Injini ya mvuke

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Muundo wa injini ya mvuke
*Mshale mwekundu: mvuke kutoka jiko unaingia hapa katika chumba cha mvuke *Kilango cha nje: inasogezwa mbele na nyuma na kufungua au kufunga nafasi mbili ambako mvuke unaingia katika silinda upande wa kulia au kushoto ya pistoni *Pistoni inasukumwa mbele na nyuma na mvuke unavyoingizwa katika pande mbili za silinda *Mwendo wa pistoni kupitia konrodi na fitokombo inazungusha gurudumo tegemeo *gurudumo tegemeo ni kubwa na nzito na mwendo wake unasukuma kilango cha nje *mwendo wa gurudumo tegemeo unapelekwa pale unapotakiwa kwa njia ya mkanda
Gari moshi la zamani likitoka Ujerumani mashariki. Hili ni daraja lililo tumia injini hiyo na lilitengenezwa kuanzia mwaka 1942 hadi 1950 na kufanya kazi mpaka mwaka 1988.

Injini ya mvuke ni injini inayotumia nguvu ya mvuke kwa kufanya kazi. Nguvu ya mvuke ni nishati ya joto iliyomo ndani yake. Nishati hii inabadilishwa kuwa mwendo.

Ndani ya mashine maji hupashwa moto kuyageukia kuwa mvuke. Mvuke unaingizwa katika silinda ambako unasukuma pistoni ndani yake. Mwendo wa pistoni unabadilishwa kuwa mwendo wa kuzunguka kupitia fitokombo.

Injini za kwanza za mvuke zilitengenezwa kwa kuendesha pampu za kuvuta maji kwenye migodi ya makaa huko Uingereza. Kuanzia miaka ya 1780 mafundi waliongeza gia na fitokombo na hivyo injini ya mvuke ilitumiwa hata viwandani kuendesha mashine mbalimbali zilizowahi kutumia awali nguvu ya wanadamu au ya wanyama. Mhandisi James Watt anakumbukwa kwa uboreshaji wa injini za kwanza.

Injini ya mvuke ilikuwa uti wa mgongo wa upanuzi wa viwanda na mapinduzi ya viwanda yaliyoendelea kubadilisha maisha na jamii kwanza huko Uingereza, halafu Ulaya na kote duniani.

Injini za mvuke ziliendelea kusukuma magari ya kwanza ama barabarani au kwenye reli. Jina la "gari la moshi" bado linakumbuka asili hii hata kama leo injini za reli ni za diseli au umeme si tena mvuke. Siku hizi injini za mvuke karibu zimepotea kiwandani na pia kwenye magari. Lakini kutokana na uhaba wa mafuta ya petroli unaotarajiwa kwa miaka ujao kuna majarabio mapya kutengeneza magari yanayoendeshwa tena kwa injini za kisasa za mvuke.

Kwa jumla kuna bado matumizi ya aina ya injini ya mvuke katika vituo vya umeme. Mara nyingi umeme hutengenezwa kwa kuchemsha maji ama kwa mafuta au makaa au nyuklia na kutumia nishati ya joto ndani ya mvuke wa maji kuzungusha tabo au jenereta.

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Injini ya mvuke kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.