Calvin

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Calvin.

John Calvin, kwa Kifaransa Jean Calvin au kizamani Jehan Cauvin (10 Julai 1509 - 27 Mei 1564) alikuwa mwanateolojia toka Ufaransa aliyeanzisha madhehebu maalumu ya Ukristo katika karne ya 16 akiunga mkono Matengenezo ya Kiprotestanti yaliyoanzishwa na Martin Luther nchini Ujerumani, lakini kwa kutofautiana naye katika mafundisho mbalimbali.

Mwalimu huyo aliandika kitabu akiweka mkazo kuelezea jinsi mapenzi ya Mungu yalivyokwishaamua juu ya maisha ya mwanadamu kabla ya huyo kuamua mwenyewe.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Kisha kusoma kwa maelekeo ya Renaissance na kuwa mwanasheria, alijitenga na Kanisa Katoliki mwaka 1530 hivi.

Kutokana na mapigano ya kidini yaliyozuka Ufaransa, alikimbilia Basel, Uswisi, alipochapa toleo la kwanza la kitabu chake maarufu zaidi, Institutiones Christianae Religionis mwaka 1536.

Mwaka huohuo William Farel alimualika Geneva, lakini halmashauri ya mji ilikataa kutekeleza mapendekezo yao ikawafukuza.

Hapo Martin Bucer alimuita Calvin huko Strasbourg, alipoongoza Waprotestanti waliokimbia Ufaransa, akiendelea kuhimiza matengenezo mjini Geneva, ambapo hatimaye alikaribishwa kurudi kama kiongozi wa dini.

Huko Calvin aliingiza miundo mipya ya uongozi na aina mpya za liturujia, akishinda upinzani wote.

Wakati huo alifanya halmashauri ya mji imuhukumu adhabu ya kifo Michael Servetus, Mhispania aliyetazamwa na wote kama mzushi.

Baada ya wakimbizi wengi kuhamia Geneva, uchaguzi mpya uliwezesha kufukuza toka mji huo waliompinga Calvin.

Miaka yake ya mwisho aliitumia kueneza matengenezo yake kote Ulaya, akiacha nyuma yake madhehebu ya Reformed, Congregationalists na Presbyterians, ambayo leo yana jumla ya waamini zaidi ya milioni 80, wengi wao wakiwa wameunganika katika "World Communion of Reformed Churches".

Calvin alitetea kwa ukali misimamo yake na kusababisha mabishano mengi.

Pamoja na Institutiones, aliandika vitabu vingi vya ufafanuzi wa Biblia, teolojia na maungamo ya imani, bila kuacha kuhubiri wiki nzima.

Calvin aliathiriwa na Agostino wa Hippo hata kukazia mafundisho yake kuhusu uteule kutokana na imani ya kwamba wokovu wa binadamu unamtegemea Mungu tu.

Tathmini[hariri | hariri chanzo]

Tofauti na Luther, Calvin alijaribu moja kwa moja kujenga kanisa jipya kwenye msingi wa Biblia.

Hakupenda kuchukua urithi wowote wa Kanisa Katoliki, akaunda kila kitu upya kufuatana na jinsi alivyoelewa Biblia.

Katika utawala alikataa cheo cha uaskofu akaona kanisa liongozwe na wazee wa kuchaguliwa. Kutokana na neno wazee katika lugha ya Agano Jipya (Kigiriki) "presbyuteroi", kanisa lake linaitwa pia la "Wapresbiteri". Wafuasi wake huitwa pia "Wareformati" (to reform = kutengeneza upya). Maana yake walikataa desturi zote wasizoziona katika Biblia, wakati Luther alizikubali zile alizoziona hazipingi Biblia.

Katika ibada zao, Wareformati wanakataa altari, picha za kupamba kanisa au kuimba liturujia, wakati ibada ya Kilutheri ni Misa ya Kikatoliki iliyobadilishwa kufuatana na mawazo ya Luther. Katika jambo hilo hawakupatana na ndiyo sababu kwa muda mrefu Walutheri na Wareformati walishindwa kuwa na ibada za pamoja, lakini siku hizi wanaelewana.

Mafundisho hayo kutoka Uswisi yalienea katika nchi kama Ufaransa, Uskoti na Uholanzi. Hata Wamoravia walichukua sehemu ya mafundisho ya Wareformati, hasa juu ya Chakula cha Bwana, wakimfuata Luther katika mambo mengine.

Afrika Kusini urithi wa kidini wa Makaburu ni wa Kireformati kwa sababu babu zao walitokea Uholanzi na Ufaransa.

Vilevile ni wamisionari kutoka Uswisi na Uskoti walioanzisha mapema makanisa ya Kipresbiteri Malawi, Kenya na Afrika Magharibi.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Institutio christianae religionis, 1597

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]