Basil wa Caesarea

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Picha katika ukuta wa kanisa kuu la Ohrid inayomuonyesha Basili Mkuu akigeuza vipaji vya ekaristi.
Picha takatifu ya Kirusi ya Mt. Basili.

Basili wa Kaisarea (Kaisarea wa Kapadokia, leo Kayseri, nchini Uturuki, takriban 329 – Kaisarea wa Kapadokia, 1 Januari, 379) alikuwa mmonaki, halafu askofu wa mji huo (mkoa wa Kapadokia, leo nchini Uturuki).

Ni mmojawapo kati ya Mababu wa Kanisa muhimu zaidi. Ndiyo sababu anaitwa Basili Mkuu (kwa Kigiriki Βασίλειος ο Μέγας).

Alitangazwa kuwa mtakatifu punde baada ya kifo chake, na mwaka 1568 Papa Pius V alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 2 Januari.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Asili na ujana[hariri | hariri chanzo]

Basili alizaliwa katika familia tajiri ya mhubiri maarufu Basili Mzee na ya Emelia wa Kaisarea huko Caesarea Mazaca. Wote wawili walijulikana kwa imani yao (Oratio 43.4, PG 36. 500B).

Familia yao ilikuwa na watoto 10, waliosaidiwa malezi na bibi wa Basili, Makrina Mzee. Babu yake alikuwa mfiadini. Wote wawili wanaheshimiwa kama watakatifu, kama vile Basili na watoto wengine 4: dada yake Makrina Kijana aliyekuwa mmonaki, na ndugu zake Petro wa Sebaste aliyekuwa askofu na mwanateolojia huko Armenia, Naukratios aliyekuwa mkaapweke, na hasa Gregori wa Nisa ambaye aliyefanywa na Basili kuwa askofu wa Nisa akaandika vitabu bora kuhusu teolojia na maisha ya Kiroho.

Basili alikuwa na vipawa vya pekee: akili kali, wema mkubwa, uwezo wa kupanga na kufanikisha mambo, nguvu katika utendaji, busara na kiasi katika yote. Ni kati ya wanakanisa kamili zaidi.

Bado mtoto alihamia mkoa wa Ponto hadi alipofiwa baba yake ambapo akarudi Kaisarea ili kupata wlimu. Huko alikutana na Gregori wa Nazianzo, akawa rafiki yake maisha yake yote.

Wote wawili walikwenda kusoma Konstantinopoli, halafu kwa miaka sita Athens, walipokutana na atakayekuwa kaisari Juliano Mwasi. Ndiko alikoanza kufikiria maisha ya Kikristo hasa. Hata hivyo hakuacha kutia maanani elimudunia, aliyokuwa nayo kwa wingi, hasa kwa ajili ya malezi ya vijana, ambao daima aliwashughulikia sana.

Alipohama Athens mwaka 355 hivi, Basili alifanya kwa muda mfupi kazi ya wakili na mwalimu wa kuhubiri huko Kaisarea, lakini mwaka uliofuata alibadili maisha kisha kukutana na askofu Eustathius wa Sebaste.

Umonaki[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kupata ubatizo, Basili alisafiri tena (357) kwenda Misri, Palestina, Syria na Mesopotamia ili kufahamu zaidi maisha ya kiroho na umonaki.

Ingawa aliguswa na utakatifu wa wamonaki aliokutana nao huko, kipeo cha ukaapweke hakikumvutia zaidi. Badala yake alielekea maisha ya kijumuia. Hivyo baadaye alirekebisha umonaki usiwe mbali mno na watu wa kawaida, bali uathiri maisha yao kwa roho ya Kikristo.

Kiongozi halisi katika njia ya Mungu, hakuruhusu malipizi ya ajabuajabu, bali alidai utekelezaji wa matendo ya upendo.

Kisha kugawa mali zake kwa mafukara alikwenda kwa muda mfupi kuishi upwekeni karibu Neokaisaria mtoni Iris, lakini mwaka 358 alianza kupokea wafuasi, mmojawao ndugu yake Petro. Pamoja naye alianzisha monasteri huko Arnesi kwenye mkoa wa Ponto.

