Damian de Veuster

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Damian akiwa mkoma mwaka 1888.

Damian de Veuster (3 Januari 1840 - 15 Aprili 1889) alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mtawa wa Shirika la Mioyo Mitakatifu maarufu kama Picpus. Kwa miaka mingi alikuwa mmisionari katika kisiwa cha Molokai (Hawaii), alipojitosa kutumikia wagonjwa wengi wa ukoma waliotengwa huko hata akaambukizwa nao.

Papa Yohane Paulo II alimtangaza mwenye heri mwaka 1995, na Papa Benedikto XVI alimtangaza mtakatifu tarehe 11 Oktoba 2009.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe ya kifo chake[1] au 10 Mei.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Tremelo, nyumba alipozaliwa

Jozef, mtoto wa wakulima, alisoma uganga kwenye chuo kikuu cha Braine-le-Comte, halafu alimfuata kaka yake katika shirika la Picpus.

Akiingia unovisi huko Louvain alijichagulia jina la Damian: baada ya kusomafalsafa na teolojia huko Paris, aliweka nadhiri za daima tarehe 7 Oktoba 1860: baada ya kaka yake kushindwa kutekeleza hamu ya umisionari, Damian aliamua kushika nafasi hiyo.

Mmisionari kwenye visiwa vya Hawaii[hariri | hariri chanzo]

Padri Damian kati ya kwaya ya wasichana ya Kalawao.

Tarehe 19 Machi 1864, alitua katika bandari ya Honolulu, akapewa upadrisho tarehe 24 Mei 1864 kwenye kanisa kuu.

Baadaye akahudumia parokia mbalimbali kwenye kisiwa cha Oahu.

Wakati huo ufalme wa Hawaii ulipokuwa unapitia kipindi kigumu upande wa afya, kutokana na wageni kuleta maradhi mengi ambayo wenyeji hawakuwa na kinga dhidi yake, kama vile kaptura na kaswende, pamoja na ukoma.

Mfalme Kamehameha IV aliwatenga wakoma wa ufalme mzima katika maeneo maalumu kaskazini mwa kisiwa cha Molokai.

Padri Damian mwaka 1865 alimuomba askofu Luigi Maigret, ruhusa ya kuhamia Molokai.

Kituo cha mauti[hariri | hariri chanzo]

Padri Damian mahututi.
Mt. Marianne Cope akiwa amesimama karibu na maiti.
Wakoma wakiomboleza kwenye kaburi la Damian siku ya mazishi yake, mnamo Aprili 1888.

Mwaka 1870 padri Damiano alishika nafasi yake kama padri na mganga wa wakoma na tarehe 10 Mei 1873 alifika kwenye kituo cha Kalaupapa walipokuwepo wakoma 600 na zaidi.

Askofu Maigret alimtambulisha Damiano kwa wagonjwa akisema atakuwa kama baba yao na kuwa tayari kuwa kama wao: "kuishi na kufa pamoja nao".

Kitu cha kwanza alijenga kanisa na kuanzisha parokia ya Mtakatifu Filomena.

Mbali ya huduma za kipadri, alitibu madonda, alijenga nyumba, alitengeneza vitanda na majeneza na kuchimba makaburi.

Chini yake kituo hicho cha mauti kilichosahauliwa na serikali kilichangamka na kujipatia sheria, pamoja na kujenga nyumba bora, shule na kuanzisha mashamba.

Mfalme David Kalakaua alipoamua kumpa Damian nishani, malkia mdogo Lydia Liliuokalani alimtembelea akaguswa hata akapasha habari kwenye vyombo mbalimbali, hivi kwamba Damian alikuja kufahamika Marekani na Ulaya.

Kifo[hariri | hariri chanzo]

Mwezi Desemba 1884 Damian, akinawa miguu kwa maji ya moto, hakusikia maumivu: ndivyo alivyotambua ameambukizwa ukoma.

Hata hivyo mpaka kufa aliendelea kufanya kazi alizozipanga, akisaidiwa na watu 4 waliojitolea: padri Louis Lambert Conrardy, sista Marianne Cope, wa shirika la Wafransisko wa Syracuse, askari mstaafu Joseph Dutton na nesi James Sinnett.

Padri Damian alifariki kwa ukoma mwaka 1889, akiwa na umri wa miaka 48 anni akazikwa huko Louvain, karibu na kijiji alikozaliwa.

Heshima baada ya kifo[hariri | hariri chanzo]

Mahatma Gandhi, baba wa taifa la India alimtaja Damian kama kielelezo chake katika kupigania uhuru wa nchi hiyo.

Aliandika: "Siasa na ulimwengu wa magazeti vinaweza kujivunia mashujaa kadhaa, lakini wachache wanaweza kufananishwa na padri Damian wa Molokai. Inafaa kuchungulia vyanzo vya ushujaa wake".

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

reflist

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Gavan Daws, Holy Man: Father Damien of Molokai, University of Hawai'i Press, 1994.
  • Hilde Eynikel, Molokai: The Story of Father Damien, Alba House: 1999.
  • Richard Stewart, Leper Priest of Moloka'i: The Father Damien Story, University of Hawai'i Press: 2001.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  1. Martyrologium Romanum