Roma ushirika kamili. Anaishi Bkerke (Lebanoni), ambapo ana jimbo lake, ingawa anatumia bado jina rasmi la Patriarki wa Antiokia.
Kanisa hilo linakubali kuwapa upadri waamini waliooa.
Uenezi [hariri]
Huko Lebanoni, ni kundi kubwa, ingawa wanazidi kupungua kwa sababu ya kuhamia nchi nyingine.
Wanafikia 3,500,000 duniani kote, wakiishi katika majimbo 28 kama yafuatavyo.
Huko Lebanoni: Zahleh, Tiro, Tripoli, Sidoni, Sarba (vicariat), Jounieh (vicariat), Zgharta (vicariat), Joubbeh (vicariat), Jbeil, Beirut, Batroun, Baalbeck na Deir el Ahmar na Antelias
Huko Syria: Latakia, Damascus na Aleppo.
Huko Israel: Haifa na Nchi Takatifu.
Katika nchi nyingine: Cyprus, Cairo (Misri), Sudan, Paris (Ufaransa), Sydney (Australia), Buenos Aires (Argentina), Sao Paulo (Brazil), Montreal (Canada), Mexico, Los Angeles na Brooklyn (Marekani).
Marejeo [hariri]
- Moosa, Matti, The Maronites in History, Gorgias Press, Piscataway, NJ, 2005, ISBN 978-1-593-33182-5
- R. J. Mouawad, Les Maronites. Chrétiens du Liban, Brepols Publishers, Turnhout, 2009, ISBN 978-2-503-53041-3
- Kamal Salibi - A House of Many Mansions - The History of Lebanon Reconsidered (University of California Press, 1990).
- Maronite Church. New Catholic Encyclopedia, Second Edition, 2003.
- Riley-Smith, Johnathan - The Oxford Illustrated History of the Crusades (Oxford University Press, Oxford, 1995)
Viungo vya nje [hariri]
- Maronite History Project — a Maronite encyclopedia wiki
- The Druzes and the Maronites under the Turkish Rule from 1840 to 1860 Cornell University Library Historical Monographs Collection.
- Catholic Culture: News — Maronite population discussed
- Tovuti rasmi ya Kanisa la Wamaroni
- Orodha ya majimbo ya Kanisa la Wamaroni
- Maronite Rite diocese based in Sydney, Australia
- Eparchy of Saint Maron of Brooklyn
- Eparchy of Our Lady of Lebanon
- Congregation of the Lebanese Maronites Missionnaries
- The Maronite Monks of Adoration, Most Holy Trinity Monastery — monastery in Massachusetts