Elizabeti wa Hungaria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mt. Elizabeth wa Hungaria alivyochorwa na msanii wa Bavaria (1520 hivi), Musée de l’Œuvre Notre-Dame, Strasbourg (Ufaransa).

Elisabeth wa Hungaria (kwa Kijerumani Heilige Elisabeth von Thüringen, kwa Kihungaria Árpád-házi Szent Erzsébet), alizaliwa Pressburg, Hungaria (leo Bratislava, Slovakia) tarehe 7 Julai 1207, akafariki tarehe 17 Novemba 1231)[1] alikuwa malkia mdogo wa Thuringia kutoka Ufalme wa Hungaria.

Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki, Walutheri na Waanglikana kama mtakatifu.[2]

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 17 Novemba[3].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alikuwa binti wa Andrea II wa Hungaria na Getrude wa Merania. Kadiri ya mapokeo mengine, Elizabeth alizaliwa katika ngome ya Sárospatak, Hungaria, tarehe 7 Julai 1207,[4][5][6] lakini wengine wanasema alizaliwa Pressburg, alipoishi hadi umri wa miaka 4, alipopelekwa kwenye ikulu ya Thuringia (Ujerumani wa kati), ajiandae kuolewa na mtoto wa mfalme mdogo wa huko ili kuimarisha agano kati ya nchi hizo mbili.

Elizabeti aliolewa na Ludwig IV wa Thuringia akiwa na umri wa miaka 14, akazaa watoto watatu, akabaki mjane alipokuwa na miaka 20. Hapo aliwagawia mafukara mali yake, akajenga hospitali, akawa kielelezo cha matendo ya huruma hadi kifo chake alipokuwa na miaka 24 tu.

Mwaka 1223 Wafransisko walifika nchini wakamuathiri Elisabeth, lakini Ludwig hakuchukizwa na juhudi za mke wake. Ndoa yao iliendelea vizuri hadi mwisho.

Wakati huo padri Konrad wa Marburg alipata kuwa muungamishi wake.

Mwanzo wa mwaka 1226, mafuriko, njaa na maradhi vilipoathiri Thuringia, Ludwig, alikwenda Cremona (Italia) kwa kikao cha bunge la Dola takatifu la Kijerumani kama mwakilishi wa Kaizari Frederick II. Elizabeti alishika uongozi wa nchi akisaidia kwa ukarimu wote wenye shida. Alijenga pia hospitali chini ya ikulu akahudumia mwenyewe waliopokewa huko.

Maisha ya Elizabeti yalibadilika kabisa tarehe 11 Septemba 1227 kutokana na kifo cha Ludwig, akiwa safarini Otranto, kwenda kujiunga na Vita vya msalaba. Alipopata habari, Elizabeti alisema, "Amekufa. Amekufa. Kwangu ni kama kwamba ulimwengu wote umekufa."[7]

Hapo shemeji yake. Heinrich Raspe wa Thuringia alishika uongozi kwa niaba ya mtoto wa kwanza wa Elizabeti, Hermann II wa Thuringia (12221241).

Baada ya mabishano makali kuhusu mahari aliyojiletea, ambayo Konrad wa Marburg aliteuliwa na Papa Gregori IX amtetee, Elizabeti aliacha ikulu ya Wartburg akahamia Marburg huko Hesse, alipojenga hospitali nyingine na kuhudumia maskini.

Kisha kufiwa mumewe, Elizabeti alimwekwea Konrad nadhiri kuu kama za kitawa, akaishi kijumuia na wanawake wachache kama jumuia ya Utawa wa Tatu wa Fransisko wa Asizi.

Konrad alimtendea kwa ukali sana, akimlazimisha kuachana na watoto wake.

Ingawa ndugu yake, askofu Ekbert wa Bamberg, alitaka kumlazimisha aolewe tena, Elizabeti alikataa katakata.[8]

Sala yake[hariri | hariri chanzo]

Bwana, ukitaka kuwa pamoja nami, mimi nataka kuwa pamoja nawe, nisitake kutengana nawe kamwe.

Urithi[hariri | hariri chanzo]

Kanisa la Mt. Elizabeti huko Marburg
Ramani ya kanisa hilo
Kanisa la Mt. Elizabeti huko Grave, Uholanzi

Mapema baada ya kifo chake, miujiza iliripotiwa kutokea kaburini pake. Kwa pendekezo la Konrad, na agizo la Papa, kesi ilianza kati ya walioponywa kiajabu kati ya Agosti 1232 na Januari 1235.

Matokeo ya uchunguzi huo yaliambatanishwa na kitabu kifupi kuhusu maisha yake, na shuhuda za wenzake (Libellus de dictis quatuor ancillarum s. Elisabeth confectus).

Basi, Elizabeti alionekana kustahili atangazwe haraka na Papa Gregori IX kuwa mtakatifu 27 Mai 1235 huko Perugia.

Baadaye vitabu vingi viliandikwa juu yake, maarufu kati ya hivyo ni kile cha Dietrich wa Apolda, Vita S. Elisabeth, kilichoandikwa kati ya 1289 na 1297.

Patakatifu pa Elizabeti pakawa mahali pa hija hasa katika karne ya 15.

Gallery[hariri | hariri chanzo]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Catholic Encyclopedia "St. Elizabeth of Hungary". Catholic Encyclopedia. http://www.newadvent.org/cathen/05389a.htm Catholic Encyclopedia.
  2. "Saint Elizabeth of Hungary". Encyclopædia Britannica. http://www.britannica.com/EBchecked/topic/184889/Saint-Elizabeth-of-Hungary.
  3. Martyrologium Romanum
  4. Albrecht, Thorsten; Atzbach, Rainer (2007). Elisabeth von Thüringen: Leben und Wirkung in Kunst und Kulturgeschichte. Petersberg: Michael Imhof Verlag. p. 7. 
  5. Ohler, Norbert (2006). Elisabeth von Thüringen: Fürstin im Dienst der Niedrigsten. Gleichen: Muster-Schmidt Verlag. p. 15. 
  6. Zippert, Christian; Gerhard Jost (2007). Hingabe und Heiterkeit: Vom Leben und Wirken der heiligen Elisabeth. Kassel: Verlag Evangelischer Medienverband. p. 9.  , 2007), 9.
  7. Rainer Koessling, ed. and trans., Leben und Legende der heiligen Elisabeth nach Dietrich von Apolda (Frankfurt am Main: Insel Verlag, 1997), 52.
  8. Rainer Koessling, ed. and trans., Leben und Legende der heiligen Elisabeth nach Dietrich von Apolda (Frankfurt am Main: Insel Verlag, 1997), 59.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu: