Agnes wa Asizi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Agnesi wa Asizi)
Klara na wafuasi wake walivyochorwa ukutani mwa kanisa la San Damiano, Assisi (Italia).
Basilika la Mt. Klara, Assisi.

Agnes wa Asizi (Assisi 1197 au 1198 - Assisi 16 Novemba 1253) alikuwa mdogo wa kwanza wa Klara wa Asizi.

Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama mtakatifu bikira.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alikuwa binti wa pili kati ya watatu wa Favarone wa Offreduccio Scifi; mama yake Ortolana alikuwa wa ukoo wa kisharifu wa Fiumi na binamu yake Rufino ni mmmojawapo kati ya wenzi watatu wa Fransisko.

Alimfuata dada yake Klara wiki mbili tu baada ya huyo kukimbia nyumbani (18 Machi 1212) ili atawe nyuma ya Fransisko wa Asizi, mwanzilishi wa Ndugu Wadogo. Pamoja, walishinda upinzani mkali wa baba yao na ndugu wengine.

Ndipo Fransisko alipowahamishia kwenye kikanisa cha San Damiano karibu na Assisi ambacho alikuwa amekarabati kwa mikono yake.

Baada ya wanawake wengine kujiunga, monasteri yao ikawa asili ya Utawa wa Mt. Klara.

Mwaka 1219 Agnes aliteuliwa na Fransisko kama abesi wa monasteri ya Monticelli, karibu na Firenze, ambayo ikazaa monasteri nyingine Italia kaskazini, kama vile Mantova, Venezia na Padova.

Mwaka 1253 Agnes alirudishwa San Damiano wakati wa kihoro cha dada yake, akamtumikia hadi mwisho.

Mwaka huohuo, mwenyewe alifariki, tarehe 16 Novemba.

Kwa wakati huo mama yao Ortolana, na mdogo wao Beatrice, walikuwa wameshafariki katika monasteri hiyohiyo.

Heshima baada ya kifo[hariri | hariri chanzo]

Masalia ya Agnes yanatunzwa katika Basilika la Mt. Klara mjini Assisi, yalipohamishiwa pamoja na yale ya Waklara wote wa kwanza.

Papa Benedikto XIV aliruhusu Wafransisko kuadhimisha sikukuu yake kila tarehe 16 Novemba.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Bartoli, Marco. Chiara d'Assisi. Rome 1989: Instituto Storico dei Cappuccini.