Edward Tingatinga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Edward Saidi Tingatinga (1937 - 1972) alikuwa mchoraji na msanii Mtanzania aliyeanzisha mtindo wa uchoraji wa Tingatinga unaojulikana sana siku hizi na kutafutwa na wapenzi wa sanaa ya Tanzania kote duniani.

Yaliyomo

Maisha kabla ya sanaa [hariri]

Alizaliwa 1937 Umakonde ila haijuulikana kama upande wa Tanzania au upande wa Msumbiji. Vijiji mbalimbali vimetajwa kama mahali pa kuzaliwa kama vile Mindu, Namocheli (leo Nakapanya - vyote katika wilaya ya Tunduru) au Msumbiji. Anasemekana alisoma shule ya msingi ya misioni katoliki Nandembo.

Kati ya 1955 hadi 1959 - habari zikitofautiana - alihamia Dar es Salaam alipopata kazi kama mtumishi wa nyumbani kwa Waingereza. Hao walipoondoka baada ya uhuru Edward alipaswa kujitafutia maisha kwa biashara ndogo mtaani.

Kuchora kwa kujipatia chakula [hariri]

Siku zile alianza kuchora ingawa haijulikani ilikuwa kwa njia gani. Katika miaka ya 60 aliuza picha zake barabarani kwa Shilingi 15 iliyokuwa sawa na bei ya mlo.

Mwaka 1968 baada ya kufunga ndoa na Agata Mataka alikazia uchoraji. Wengine walisema ya kwamba aliendelea na kazi ndogo kwenye hospitali ya Muhimbili ingawa hapa haijulikana alifanya kazi gani kamili na hadi lini.

Mtindo wa Tingatinga [hariri]

Wakati ule alianzisha mtindo wake. Badala ya karatasi alichora kwenye ubao aina ya "ceiling board" iliyokuwa rahisi lakini ni imara. Alikata vipande vya mraba vya futi 2x2. Akishirikiana na wadogo zake alianza kuchora picha za wanyama.

Mnamo mwaka 1970 Wazungu Waskandinavia walianza kutafuta picha zake wakimsaidia kuhudhuria kwenye maonyesho ya biashara ya kwanza ya Dar es Salaam. Mara ghafla Tingatinga alikuwa maarufu, picha zake zikatafutwa bei zikapanda. Picha zake zilikuwa uso wa sanaa ya Tanzania akawa msanii mchoraji maarufu wa Afrika yote.

Kifo na ushirika wa Tingatinga [hariri]

Kwa bahati mbaya Edward Tingatinga aliaga dunia mwaka uliofuata 1972. Alipigwa risasa na polisi kwa kosa akafa na kuzikwa kwenye makaburi ya Msasani Mikoroshoni mjini Dar es Salaam.

Ndugu zake waliendelea na mtindo wake wa uchoraji na wengi walimfuata wakiiga mtindo huo.

Awali walikuwa na matatizo kwa sababu walifukuzwa mara nyingi toka mahali walipofanya kazi. Mwaka 1977 wachoraji Hashimi Mruta, Zaburi Muradi Chimwanda, Amonde, Tedo, Mpata, Amadi Saidi, Mchisa, Abasi, Salum Mussa, Mohamedi Saidi Chilamboni na Fr. J. Linda walunda ushirika wa "TINGATINGA Partnership" wakaiandikisha serikalini. Mwenyekiti wa kwanza alikuwa Omari Amonde.

Washirika walijenga vibanda karibu na Morogoro Stores ambako picha zao ziliuzwa.

Ushirika ulibadilisha jina mwaka 1990 kuwa "Tingatinga Arts Cooperative Society Limited".


Viungo vya Nje [hariri]