Huko walijiunga hata mama yake, dada yake Makrina na wanawake wengine, wakijitoa kusali na kutekeleza matendo ya huruma.

Ni huko kwamba Basili aliandika vitabu vyake kuhusu umonaki (Kanuni mbili) vilivyoathiri Kanisa lote hadi leo, hata akaitwa "baba wa umonaki wa mashariki".

Mwaka 358 alimualika Gregori wa Nazianzo ajiunge naye, halafu kwa pamoja walitunga Filocalia, mkusanyo wa maandishi bora ya Origen. Baadaye Gregori akarudi kwao.

Basili alishiriki Mtaguso wa Konstantinopoli wa mwaka 360 alipokubali neno "homoiousios" kama sahihi kuelezea Yesu ni "kama" Mungu Baba, si "sawa" wala si "tofauti" naye. Baada ya kulaumiwa na askofu wake, Dianius wa Kaisarea, aliacha mtazamo huo akashika moja kwa moja Kanuni ya imani ya Nisea.

Daraja takatifu[hariri | hariri chanzo]

Picha takatifu ya Maaskofu watakatifu watatu: Basili Mkuu (kushoto), Yohane Krisostomo (katikati) na Gregori wa Nazianzo (kulia) kutoka Lipie, Historic Museum huko Sanok, Poland.

Mwaka 362 Basili alipewa daraja takatifu ya ushemasi kwa kuwekewa mikono na askofu Meletius wa Antiokia.

Aliitwa na Eusebius arudi kwao, akapewa upadirisho mwaka 365.

Miaka iliyofuata Basili na Gregori walishindana na uzushi wa Ario ulioenea Kapadokia. Katika midahalo wakawa washindi.

Hivyo Basili alikabidhiwa usimamizi wa mali ya dayosisi ya Kaisarea. Eusebius akamuonea kijicho akamruhusu arudi upwekeni. Lakini Gregori alimshauri ashike tena nafasi yake kama kiongozi halisi wa jimbo hilo.

Mwaka 370 Eusebius alifariki, na Basili alichaguliwa mwandamizi wake akapewa uaskofu tarehe 14 Juni 370. Kama askofu wa Kaisarea akawa pia askofu mkuu mwenye majimbo 5 chini yake.

Hapo alikataa katakata mashinikizo ya kaisari aliyetaka aunge mkono uzushi wa Ario, akajitosa kwa ajili ya maskini, wezi na makahaba, akilaumu hadharani walioshindwa kutoa hukumu kwa haki.

Alianzisha mtaa wenye majengo kwa ajili ya mafukara, wageni na wagonjwa, uliokuja kuitwa Basiliade. Ulikuwa na hospitali, shule na viwanda.

Hata katika makanisa mengine yaliyokuwa chini yake alianzisha makimbilio kwa shida yoyote ile.

Kama askofu, alianzisha maisha ya pamoja katika “jamaa” kwa lengo la kushika kikamilifu udugu wa Kiinjili kama katika Kanisa la mwanzoni.

Tofauti na monasteri za Pakomi, zilizofikia kuwa na watawa elfu, jamaa hiyo haikuwa na idadi kubwa wala ngome; tena haikuwa jangwani, bali karibu na mji wa Kaisarea wa Kapadokia.

Akiwa askofu huko alisisitiza uhusiano na Kanisa: alitaka watawa wa kiume na wa kike wawe chachu inayofanya Wakristo wenzao wote wafuate utakatifu wa wito wao. Tena aliwakabidhi shughuli mbalimbali kama vile kuhubiri na hasa kuhudumia wenye shida.

Mtindo huo ulisisitiza ushirikiano kati ya ndugu kuliko uongozi wa abati na miundo mikubwa.

Tofauti na unyofu wa wamonaki wa jangwani, alitia maanani masomo ya kidini, na hasa maandishi ya Origene.

