Hilari wa Poitiers

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ilari wa Poitiers)
Rukia: urambazaji, tafuta
Hilari akiwekwa wakfu kuwa Askofu wa Poitiers.

Hilari wa Poitiers (315 hivi - 367), askofu wa mji huo (kwa Kilatini Pictavium), mwanateolojia, mwanafalsafa na mwandishi, tangu zamani anaheshimiwa na Kanisa Katoliki, Waorthodoksi na Waanglikana kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Wakatoliki wanamheshimu pia kama mwalimu wa Kanisa tangu mwaka 1851, alipotangazwa na Papa Pius IX.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Januari.

Yaliyomo

Maisha [hariri]

Akizaliwa katika familia ya kisharifu, Hilari alivutiwa mapema na falsafa. Akitafakari hatima ya binadamu na kusoma Biblia, aliongokea Ukristo.

Alikuwa baba wa nyumbani alipochaguliwa askofu wa Poitiers mwaka 353.

Mwaka 354 tu alikuja kujua Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli, akaanza kuitetea katika sinodi na mitaguso dhidi ya uzushi wa Waario.

Kwa ajili hiyo mwaka 356 alipelekwa na kaisari Kostanzo II uhamishoni Frigia (leo katika Uturuki).

Akiishi huko miaka mitano iliyofuata alipata nafasi ya kuchimba mafundisho ya mababu wa Kanisa wa mashariki, hata akaweza kuandika juu ya Utatu (De Trinitate). Pia aliandika ufafanuzi wa Zaburi na sehemu nyingine za Biblia, mbali ya tenzi za dini na vitabu vya historia. Kati ya maandishi yake yote, mengi yametufikia.

Alichangia teolojia, k. mf. kuhusu Ufunuo, akiunganisha mitazamo ya Kikristo ya mashariki na ya magharibi.

Aliporuhusiwa kurudi kwao alikuwa mhusika mkuu wa Mtaguso wa Paris (361), na kwa kutumia nguvu na busara pamoja, alifaulu kurudisha Waario wengi katika Kanisa na kueneza Ukristo.

Kutokana na juhudi zake aliitwa “Atanasi wa magharibi”.

Alifariki mwaka 367.

Sala yake [hariri]

Mungu, Baba Mwenyezi, najua vema kuwa huduma kuu inayonipasa kwako katika maisha yangu ni kwamba kila neno na wazo langu liseme juu yako.

Kipawa cha kusema ulichonijalia hakiwezi kunipa furaha kubwa kuliko ile ya kukutumikia kwa kuhubiri na kuonyesha kwa ulimwengu usiokujua, au kwa mzushi anayekukanusha, jinsi ulivyo, yaani Baba, Baba ambaye Mwanae pekee ni Mungu.

Lakini kwa kusema haya, nasema tu ninachotaka kufanya. Ili niweze kukifanya kweli nahitaji kuomba msaada wako na huruma yako, kuomba ujaze upepo tanga nilizozipandisha kwa ajili yako na uzisukume mbele katika mwendo wangu, yaani umvuvie Roho wako katika imani yangu na katika kuiungama, na uniwezeshe kuendelea mahubiri niliyoyaanza…

Acha niseme nawe, Mwenyezi Mungu, ingawa ni mavumbi na majivu tu, acha niseme kwa uhuru kwa kuwa nimefungamana nawe kwa vifungo vya upendo.

Kabla sijakufahamu nilikuwa si kitu. Nilikuwa na bahati mbaya ya kutojua maana ya maisha, nilikuwa sijielewi, nilikuwa tofauti kabisa na jinsi nilivyo. Huruma yako ndiyo iliyonipa uhai…

Muda wote ambao nitaishi na kupumua kwa pumzi uliyonipa, Baba Mtakatifu, Mwenyezi Mungu, nitakiri kwamba tangu milele yote wewe si Mungu tu, bali Baba pia.

Sitakuwa kamwe na kichaa na uovu wa kujifanya hakimu wa uwezo wako usio na mipaka, wala wa mafumbo yako, hata nipendelee wazo langu maskini kuliko yale ambayo dini inakiri juu ya ukuu wako usio na mipaka au imani inafundisha kuhusu umilele wake…

Nakuomba, utunze salama imani hiyo uliyonijalia, na kunifadhilia kwamba muda wote wa maisha yangu niweze tu kuzingatia yale ambayo dhamiri yangu inasema juu yake.

Niweze daima kushika imani niliyoiungama nilipozaliwa upya, Nishike ungamo lake nililolitamka nilipobatizwa kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu.

Niweze kukuabudu wewe, Baba yetu, na kumuabudu Mwanao pamoja nawe; niweze kuwa jinsi Roho wako Mtakatifu anavyotaka niwe, yeye atokaye kwako kwa njia ya Mwanao pekee.

Maandishi [hariri]

  • De Trinitate ndio kitabu chake bora; kilikuwa cha pekee katika Kilatini
  • Tenzi
  • Contra Arianos vel Auxentium Mediolanensem liber
  • Contra Constantium Augustum liber
  • Commentarius in Evangelium Matthaei
  • Tractatus super Psalmos

Viungo vya nje [hariri]

Christian cross.svg Makala hii kuhusu Mkristo huyu bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hilari wa Poitiers kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.