Basutoland

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bendera isiyo rasmi ya nchi ya Basutoland

Basutoland ilikuwa jina la kikoloni la nchi ya Lesotho katika Afrika ya Kusini.

Eneo lililokaliwa kiasili na Wasan likaingiliwa na Wabantu tangu karne ya 16. Kuanzia miaka ya 1820 chifu Moshweshwe alikusanya watu mbalimbali waliowahi kukimbilia huko mbele ya mashambulio ya Wazulu akaunganisha nchi mara ya kwanza.

Baada ya vita mbalimbali dhidi ya Makaburu Moshweshwe aliomba msaada wa Uingereza na mwaka 1868 eneo lake likawa eneo lindwa chini ya Waingereza. Baada ya kifo cha Moshweshwe I eneo lake likaunganishwa na koloni ya rasi (Cape Colony) bila kibali cha wenyeji waliopinga utawala wa serikali ya kikoloni kwa vita ya msituni. Serikali ya Cape Town ilichoka ikarudisha eneo la Basutoland kwa serikali ya London likawa tena eneo lindwa.

Serikali ilikuwa mkononi mwa afisa mkazi Mwingereza pamoja na machifu wenyeji. Wakati wa vita ya Waingereza dhidi ya Makaburu Basutoland ilikaa nje ya mapigano. Wakati wa kuundwa kwa Umoja wa Afrika Kusini majaribio ya kuunganisha nayo Basutoland humo yalishindikana kwa sababu ya upinzani wa wenyeji. Hivyo Basutoland ilibaki kama eneo la pekee ndani ya Afrika Kusini.

Tangu 1959 nchi ikapewa katiba na 4 Oktoba 1966 Basutoland ikawa nchi huru iliyobadilisha jina kuwa Lesotho.