Mpaka leo kanuni zake zinaongoza karibu monasteri zote za mashariki, na kwa njia hiyo makanisa ya Kiorthodoksi kwa kuwa kwao maaskofu kwanza ni wamonaki, nao wanaelekeza Wakristo wote kufuata mifano yao.

Alirekebisha pia liturujia na kuhimiza waamini wapokee Ekaristi kila siku.

Mhubiri mwenye nguvu, alishambulia uroho wa matajiri na ulegevu wa Wakristo wasiotimiza wajibu wao.

Alipanga maisha ya Kanisa bila kukubali serikali iyaingilie.

Alipodaiwa na mjumbe wa kaisari Valens alegeze msimamo wake dhidi ya Ario, Basili alimjibu, "Labda wewe hujawahi kuhusiana na askofu yeyote." Baada ya jibu hilo kaisari alikwenda kushiriki misa yake akampe eneo kwa ajili ya Basiliade. Tukio hilo lilisaidia kuonyesha mipaka kati ya mamlaka ya serikali na ile ya Kanisa.

Basili aliwasiliana pia na Papa Damaso I ili Kanisa la Roma litumie mamlaka yake kulaani uzushi wa Ario,mashariki kama magharibi.

Lakini hakuishi kirefu kutosha aone ushindi wa imani sahihi aliyotetea. Juhudi zake zilimmaliza tarehe 1 Januari 379, akiwa na umri wa miaka 49 tu.

Maandishi[hariri | hariri chanzo]

 • On the Holy Spirit
 • Refutation of the Apology of the Impious Eunomius
 • Refutation (vitabu 3 vya kwanza tu)
 • Hexaëmeron
 • Ufafanuzi wa Zaburi
 • Moralia
 • Asketika
 • Barua 300

Tafsiri ya Kiswahili[hariri | hariri chanzo]

 • MT. BASILI WA KAISARIA, Kanuni za kimaadili – tafsiri ya Familia za Maamkio – Mapanda - ed. Ndanda Mission Press – Ndanda 2005 – ISBN 9976-63-674-X

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

Kwa Kiswahili[hariri | hariri chanzo]

•PADRE FRIDOLIN, Maisha ya Mtakatifu Makrina - ed. N.M.P. - Ndanda

Kwa lugha ntyingine[hariri | hariri chanzo]

 • Bebis, George (Fall-Winter 1997). "Introduction to the Liturgical Theology of St Basil the Great". Greek Orthodox Theological Review 42 (3-4): 273–285. ISSN 0017-3894. 
 • The New Encyclopaedia Britannica, 15th edition, v. 1. London: Encyclopaedia Britannica. 
 • Hildebrand, Stephen M. (2007). The Trinitarian Theology of Basil of Caesarea. Washington, D.C.: Catholic University of America Press. ISBN 978-0-8132-1473-3. 
 • Keary, Charles Francis (1882). Outline of Primative Belief Among the Indo-European Races. New York: C. Scribner's Sons. 
 • Meredith, Anthony (1995). The Cappadocians. Crestwood, NY: St. Vladimir's Seminar Press. ISBN 0-8818141-112-4. 
 • Murphy, Margaret Gertrude (1930). St. Basil and Monasticism: Catholic University of America Series on Patristic Studies, Vol. XXV. New York: AMS Press. ISBN 0-404-04543-x. 
 • Rousseau, Phillip (1994). Basil of Caesarea. Berkeley: University of California Press. ISBN 0-520-08238-9. 
 • Ruether, Rosemary Radford (1969). Gregory of Nazianzus. Oxford: Oxford University Press. 
 • Silvas, Anna M. (Septemba 2002). "Edessa to Cassino: The Passage of Basil's Asketikon to the West". Vigliae Christianae (Brill Academic) 56 (3): 247–259. doi:10.1163/157007202760235382. ISSN 042-6032. 
 • Corona, Gabriella, ed. (2006). Aelfric's Life of Saint Basil the Great: Background and Content. [1] Anglo-Saxon Texts 5. Cambridge: D.S. Brewer. ISBN 9781-84384-095-4. 

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Christian cross.svg Makala hii kuhusu Mkristo huyu bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Basil wa Caesarea kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.